Showing posts with label Fasihi ya Kiswahil. Show all posts
Showing posts with label Fasihi ya Kiswahil. Show all posts

Wednesday, October 13, 2021

NAFASI YA MITANDAO YA KIJAMII KATIKA UKUZAJI WA LUGHA YA KISWAHILI KARNE 21

 

NAFASI YA MITANDAO YA KIJAMII KATIKA MABADILIKO YA LUGHA YA KISWAHILI KATIKA KARNE YA 21

Na Kenyani Sangili Rongo University

Department of Languages, Linguistics and Literature IKISIRI

Wanafalsafa wa kale walidai kuwa, duniani, hakuna kitu ambacho hakikosi kubadilika. Mojawapo ya vitu vinavyobadilika ni lugha. Lugha za binadamu hubadilika katika kila kizazi kwa sababu mbalimbali za kiisimujamii na kiteknolojia. Kwa kuwa lugha za binadamu ni kitu changamano, mabadiliko yake hutokea kwa matawi ya kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia, kisemantiki na kipragmatiki. Kuna sauti ambazo hutokeweka katika lugha, na zingine hukopwa. Maana za leksimu hupanuka au hufinyika kutegemea matumizi yake kimuktadha. Kwa njia hii, mawasiliano ya binadamu huathirika kwani mabadiliko ya lugha hubadilisha mawasiliano na jinsi washiriki wanavyofasiri maana za kauli. Utafiti huu ulilenga kuchunguza mabadiliko ya lugha ya Kiswahili mintarafu mitandao ya kijamii. Hii ni kwa sababu mojawapo ya vitu vinavyosababisha lugha kubadilika katika karne ya 21 ni kiteknolojia. Utafiti ulilenga kuchunguza mabadiliko ya kifonolojia kwa kurejelea viunganishi mbalimbali vya kitandazi.


Utangulizi

Mabadiliko ni dhana inayojikariri kila mara katika shughuli zote za binadamu na viumbe wengine. Watoto hubadilika kwa kukua watu wazima na mimea hubadilika kwa kuzalisha matunda na majani. Wanavyosema wanafalsafa wengi kama vile Heraclitus, Edmund Spenser na von Humboldt, mabadiliko ni kitu kisichoepukika, hasa mabadiliko ya lugha (Aitchson, 2001). Lugha za binadamu zinachukua mikondo na mielekeo mipya kila kizazi kwa kulenga matumizi na ufaafu wa kijamii wa wakati huo. Lugha za kale za Kingereza, Kifaransa, Kijerumani na Kiswahili ni muhali kueleweka zinapotumika katika kizazi cha leo. Hii ni kwa sababu, zimepoteza baadhi ya maneno, zimepanuka kimaana, zimedhalilishwa kimaana, na vilevile, sauti za baadhi ya maneno zimetoweka au zingine kuongezwa kutokana na mtagusano au usahilishaji wa matamshi (Strazny na Trask, 2000; Lewis, 2009). Katika lugha ya Kiswahili, na hususan ushairi wa jadi wa Kiswahili, leksimu nyingi ni ngeni kwa wasomaji wa leo kwa sababu baadhi ya maneno yaliyotumika ni mageni kwao, yabadilika kitabdila au sauti zimedondoshwa kabisa. Baadhi ya haya maneno yamechambuliwa kutoka tenzi mbalimbali na mashairi ya Kiswahili ya kabla ya karne ya 20 (kwa mfano, taz. Shitemi, 2010).

 

Kwa mujibu wa Breivik na Jahr (1989) lugha zinabadilika ili kutosheleza mahitaji ya mawasiliano ya kipindi fulani. Huenda tunashuhudia mabadiliko ya mnyonge msonge na mwenye nguvu mpishe, kwa maana kuwa, mabadiliko yenye nguvu kuu kiuamilifu ndiyo yanakubalika huku yale yaliyo dhaifu yakipotea baada ya msimu. Katika jamii za leo wanajamii wengi wamesoma lugha na sheria zake katika mifumo mbalimbali ya shule, hata hivyo, badala ya wao kuzitumia sheria hizi, wanazikaidi katika kile ambacho Jahr (1998) anataja kama “kuchezea lugha ili kutimiza mahitaji na stadi”. Kwa mujibu wa wanasarufi elekezi, baadhi ya wanajamii hawa hawana haja ya kuzingatia sheria za lugha kama zinavyowekwa na watu fulani katika jamii lugha. Wao huona kwamba, wanapowekewa sheria za kufuata katika mawasiliano kisarufi, wanakosa uhuru wa kujieleza ipasavyo. Ndiposa Mohamed (2002) anapozungumzia dhana ya kukaidi sheria katika shairi ‘Arudhi’ anadai kuwa:

Kina, cha nini kina?

Kina, sitaki kina- iwapo chalazimishwa: la kije kwa hiari

tena kije vizuri

kilingane na pumzi (2002 : 78)


Kukaidi sheria za utunzi wa mashairi ya Kiswahili ndiko kulizalisha mashairi ya kisasa au ya kimapinduzi, vivyo hivyo, kukaidi sheria za kiisimu ndizo huzalisha mabadiliko ya lugha miongoni mwa watumiaji wake. Mifumo mipya ya kileksimu tunayoshuhudia katika Isimu- Kihistoria imetokana na wanajamii wenyewe kukaidi sheria mahsusi zinazotawala urasimi wa mifumo ya kiisimu. Lengo kubwa la kukaidi sheria hizi ni mwanajamii kupata uwezo na uhuru wa kujieleza bila vikwazo vyovyote vya kiisimu au kiarudhi.

 

Watumiaji lugha hufuata kile kinachofafanuliwa na wanasarufi fafanuzi kuwa katika lugha, kile ambacho ni muhimu katika uchanganuzi ni kile kinachosemwa na watu. Kanuni hizi si za kidhahania bali zinatokana na jinsi lugha hiyo inavyosemwa. Kwa mfano, katika lugha ya Kiswahili, uunganishaji wa sauti ili kuunda maneno hufuata sheria maalum kama vile :

[K+I, K+I+K+I]

Kwa mfano sauti hizi ni za kiswahili na zinapounganishwa, zinazalisha maneno ya Kiswahili kwa jinsi hii :

/a/, /a/, /ch/                   =          [acha] na wala siyo

=          [aach]

/a/,/a/,/p/                       =          [paa]

=          [apa] na wala siyo

=          [aap]

Kimsingi, maneno ya Kiswahili hayaishii kwa konsonanti, hivyo, ikiwa itatokea kinyume na sheria hii,na kinyume hiki kivumishwe kiuamilifu, basi hili ni badiliko la lugha. Sheria hizi hutawala pia mofolojia, hasa katika viambatishi na vinyambuo vya Kiswahili.

 

Nini Hubadilika katika Lugha?

Tunaposema kwamba lugha za binadamu zinabadilika tunamaanisha nini? Ni vipengele vipi ambavyo vinastahili kuchunguzwa ili kudhibitisha kwamba lugha imebadilika? Kulingana na watafiti mbalimbali lugha hubadilika kwa ujumla, yaani, kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia, kisemantiki na kipragmatiki (Hickey, 2001; Mey, 2009; Androupolous, 2011). Kwa hivyo, katika utafiti wa mabadiliko ya lugha, panatokea haja ya kutafitia vipengele hivi kama vinavyodhihirisha mabadiliko wakati fulani.


Sababu za Kubadilika kwa Lugha

Lugha hubadilika kwa sababu mbalimbali kama wanavyofafanua wataalam mbalimbali. Mey (2009) anadai kwamba lugha za binadamu zinabadilika kwa sababu utamaduni unaoambatana na lugha hizi unabadilika. Kwa kuwa lugha na utamaduni ni vitu viwili visivyoweza kutenganishwa, kimoja kinapobadilika hupelekea chenzake pia kubadilika. Utamaduni ni dhana pana kwani inahusisha vipengele vingi kama vile tabia za watu wa jamii moja, mapendeleo yao kijamii, na jinsi ya kujieleza au kuelezea dhana mbalimbali zinazowatawala (Wardhaugh, 2002). Elmes (2013) anadai kwamba utamaduni hudumishwa na kuwasilishwa kupitia lugha nayo lugha hudumishwa kupitia utamaduni. Kunapotokea upya katika utamaduni, husababisha uzalishaji, ukopaji na ubunaji wa misamiati mipya inayoelezea tukio au dhana hiyo mpya. Kwa mfano, kwa sababu jamii za Afrika Mashariki zimeingiza teknolojia katika utamaduni wake, hali hii imepelekea ubunaji wa msamiati mipya na kubadilisha lugha ya Kiswahili kwa kuiongezea maneno mapya. Maneno haya yameingizwa katika lugha ya Kiswahili kupitia njia mbalimbali kama vile ubunaji, ukopaji, na upanuaji kimaana na kimatumizi.

Diskimweo/Kinyonyi – Flashdisk

King’amuzi- Decoder

Kiwambo- Monitor

 

 

Jumla ya maneno haya yanaelezea upya ulioingizwa katika utamaduni wa jamii za Afrika Mashariki, na hivyo, palihitajika kubuni au kupanua istilahi zilizokuwepo kuelezea upya huu. Kiswahili hiki kinapolinganishwa na Kiswahili cha kale ambacho ni Kingozi, ni bayana kwamba baadhi ya maneno haya hayakuwepo, na kama yalikuwepo, hayakuwa na fahiwa hizi mpya za kiteknolojia.

 

Sababu ya pili ya kubadilika kwa lugha ni upashanaji wa lugha kutoka kizazi  kimoja hadi kingine. Tafiti zinaonyesha kwamba njia pekee ya kudumisha lugha ni kupitia kwa kizazi kimoja hadi kingine (Crystal, 2003). Ikiwa lugha itakufa au kutoweka, basi ni dhahiri kwamba, ilikosa wasemaji, hasa kizazi kichanga kilichostahili kuiendeleza. Mara nyingi, vipengele vya lugha vinapopitia kizazi baada ya kingine, husababisha mabadiliko ya sauti, misamiati, maana na matumizi ya maneno (Hickey, 2001). Baadhi ya sauti hutoweka au kupitia hatua za ukakaishaji, usimilishwaji  na  michakato  mingine  (Mgullu,  1999).  Vilevile,  kwa  kuwa  vizazi       vingine


huhamahama na kujikuta katika mazingira mapya ya kiisimu, misamiati mipya hukopwa kutoka kwa lugha hizi ngeni. Misamiati hii husimilishwa katika lugha na kuwa sehemu ya hazina mpya. Baadhi ya maneno huchukua maana mpya au kufunyika kimaana. Maana inapopanuka, husababisha ung’amuzi wa wanajamii kupanua kamusi ya akili zao ili kuhusisha maana hizi mpya. Kwa mfano, katika mawasiliano miongoni mwa baadhi ya wanajamii nchini Kenya, maneno haya yamepanuliwa kimaana na kizazi cha vijana.

 

Hitimisho


Mabadiliko ya lugha ni jmbo la kawaida na lisiloepukika katika kizazi chochote. Lugha ya Kiswahili kwa kuwa ni sehemu ya shani zinazobadilishwa na mambo kadha wa kadha, inadhihirisha mabadiliko haya katika mtagusano na teknolojia. Hakika, teknolojia ya kitandazi imekuwa na athari kubwa kwa lugha hii. Ingawa mabadiliko tuliyoshuhudia katika kazi yameegemea sana fonolojia, upo uwezekano kwamba fonolojia inaathiri mofolojia na mofolojia kuathiri semantiki ya mawasiliano ya kitandazi. Baadhi ya mabadiliko ya kifonolojia ambayo yalijadiliwa ni kama vile udondoshaji, uchopekaji wa sauti au mkururo wa sauti katika neno na pia ubadilishaji wa sauti badala ya nyingine. Utafiti mwingi zaidi wa kimofolojia unastahili kufanywa katika nyanja hii ili kuthmini mabadiliko yanayotokea.

 

Marejeleo


Aitchison, J. (2001). Language Change: progress or decay? 3rd edition. Cambridge: Cambridge University Press.

 

Androutsopoulos, J. (2011). Language Change and digital media: a review of conceptions and evidence. In Coupland N. & Kristiansen, T. (Eds). Standard languages and

language standards in a changing Europe. Oslo: Novus.

Bakari, M. (1982). The morphophonology of Kenyan Swahili dialects. Unpublished PhD Dissertation. Nairobi: University of Nairobi.

 

Bertoncini, Z.E. (2002). When grandfather came to life again: Said Ahmed Mohamed’s new novel beyond realism. Swahili Forum IX: 25-33.

 

Bynon, T. (1977). Historical linguistics. Cambridge: Cambridge University press. Cambridge University Press.


Chiraghdin, S. & Mnyampala, M. (1977). Historia ya Kiswahili. Oxford: Oxford University press.

 

Crawely, T. (1992). An introduction to historical linguistics. Oxford: Oxford University Press. Crystal, D. (2003). Engish as global language. 2nd ed. Oxford: Oxford University Press.

Elms, D. (2013). The relationship between language and culture. Kayanora International exchange and language education center.

 

Hickey, R. (2001). Language Change in Verschueren, J., Östman J., & Blommaert J. (eds.)

Handbook of pragmatics. Amsterdam: John Benjamins

 

Lewis, M.P. (2009). Language family trees in Indo-European: Ethnologue languages of the world. SIL International.

 

Mey, J.L. (2009). Concise encyclopedia of pragmatics, 2nd ed. Oxford: Elsevier Ltd.

 

Mgullu, R. S. (1999). Mtaala wa isimu: fonetiki, fonolojia na mofolojia ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn.

 

Milroy,  J.  &L.  Milroy.  (1985).  Linguistic  change,  social  network,  and  speaker  innovation.

Journal of Linguistics 21: 339-384.

 

Mohamed,S.A. (2002). Jicho la ndani. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

 

Njogu, K. na wenzake. (2007). Sarufi ya Kiswahili: uchanganuzi na matumizi. Nairobi : Jomo Kenyatta Foundation.

Shitemi, N.L. (2010). Ushairi wa Kiswahili kabla ya karne ya ishirini. Moi University: Moi University Press.

 

Strazny, P. & Trask. R.L. (2000). Dictionary of historical & comparative linguistics. 1st ed. New York: Routledge.

 

Trask, R.L. (1994). Language Change. London: T.J. International Ltd.

 

 

Trudgill, P. (1989). Contact and isolation in linguistic change. In Breivik, L. E. & Jahr, E. H. (eds.), Language change: contributions to the study of its causes (pp.227-237). Berlin: Mouton de Gruyter.

 

Wardhaugh, R. (2002). An introduction to sociolinguistics (4th ed.). Oxford: Blackwell Publishers.

Featured Post

 SOMA SIMULIZI ZENYE KUSISIMUA HAPA A. UTAJIRI WENYE UCHUNGU     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-1     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-2      UTAJIRI WENYE UCH...