Saturday, October 30, 2021

ADILI NA NDUGUZE -sehemu ya 4

 

ADILI NA NDUGUZE - 4

  


Simulizi : Adili Na Nduguze 

Sehemu Ya Nne (4)




Ulimwengu uliajabia dola yao kwa ushujaa wa askari na kwa busara ya mawaziri wao. Walakini, juu ya sifa hizo, mfalme, malkia na raia walikuwa waabudu mizimu. Mizimu yao ilikuwa miti. Miti yenyewe ni ile iliyogeuka mawe ukutani. Kabwere, Mganga na imamu wa mizimu hiyo alivuta mioyo ya watu wote. Siku moja asubuhi mfalme na malkia walikwenda katika halmashauri zao, kila mmoja akakaa juu ya kiti chake. Madiwani walikuwa wamewazunguka kabla ya kuanza kazi zao za desturi; mtu mmoja ambaye hakujulikana alikotoka alisimama ghafula mbele ya mfalme akajitangaza kuwa aliitwa Mrefu.



Mrefu alikuwa mwujiza katika viumbe. Alikuwa na miguu mikubwa na mapaja manene, kiuno cha utambo na kifua kipana na shingo yake ndefu ilichukua kichwa kikubwa. Mabega yake ya mraba yalining'iniza chini mikono iliyokuwa na nguvu kama manjanika. Kwa kimo cha kukithiri alitembea baharini bila ya kuguswa na maji magotini, akafikia vilele vya milima kwa mikono yake. Aliweza kukamata ndovu chini au nyangumi baharini akamwoka kwa jua mbinguni. Sauti yake ilikuwa kama radi kwa wepesi wake wa ajabu wa kuzunguka dunia nzima kwa sekunde moja, alionekana kama kiumbe kilichoumbwa maalum kuokoa kitu motoni, baharini au katika hatari nyingine.



Mrefu alimwambia Tukufu kuwa mfalme ni naibu wa Mungu duniani. Kwa hiyo , ufalme ni amana kubwa. Amna hiyo ilitaka uangalifu mkubwa kwa sababu ni dhima bora iliyowekwa mikononi mwa wanadamu. Wajibu wa kwanza wa mfalme ni kuwa mwadilifu katika matendo yake. Kila tendo, jema au baya , ni mfano kwa raia wake. Kwa sababu ya maisha ya milele ibada ya mizimu ilikuwa maangamizi , na uimamu wa kabwere ujinga mtupu.



Tukufu alimtazama msemaji akasema kwa ukali, "Nini kilichokujusurisha kusema upuuzi, Mrefu? Kama kwa sababu ya urefu ubongo wako umeyeyuka kwa jua, kaa kitako chini ya kivuli cha mizimu yetu utaburudika. Kama umerogwa, Kabwere atawakomesha waliokuroga. Riziki ya wanadamu hutoka mimeani. Kwa sababu hiyo, mimi na kaumu hii twaabudu miti. Funga ulimi wako, bwana. Usipofunga hasira ya mizimu itakuwa juu yako. Tafadhari jiokoe."



Mrefu alionya , "Hapana haja ya jibu la haraka. Tumia wakati upendao wa kufikiri. Nimesema neno la Mungu. Mungu hachelei tisho la mwanadamu, kazi ya mikono yake mwenyewe. Neno takatifu gumu kufahamika, lakini lina tija kwa wajisumbuao kulifasiri. Kila msaada nitakupa wa kulifasiri."



Tukufu hakujali onyo hili akaamrisha kushikwa kwa Mrefu aliyekuwa hasogeleki wala hashikiki. Uwezo usio hadhari ni kileo kibaya sana. Siku ile ilikuwa ya tisho na msiba, ole na maangamizi makubwa. Kwa laana iliyotamkwa na Mrefu, miji mingine yotw ya dola hii iligharika, na kila kiumbe kilichokuwa na maisha katika Fahari kiligeuka jiwe.



Hili lilipotokea Mwelekevu alikuwa darini anachungulia nje kwa dirishani. Toka pale aliweza kumwona Mrefu na kusikia maneno yake. Hakupendelea kushindwa kwa baba yake. Hapana mtoto apendeleaye hili . Walakini, mapendeleo yakiachwa mbali, nuru ya fikira humulika mno siku zote juu ya kweli kuliko uongo, na juu ya haki kuliko dhuluma. Nuru hii ndiyo iliyomwokoa Mwelekevu katika maangamizi yale ya kutisha. Na tangu siku ile aliamini kuwa onyo la bure likikataliwa huleta majuto ya milele.



Hayo yalipokwisha jiri Mrefu alimpa binti mfalme chuo kitakatifu alichomsifia kuwa bora kuliko vitabu vyote vya duniani vikichanganywa pamoja. Kwa matumizi mengine, Mrefu aliomba mkomamanga uote. Mkomamanga huo ulizaa komamanga moja kila siku. Kila chembe katika komamanga hilo ilikuwa chakula na kinywaji mbalimbali. Kwa mti ule wa ajabu binti mfalme aliweza kuishi maisha ya faraja. Mwisho alionywa kuwa siku ya kuona mti ule umezaa matunda mawili ajue Adili, mwokozi wake amefika. Hilo ndilo lililomjulisha siku ile kuwa mgeni wake alikuwa si mtu mwingine ila Adili.



Usemi wa binti mfalme ulimwonyesha Adili kuwa turufu huenda kwa mchezaji siku zote. Laiti asingalikwenda wenziwe walikoogopa akatafuta tafuta asingalikutana na bahati ambayo hakutazamia kuja katika ndoto zake . Alishukuru akamchukua binti mfalme pamoja na tunu bora alizoweza . Katika tunu zake yalikuwemo pia makomamanga mawili ya ajabu. Hayo yalikomesha kiu na njaa katika merikebu yao kwa muda wa siku kadha wa kadha.



Adili aliyageukia manyani akayauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea. Manyani yaliziba nyuso zao kwa viganja vya mikono yao kwa aibu.



Kutoswa kwa Adili



Nahodha na mabaharia walimshangilia Adili kama mtu wa bahati ya peke yake, na kuwa mtu mwingine yeyote kati yao angalifuatana naye kwenda walikoogopa , asingalikutana na bahati ile kubwa. Adili aliwashukuru wote akisema kwa furaha mkulima alikuwa mmoja siku zote, lakini walaji wengi. Pato lake lilikuwa pato lao vile vile.



Aligawa tunu zake katika mafungu manne yaliyokuwa sawasaw. Fungu la kwanza alimpa nahodha, na kila ndugu yake akapata fungu moja. Fungu lililobaki lilikuwa lake mwenyewe. Hili aliligawa tena katika mafungu mengi, kila baharia akapata sehemu yake. Isipokuwa ndugu zake, watu wote chomboni walishukuru wakamwombea heri. Nyuso za ndugu zake zilionekana zimekunjamana na macho yao yaliiva. Alifahamu hawakuridhika kwa sababu ya choyo chap kikubwa.



Aliwataka radhi akawaambia kuwa ingawa mafungu yao yalikuwa madogo, lakini wao walikuwa ndugu zake. Mali yake ilikuwa mali yao katika maisha na mauti. Palikuwa hapana sababu ya kukasirika.


Wakati alipokuwa akisema na ndugu zake stahani, Mwelekevu alikuwa amekaa ngamani na jahazi inakwenda moto mmoja.


Sasa Hasidi na Mwivu walimwuliza Adili nia aliyokuwa nayo juu ya bibi yule mzuri aliyempata katika mji wa Mawe.


Aliwajibu kuwa wakifika salama janibu nia yake ilikuwa kumwoa.


Hasidi aliomba kuwa angalifurahi kama angalimwoa yeye bibi yule.


Mwivu kadhalika alinasihi kuwa angalipenda kumwoa yeye.


Kwa kusikitika, lakini kwa imara kabisa, Adili alijibu kuwa kama walitaka neno jingine lolote katika miliki yake angaliwapa, ila hakufikiri kuacha mkono wa bibi yule kuguswa na mru mwingine katika ndoa ila yeye mwenyewe. Wao walimtaka lakini yeye alimpenda zaidi. Walakini wakirudi Janibu atawatafutia mabibi wawili wazuri. Gharama yote itakuwa juu yake. Arusi zao na yake zitakuwa siku moja , fungate na furaha yao itakuwa moja.



Ndugu zake walihoji kama mume mmoja katika Afrika aliweza kuoa wake wengi, na mke mmoja katika Asia alipata kuolewa na waume kadhaa, isingalikuwa vema kama ndugu watatu wa Janibu wangalishiriki uzuri wa mke mmoja?



Adili alibisha kuwa kulikuwa na mambo yaliyofaa na yaliyokuwa hayafai kushiriki. Ndoa ilikuwa jambo moja katika yale yaliyokataa ushirika. Ushirika katika ndoa ulipasa wanyama na ndege. Mtu alitukuzwa mno kuliko mnyama. Huchukiza akiishi katika maisha duni. Ilipasa watu wa wakati ujao katika Afrika, Asia na Janibu kuishi katika maisha bora ya utu, na kuifanya dunia mahali pa kiasi, sio ulafi na uchafu. Mwanamume hakukusudiwa kuwa fahali wa kila mtamba, wala mwanamke kuwa tembe la kila jogoo.



Ushirika wa ndoa ulipofanikisha na uvundo wa kuchukiza duniani, ndugu zake walinyamaza kimya kama walioridhika, lakini moto ulikuwa ukiwaka mioyoni mwao. Usiku Adili alipokuwa amelala na jahazi inakwenda mbio kwa pepo za omo, ndugu zake walikuwa macho. Mawazo mabaya hurusha usingizi. Kuzinduka kwake usingizini Adili alijiona amechukuliwa hangahanga. Kufumbua macho aliona ndugu zake wamemfunga kifati. Mmoja alimshika kichwani na mwingine miguuni. Koo yake ilisongwa sana. Aliwauliza kwa pumzi nyembamba aliyoweza kuvuta neno walilotaka kumtendea.



Alijibiwa , "Huss, fedhuli wee! Wauliza neno ulijualo. Koma sasa! Tumesalitika na mapenzi ya mwanamke aliyeko chomboni. Tumekushauri kumwoa shirika. Umekataa. Huna budi kufa."


Alitoswa baharini kama kitu kilichokuwa hakifai.



Adili aliyageukia manyani akauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea. Manyani yaliziba nyuso kwa viganja vya mikono yao kwa aibu.



Wokovu wa Adili



Adili alipotupwa alizama kama jiwe katika kilindi cha bahari ambacho urefu wake haukutambulikana. Viwambo vya masikio yake vililia akadhani maji yalipenya sikio hata sikio, na mianzi ya pua yake ilijaa maji yaliyozuia pumzi. Macho yake yalipofumbuka vimemeta kama nyota mbinguni vilionekana katika maji, vimemeta hivyo vilifanywa na mtikiso wa mwili wake. Kutumbukia baharini usiku wa giza ni hatari ya kutisha sana.



Kasi ya kutupwa ilipokoma alijitatamua akakata vifungo vya kamba iliyotatizwa mwilini mwake. Sasa mikono na miguu yake ilianza kufanya kazi. Nusu ya nguvu yake ilikuwa imetumika, lakini matumaini yake yalikuwa kamili. Adili alikuwa si mkata tamaa, na kabla pumzi yake haijakwisha alikusudia kuebuka. Jaribu lake lilikutana na fanaka, maana kabla moyo wale haujakoma alijiona anaelea juu ya bahari. Aliinua kichwa juu ya maji akahema kwa nguvu kama gari moshi. Kulipopambazuka alikuwa katika bahari iliyoghadhibika kwa dhoruba kali, na halibyake ilikuwa taabani. Kutazama hatari usoni kunavunja moyo wa mtu lakini alijikaza kiume.



Mara ile palikuja ndege aliyekuwa na umbo la kutisha akamwopoa Adili majini. Kama koleo, miguu ya ndege ilimshika kwapani akaruka naye. Fikiri wewe mwenyewe hofu aliyokuwa nayo Adili. Binafsi yake alijiona ameokoka kuliwa na papa akawa chakula cha tai. Ndege mwenyewe alipaa juu mpaka Adili alipotelewa na fahamu. Fahamu yake ilipomrudia alijiona katika nyumba kubwa sana iliyokuwa nzuri ajabu. Wasichana warembo na walio changamka walikuwa watumishi katika nyumba hiyo . Miongoni mwao palikuwa na bibi mmoja aliyejipambanua kama malkia, huyo alikaa juu ya kiti cha enzi kilichopambwa na majohari mbalimbali. Rangi ya mavazi yake ilikuwa fua, na kichwani alivaa taji lililopigisha moyo mshindo kwa uzuri.Yule ndege alikuwapo, lakini mara ile alijigeuza msichana wa utanashati mkubwa. Msichana mwenyewe alikuwa yule aliyezama ardhini, baada ya kuokolewa na Adili, alipokuwa katika umbo la tandu na kushambuliwa na nyoka jabalini.



Malkia alimwuliza msichana mtu aliyemwokoa baharini alikuwa nani, na kwa nini aliletwa mbele yake.


Msichana alieleza kuwa mtu yule alikuwa mfadhili wake mkubwa. Zamani maisha yake yalipokuwa katika hatari ya nyoka alipata wokovu kwake. Alimwokoa na kumleta mbele yake kwa sababu aliahidi kulipa fadhili yake.


Kusikia vile, Malkia alisimama akampa mkono Adili aliyeupokea huku amepiga magoti chini. Malkia alimwinua akamkaribisha kuketi kitini akisema, "Starehe, mwanangu. Hali yako ni hali yetu".


Kisha msichana alimwuliza Adili kama aliweza kumtambua yeye alikuwa nani. Adili alijibu kuwa hakuweza.


Msichana alieleza kuwa yeye alikuwa tandu katika jabali fulani zamani akakaribia kuuwawa na nyoka, lakini aliokolewa.


Adili alikubali kuwa alikumbuka kuona tandu jeupe, nyoka mweusi, na msichana aliyezama ardhini.



Tandu lilikuwa yule msichana. Naye alikuwa Huria binti Kisasi. Kisasi alikuwa mfalme wa Majini. Aliyekaa kitini alikuwa mama yake. Jina lake lilikuwa Mjeledi, Malkia wa Majini. Nyoka aliyepigana naye Huria alikuwa waziri wa Ngazi. Alijulikana kwa jina la Hunde. Hunde alikuwa kiumbe cha mwisho katika wanaume waliokuwa na sura mbaya. Siju moja katika matembezi Huria alikutana na Hunde. Alikuwa hatazamiki kwa ubaya, licha ya yeye kumtazama mtu. Pale pale Hunde aliingiwa na shauku kubwa juu ya Huria. Wanawake hukutana na mikasa mingi mibaya duniani. Mioyo yao hulemewa na haja zisizokubalika; masikio yao hutiwa uziwi kwa maombi ya haraka; na miili yao ni mawindo ya jeuri daima.



Hunde alikwenda kwa Kisasi kumposa Huria. Kisasi alijibu Hunde alikuwa ni sufu kwa binti yake ijapokuwa alikuwa waziri wa Ngazi, na kwamba asingalithubutu mbele yake haja kama ile. Tangu siku ile alikomeshwa tamaa ya kuposa mabinti wafalme. Aliudhika akatisha kumwonyesha Huria uwezo wake. Na tangu alipotisha hivyo hakumpa nafasi hata ya uzi kupenya tundu la sindano.



Kila mahali Huria alipopita , Hunde alifuata nyayo zake mpaka aligundua alikokuwa. Iliendelea hivyo mpaka Kisasi akapigana naye. Alishindwa akakimbia. Huria alipotaka kutembea alijigeuza umbo la mnyama. Kila alipojigeuza na yeye alijigeuza vile vile akanusa harufu yake kama mbwa. Alipojigeuza panya, yeye alikuwa paka, alipojifanya paka, yeye alijigeuza chui; na alipokuwa chui, yeye akawa simba. Kila alipoingia yeye alipajua kwa kufuata nyayo zake. Wanaume wana inda mbaya ufisadi unapowapofusha.



Siku aliyojigeuza tandu , yeye alikuwa nyoka akamfukuza. Alipochoka kukimbia alimkamata. Kabla hajamhasiri, Adili alimpiga jiwe akafa. Alijigeuza mtu akaonekana na Adili kwa macho yake. Kabla ya kujizamisha chini aliahidi kulipa wema kwa Adili.



Huria aliomba dua siku zoye ya kuweza kutimiza ahadi yake kwa Adili. Siku aliyotoswa baharini na ndugu zake alikuja upesi kumwokoa katika hatari. Ilipasa wazazi wake, Mfalme na Malkia wa Majini kumkirimu mfadhili wake.


Alimwambia mama yake kwa deni alilowiwa na Adili lilikuwa kubwa sana. Hakudai lilipwe lote lakini lipunguzwe kama lilivyowezekana.



Mjeledi alimwambia Adili kuwa wema wake haukuoza. Kwa kumwokoa Huria aliwatendea wazazi wake fadhili na heshima kubwa nchi ya Majini. Ilikuwa zamu yao kumkirimu walivyoweza sasa.



Adili aliyenyamaza kwa muda mrefu alijibu, "Deni langu limekwisha lipwa lote. Niliokoa maisha ya binti yako, naye ameokoa yangu. Hapana deni tena kati yetu."



Malkia wa Majini alitabasamu akasema, "Usiseme kikembe mwanangu. Wema wako ulikuwa asilia, nawe ulitangulia kuutenda; wa binti yangu ulikuwa wa kuigiza, naye ameutenda nyuma. Asili na uigaji ni vitu mbalimbali. Havilinganiki wala havitalinganika milele."



ITAENDELEA

No comments:

Featured Post

 SOMA SIMULIZI ZENYE KUSISIMUA HAPA A. UTAJIRI WENYE UCHUNGU     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-1     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-2      UTAJIRI WENYE UCH...