Sunday, June 27, 2021

Umuhimu wa maudhui katika riwaya ya Pambazuko gizani au ......


KF: FALSAFA YA KIAFRIKA NA NADHARIA YA FASIHI

 SWALI LA : Kwa mifano kutoka Pambazuko Gizani (Mboneka) au utungo wa Al-inkishafi (Sayyid Abdallah), jadili umuhimu wa maudhui ya kazi hizo katika kuadilisha jamii. Nini changamoto za waandishi katika uwasilishaji wa maudhui hayo

               Maudhui ni mojawapo ya mambo mawili yanayokamilisha kazi ya sanaa, jambo likamilishalo kazi ya sanaa ni fani au umbo. Kwa mujibu wa senkoro (1982) “Maudhui hujumuisha mawazo na pengine mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma mtunzi ama msanii hadi kutunga kazi fulani ya sanaa”.Pia Wamitila( 2003) anasema “Maudhuini yaliyomo au jumla ya masuala yanayozungumziwa katika kazi ya fasihi yoyote”. Riwaya ya Pambazuko Gizani imeandikwa na Karumuna Mboneka, mwaka 2004. Riwaya hii imeelezea safari ya Klaus Mahyofer ambaye anatokea ujerumani na kuja kutafuta ndugu zake Afrika hususani bubako ambao waliachwa na babu yake Klaus wa White Fathers. Katika safari yake anakutana na kijana wa kiafrika aliyeitwa Kalinguliza ambaye alikuwa ni padre.Katika safari yao (Klaus na Kalinguliza ) waliweza kupita katika parokia mbalimbali zilizokuwa zinamilikiwa na dini na kupitia safari yao hiyo wameweza kuibua maudhui mbalimbali ambayo yameiadilisha jamii,

               Athari za uhujumu uchumi katika jamii. Mwandishi wa Pambazuko Gizani amekemea suala la uhujumu uchumi kwani hupelekea athari mbalimbali kwa watu wa hadhi ya chini. Mwandishi amemtumia mhusika Askofu Yona Kyalemile ambaye anaishi jimbo la Bishuba. Askofu huyu anamiliki jumba kubwa la thamani ambalo lina kila kitu cha kisasa, milango ya umeme ya kumchukua Askofu kutoka maegesho ya ya gari hadi chumbani mwake, nyumbani kwake kuna maji ya kutosha, umeme na simu za mikononi, chombo cha kunasia habari za televisheni za dunia nzima, mashine za kufua na mambo mengine mengi. Lakini watu wake wa jimbo la Bishuba ni watu mafukara kabisa ambao wanaishi maisha ya shida. Wanaishi kwenye nyumba za wasiwasi kiasi kwamba wakati wa kipindi cha mvua hakuna tofauti ya kuwa ndani au kuwa nje. Pia wana tatizo la maji kwani hutembea umbali mrefu takribani kilometa kumi kuyafuata maji. Mwandishi anaeleza katika uk.52 kuwa “Pesa anazozitumia Askofu Yona Kyalemile kuitunza bustani yake kubwa zingeweza kuwapatia watu wote huduma ya maji.” Pia mwandishi anaeleza suala hili la uhujumu uchumi pale anapomtumia Klausi akiwa anaelekea Kibona. Alikuwa anajibizana na kijana mchangamfu ambapo waliongea mambo mbalimbali ikiwemo suala la viongozi. Klausi anasema kuwa baadhi ya viongozi wa nchi wanasomesha watoto zao nje ya nchi ambapo huo ni ubadhilifu wa mali. Pia Klausi katika (uk. 29) anasema “Hasa nyinyi mnajibana zaidi. Juzi tulielekezwa kwamba barabara hii imefanyiwa ukarabati sasa ona inavyoonekana! maana yake ni kwamba pesa za ukarabati zimeingia kwenye mifuko ya watu!” Hivyo basi mwandishi amesukumwa kuiandikia jamii kuhusu athari zitokanazo na uhujumu uchumi kwani ni kikwazo cha maendeleo katika jamii ndio chanzo kikubwa cha matabaka kwani wale wenye mamlaka watawanyonya wanyonge na watazidi kuendelea na wanyonge watazidi kudidimia. Kwa hiyo viongozi hawanabudi kuachana na suala la kuhujumu mali za nchi ili maendeleo yaweze kupatikana.

            Athari za ulevi katika jamii. Ulevi ni suala ambalo linasababisha athari au matatizo mbalimbali katika jamii, Mfano wa matatizo ni kama kutowajibika kikazi au kifamilia, kufutwa kazi au hata kudharaulika. Hivyo katika riwaya hii Ya Pambazuko Gizani mtunzi ameweza kuonesha au kueleza namna ambavyo ulevi unasababisha watu kutosikilizwa mawazo yao hata kama wanachoongea ni cha msingi na kina manufaa kwa watu. Kwa mfano amemtumia Padre Prudence ambaye ni msaidizi wa Bwana Mkubwa katika kanisa katoliki. Padre huyu alikuwa ni mlevi kupindukia na hakupata nafasi ya kusikilizwa na Bwana Mkubwa alipokuwa akitoa mawazo yake kama msaidizi wake. Hii inadhihirika katika (uk, 15), Padre Prudence anasema “......ona huyu padre mkubwa ana madaraka yote. Yeye ni kila kitu hapa. Hatupi nafasi ya kuleta mawazo mapya katika kanisa letu.” Lakini pia ulevi ulipelekea au ulisababisha padre Prudence kupangiwa majukumu kama mtoto na malipo yake ni pombe. Mfano katika ukurasa wa 16, Prudence anasema “......kazi ninapangiwa kama mtoto mdogo, kitulizo pekee ni pombe. Ninakunywa na kulewa na kama mjuavyo pombe ni pombe tu nikishakunywa inanituma pengine.” Kutokana na hili, ilimpelekea kufumaniwa, Pia katika jamii zetu ulevi umekuwa changamoto kubwa ambapo jopo kubwa la vijana ndio wahanga wa ulevi, watu hukosa kazi, hudharauliwa na kushushwa thamani yote hii ni kutokana na ulevi. Hivyo suala la ulevi sio zuri kwani lina madhara makubwa kwa mtu binafsi na kwa jamii nzima.

Hutusaidia kujua athari za uongozi mbaya katika jamii. Mwandishi wa riwaya ya Pambazuko Gizani ameweza kuelimisha jamii juu ya athari za uongozi mbaya katika jamii. Mwandishi ameelimisha jamii kwa kuonesha namna viongozi wanavyo watumikisha watu wanaowaongoza bila kujali utu wao bali hujali maslahi yao. Mfano katika (uk. 14) Padre alipokea mapendekezo ya kuwajengea nyumba wafanyakazi walio kuwa wakisomba miti na kusaidia ujenzi, lakini padre kama kiongozi hakukubaliana nalo alisema “Sisi tumetumwa kueneza neno la Mungu, kujenga nyumba ya Bwana na wala si nyumba za wapagani hawa ambao bado wanaishi gizani.” Padre mkubwa alikuwa akiwatumikisha watu na kuwaacha katika giza nene. Suala hili linajitokeza katika jamii zetu kwa wenye mamlaka au wadhifa fulani kutumia nguvu yake dhidi ya wale anaowaongoza mfano, kuwatishia kuachishwa kazi. Hivyo, mwandishi anaidhihirishia jamii ya kuwa ili tuweze kusonga mbele lazima viongozi watumie nafasi zao vizuri kwa kuleta maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Hutusaidia kuelewa athari za matabaka katika jamii. Mwandishi wa riwaya ya Pambazuko Gizani amefanikiwa kuonesha matabaka na athari zinazotokana na matabaka hayo katika jamii. Kwa mfano, mwandishi amemtumia mhusika Klausi ambaye alikuwa anashangaa meli ya MV-Viktoria kugawanywa katika matabaka matatu. Daraja la kwanza ni sehemuya wtu wenye pesa, viongozi wa serikali, na viongozi wa dini. Daraja la pili ni la watu wa kati ambao si maskini na daraja la mwisho hubeba mizigo pamoja na watu bila tofauti. Mfano wake ni sawa na jehanamu. Mwandishi ameweza kufanikiwa kuyasawiri vyema maisha halisi ya waafrika ambayo yamejaa matabaka ambapo matajiri wanapata huduma zote za kijamii, wanapewa wadhifa mkubwa wa kimadaraka serikalini lakini tabaka la chini huwa ni tabaka lililosahaulika, hakuna huduma za kijamii kama umeme, hospitali, maji safi na ni nadra sana kuwapata viongozi wa juu katika tabaka hili la chini. Mwandishi wa riwaya ya “Pambazuko Gizani” katika (uk. 8) anazungumzia hilo “......jinsi meli ilivyotegwa, hivyo hivyo na miji kuna mitaa ya daraja la kwanza, kama Mikocheni, Msasani, na Mbezi. Mitaa ya daraja la pili, Kijitonyama na Sinza, na daraja la tatu, Tandika na Magomeni.” Hivyo matabaka haya husababisha watu wengi wasiojiweza kutaabikana hatimaye kufariki kabla ya kupatiwa msaada husika. Hivyo mwandishi amesisitiza kuwa matabaka ni kikwazo katika maendeleo.

Athari za mapadri kubariki ndoa. Mapadre ni viongozi ambao wanapewa dhamana ya kuliongoza kanisa na kusimamia watu katika suala zima la imani katika parokia mbalimbali. Ambapo katika kuhudumia jamii katika suala la imani kupitia dini ya kikristo wanaapizwa kuwa wasiwe na mke au kuoa ikiwa ni pamoja na kutofanya tendo la ndoa yaani kuwa seja(maseja). Lakini kuna baadhi ya mapadri wanaojiongezea majukumu mbalimbali tofauti na lengo lao la kufanyika maseja na kuanza kuwaingilia wanawake na kusababisha watoto wasiotarajiwa. Mfano katika riwaya yetu ya Pambazuko Gizani katika ukurasa wa 49, mwandishi anaeleza na kuonesha ni jinsi gani watoto wengi wa kwanza kuwa ni matokeo ya mapadri kuwaingilia(kufanya tendo la ndoa na wanawake) wake wa waumini wao kwa kisingizio cha kubariki ndoa. Mwandishi anasema “Inasemekana kwamba, watoto wengi wa kwanza kwenye familia za kiparokia hiyo enzi hizo walikuwa ni matunda ya baraka za huyo padre.” Pia suala hili linapelekea baadhi ya watoto kufa ambayo ni matokeo ya mapadre kufanya tendo la ndoa na waumini wao (uk. 19-20) ambapo watoto hao wanakufa bila kutajwa majina ya baba zao ikiwa ni nyenzo mojawapo ya kuficha siri ya mapadre waliokuwa wakifanya tendo la ndoa  na wanawake ikiwa kinyume cha maadili ya kazi yao. Hivyo ni muhimu kila mtu katika jamii yake kufanya kazi sahihi na kuzingatia maadili ya kazi na maadili ya jamii kwa ujumla ili tuweze kupiga hatua za kimaendeleo.

Umuhimu wa umoja na mshikamano katika jamii. Mwandishi wa Pambazuko Gizani ameonesha kuwa umoja na mshikamano ndio ngao ya maendeleo katika jamii. Umoja na mshikamano huo unaweza kuwa baina ya watu walio katika ngazi moja au ngazi tofauti (viongozi na wanaoongozwa). Mwandishi anawatumia wahusika kama vile Klaus Mahyhofer na Kalinguliza Kamuhanda ambao wameshirikiana haswa tangu walipokutana katika meli ya MV Viktoria. Mwandishi amesema katika (uk. 8) “wawili hao walishirikiana na kutokata tamaa, ingawa walinyanyaswa na mapadri, walinusurika kuuawa, walitembea umbali mrefu hawakukata tamaa. Kupitia wawili hawa ndio waliofichua uovu unaofanywa na viongozi wa dini kwa kushirikiana na Ma Paulina. Mfano mwandishi anasema katika (uk. 47) “…….haikuwa kazi rahisi kumtafuta Makokuleba na kumpata. Ilichukua mwezi mzima, kwani kilikuwa kigumu cha mvua na barabara zilipitika kwa shida sana. Wakati mwingine tulilala barabarani……” Hii inadhihirisha kwamba Klaus na Kalinguliza walipitia maisha ya taabu hadi kufanikisha kuipata familia ya Klaus. Suala hili la umoja na mshikamano linaendana sambamba na jamii zetu za kiaafrika hususani nchini Tanzania ambapo kwamba kuwepo kwa maelewano, umoja na mshikamano baina ya viongozi na wananchi kumesababisha kuwepo kwa  maendeleo katika nyanja mbalimbali. Hivyo mwandishi anasisitiza suala hili lazima liendelezwe kwa ajili ya manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

  Mbali na maudhui ambayo yamejitokeza katika riwaya ya Pambazuko Gizani, pia kuna changamoto mbalimbali zinazowakumba waandishi katika uwasilishaji maudhui na maudhui hayo, nazo ni;

Changamoto katika lugha, hii ni moja ya changamoto za mwandishi wa kitabu hiki katika uwasilishaji wa maudhui. Changamoto hii inajidhihirisha katika misamiati aliyoitumia mwandishi kama vile Majina, inaonekana kuwa majina mengi yanayotumika kwenye hadithi yamebeba taswira na maana kubwa ndani yake. Kwa Wahaya hadithi inakuwa na ujumbe mzito kwa kuelewa maana inayobebwa kwenye majina. Pia kufahamu maana ya majina kunaongeza utamu wa hadithi yenyewe na kama mtu hajui Kihaya atapata ujumbe nusu wakati majina aliyotumia mtunzi ya hao wahusika yangetafsiriwa ujumbe ungewafikia watu wengi katika jamii mbalimbali. Mfano wa majina ya wahusika na maeneo mbalimbali aliyotumia mtunzi bila kutafsiri kama kalinguliza maana yake ni mtu “anayechunguza chunguza” Kabanga maana ni “mlima”, Mushenyele lina maana “Askofu”, Bishuba lina maana “uongo”. Hivyo hii ni changamoto kubwa  kwa kuwa ametumia jamii ya wahaya sana sio watu wote ni Wahaya.                    Changamoto ya kimtazamo wa mtunzi. Katika riwaya hii, mtunzi ameonekana kujikita sana katika suala la dini hasa dini ya kikristo katika dhehebu la kikatoliki. Kwa kuonesha ni jinsi gani mapadre wa kanisa hilo walivyokuwa wanafanya maasi, kama kuwa na watoto machotara, kuzaa na wanawake wa kiafrika, kudidimiza dini ya kijadi, kunyang’anya ardhi na kadhalika. Hivyo hatuelezei wazi kuhusu masuala ya kiuchumi, kihistoria na kisiasa yanavyopelekea pia kutokea kwa hayo maasi kama mauaji, na vipi kuhusu huduma za afya kwa hiyo jamii iliyomzunguka, kama maji, hospitali, elimu, barabara hajafafanua vizuri na hajalieleza kiupana zaidi. Hivyo hii ni changamoto katika uwasilishaji wa maudhui kwani mtunzi anautafsiri mwenendo wa kihistoria ya kidini zaidi, na hivyo kushindwa kuangalia ulimwengu katika nyanja mbalimbali na hata hiyo dini kazungumzia dini moja ilhali dini ya kiislamu, mtunzi hajaizungumzia.

Kwa kuhitimisha,mwandishi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuadilisha jamiii katika kuzungumzia mambo mbalimbali ambayo yanadhoofisha maendeleo ya jamii kama vile ulevi,kijilimbikizia mali pamoja na matabaka , lakini pia mwandishi amefanikiwa kuanzisha mjadala juu ya mambo mbalimbali ambayo wengi wetu tunaogopa kuyagusia ,mambo ya imani ambayo wengi wetu tunaamini tu bila kutumia akili  mfano mwandishi anaweka wazi kuwa wamishonari walipokuja watu walippenda maendeleo ya vitu kama vile shule,madawa na nyumba kuliko walivyotamani dini hiyo ya kigeni ukweli ni kwamba wamishonari walitumia vitu hivyo walivyotamani watu kama chambo,pia mwandishi anazungumzia swala la useja na athari zake

 

 

 

 

 

 

 

Marejeleo

MBONEKA K (2004), Pambazuko Gizani.E & D Limited

WAFULA R & NJOGU K, (2007). Nadharia ya uhakiki wa fasihi. Sai Industri Ltd. Nairobi

WAFULA K.W (2003).Kichocheo cha fasihi Simulizi na Andishi.Focus Publication Ltd:Nairobi,                                           Kenya


No comments:

Featured Post

 SOMA SIMULIZI ZENYE KUSISIMUA HAPA A. UTAJIRI WENYE UCHUNGU     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-1     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-2      UTAJIRI WENYE UCH...