Saturday, October 30, 2021

ADILI NA NDUGUZE sehemu ya 1

     

ADILI NA NDUGUZE - 1

 


IMEANDIKWA NA : SHAABAN ROBERT

*********************************************************************************

Simulizi : Adili Na Nduguze 

Sehemu Ya Kwanza (1)



SURA YA 1


Mfalme Rai


Rai, mfalme wa Ughaibu , alikuwa mfalme namna ya peke yake duniani. Alikuwa na tabia iliyohitilafiana kabisa na tabia za watu wengine wa zamani zake. Tabia yake ilijigawa katika theluthi tatu mbalimbali kama rangi ya ngozi ya punda milia. Kwa theluthi ya kwanza alikuwa msuluhifu akapendwa na watu, Kwa theluthi ya pili alifanana na Daud akaheshimiwa kama mtunzaji mkuu wa wanyama, na kwa theluthi ya tatu alikuwa kama Suleiman akatiiwa na majini. Kutawala suluhu na mapenzi ya wanadam, utunzaji wa wanyama, na utii juu ya viumbe wasioonekana kama majini hutaka uwezo mkubwa sana. Kwa hivi, fikiri wewe mwenyewe jinsi Rai alivyojipambanua mwenyewe na wafalme wengine.


Katika miliki ya mfalme huyu kodi ilitozwa juu ya mifugo ya wanyama. Kodi hii ilihalalishwa kwa sababu Ughaibu ilikuwa nchi ya mifugo. Ughaibu ilipokuwa juu ya kilele cha usitawi mifugo yake ilikuwa hailingani kwa ubora na mifugo ya nchi yoyote nyingine ulimwenguni. Fahari yake ya mifugo ilikuwa kubwa kabisa. Fahari hiyo haikuwezekana kukadaika ikatazamwa kwa wivu katika dunia nzima. Malipo ya kodi hii yalifanywa kwa wanyama waliozaliwa pacha. Kila zizi lilitozwa pacha moja kila mwaka. Mazizi yaliyokuwa hayana wanyama waliozaliwa pacha katika mwaka uliodaiwa kodi yalisamehewa. Zizi lililoshindwa kulipa kodi lilitokea kwa nadra sana kwa sababu mifugo yote ilikuwa mizazi ya ajabu. Zilipatikana pacha katika mbuzi, kondoo, ng'ombe, farasi, na wanyama wengine.


Masurufu ya serikali ya Ughaibu yalitegemea katika juu ya wanyama wake. Kwa sababu hiyo kila zizi katika nchi lilihesabiwa kama hazina maalum, na kila mnyama katika zizi hilo alikuwa kama johari hasa. Mazizi yaliyopotelewa na mifugo yake kwa maradhi yalijazwa tena wanyama wapya. Masikini waliotaka mifugo, lakini waliokuwa hawana njia ya kuipata, walikidhiwa haja zao na serikali bila malipo yoyote. Basi mifugo ilienea katika nchi yote ya Ughaibu.


Kwa masurufu haya na misaada kama hii uangalifu wa mfalme juu ya wanyama wa mifugo ulikuwa hauna kiasi wala kadiri, na huruma yake juu ya wanyama wasiokuwa wa mifugo ilishawishika sana.


Rai alikuwa kiongozi muadilifu na mfalme mwema sana. Hakusita kufanya kazi ndogo wala kubwa kwa mikono yake mwenyewe. Kazi nyingi za ufalme alizitenda yeye mwenyewe. Zile ambazo hakuwahi kuzitenda yeye mwenyewe alipenda kuziona kwa macho yake zilivyofanywa. Kwa bidii zake kubwa aliweza kushiriki katika mambo mengi ya maisha akasaidia maendeleo makubwa ya nchi yake. Hakulazimisha mtu yeyote kutenda tendo fulani, lakini alishawishi kila moyo wa mtu kuiga alivyotenda kwa hiyari yake mwenyewe. Alikuwa na mvuto mkubwa juu ya mioyo ya watu. Alitumia mvuto huu juu ya watu mpaka nchi yake ilikuwa haina mvivu, goigoi wala mwoga.


Kuondoa uvivu , ugoigoi na woga katika nchi ni kazi ngumu. Mambo haya yanapendwa sana na watu ingawa yana madhara makubwa kwao. Kwa hivi, kufaulu kwa Rai kulistahili sifa kubwa sana. Sifa yake ilifurahiwa na viumbe wote. Malaika mbinguni waliitungia mashairi; ndege hewani waliimba kwa sauti zao nzuri; wanadamu duniani waliisimulia kwa hadithi; majini na mashetani waliikariri kwa tenzi. Rai alikuwa mtu mmoja katika watu bora waliopata kutoka tumboni mwa mwanamke. Alifanya urafiki na viumbe mbalimbali kwa sababu aliwajali wote.


Ilikuwa si desturi ya Rai kusema maneno na kuacha watu wengine watende matendo, lakini alitenda matendo akaacha watu wengine waseme maneno. Tendo hukidhi haja maridhawa kuliko neno. Haja ikishughulikiwa kwa matendo hupatikana upesi, lakini ikishughulikiwa kwa maneno huchelewa kama sadaka. Rai alifaham haya lakini watu wake hawakufaham. Hawa walipaswa kuamshwa katika usingizi wao kwa matendo, sio kwa maneno. Maisha ya Rai yalipita katika matendo mbalimbali.


Katika hukumu alikuwa imara sana. Hakupendelea mkubwa wala hakudhulumu mdogo. Watu wote walikuwa sawasawa mbele ya sheria. Hakuuza haki za watu kwa rushwa. Wanadamu na wanyama walioata haki zao katika baraza lake. Hili ndilo tendo moja katika matendo yake ambalo limetia jina lake katika makumbusho yasiyosahaulika katika wakati wake, sasa na baadae katika wakati ujao duniani. Kila mtu alipoiga matendo ya mfalme yabisi katika nchi alifukuzwa. Rutuba ilienea kila mahali. Kwa rutuba hii ardhi ya Ughaibu ilikuwa na rangi ya kahawia. Juu ya ardhi hii paliota mimea iliyofanana za zabarijudiwa uzuri. Mimea hii ilie eza neema ya vyakula kwa watu na malisho ya wanyama. Hewa ya nchi nzima ilinukia manukato kwa naua mazuri ya mimea mbalimbali.


Siku moja Rai alipokuwa akitazama hesabu za wanyama waliokusanywa kwa kodi, aliona karibu mazizi yote katika miliki yake yamekwisha lipa kodi zake ila mazizi ya Janibu. Ugunduzi huu uliamsha wasiwasi mkubwa uliokuwa ukingojea mguso mdogo tu katika moyo wake. Moyo wake ulipokuwa ukiliwa kwa wasiwasi, mawazo mbali mbali yalipita katika akili yake. Alidhani kuwa labda Janibu imepatwa na mwaka wa kiu, na kuwa malisho ya wanyama yameharibika. Labda sotoka imeshambulia mazizi katika nchi, na kuwa vifo vingi vimetokea katika mifugo. Kwa kuwa wanadamu na wanyama wana shirika moja katika maisha, Rai alihamasika sana. Aliona dhahiri kuwa madhara ya wanyama ni hatari kwa watu vile vile. Rai alikuwa na akili tambuzi iliyopenya katika mashaka mengi ya maisha. Walakini, hizi zilikuwa dhana tu. Dhana zenyewe zilikuwa haziwezi kusaidia kujibu ugunduzi wake. Palikuwa hapana kitu kilichoweza kuzithibitisha.


Ughaibu na Janibu ilikuwa miji miwili mbalimbali chini ya miliki moja. Miji hii ilitengwa na umbali mkubwa. Ugunduzi wa Rai katika hesabu ya kodi ulifasiri upungufu ambao haukutazamiwa. Sababu ya upungufu ule haikujulikana kwa sababu habari za Janibu zilikosekana. Pasipo shaka, hukubalika bila ya swali kuwa miji miwili ina ina ndoto mbili zenye maana mbalimbali. Rai aliweza kujua tafsiri ya ndoto ya Ughaibu kuwa jumla ya kodi ilikuwa na kasoro, lakini hakuweza kujua maana ya ndoto ya Janibu, yaani sababu ya kasoro ile. Mambo katika maisha yamo katika mwendo huu siku zote. hmHayajulikani mpaka yamechunguzwa na kuthibitishwa kwanza. Rai alikuwa mtu arifu wa mwendo huu. kwa hivi, shauri hili liliachwa kwa Maarifa, Waziri Mkuu, kuchunguzwa.


SURA YA 2




Siri inafichuka



Ikibali alitakiwa na Maarifa kwenda Janibu kuchunguza kodi. Ikibali alikuwa mshauri katika halmashauri ya Ughaibu na mshairi wa mfalme. Alichaguliwa kwa kazi hii kwa sababu alikuwa na maarifa ya kuchukuana na watu. Kwa maarifa haya aliweza kupata mradi wake siku zote bila ya kuamsha uadui wa watu juu yake. Ughaibu ilikuwa teuzi katika wasimamizi wake na katika madaraka yao. Uteuzi wake ulikuwa na maana kwa sababu ukamilifu wa mtu duniani ni tabia njema. Mbali ya sifa nyingine, kila mtu bora alitakiwa kuonyesha ubora wake kwa kuchukuana na watu. Ikibali alikuwa mkamilifu wa tabia akaaminiwa na Rai, Maarifa, halmashauri na watu wadogo.



Siku ya pili, saa moja asubuhi, Ikibali alikwenda janibu. Mwendo wa saa sita kwa farasi ulikuwa kati ya Ughaibu na Janibu. Adhuhuri ilipokaribia Ikibali alikuwa amefika katika viunga vya mji aliokusudia. Huko alitua akapeleka taarifa kwa Adili, Liwali wa janibu kuwa amewasili. Adili alipopata habari alikwenda akamlaki mgeni wake nje ya mji kwa furaha. Baada ya kumlaki aliingia naye mjini. Saa saba mchana Ikibali alifika nyumbani kwa mwenyeji wake akapokewa kwa taadhima. Alikula chakula cha mchana na mudir wa Janibu, na saa nane akazuru idara zao. Hulka ya ikibali ilipendeza watu waliopata kukutana naye. Kicheko kilikuwa midomoni mwake na shukrani katika pumzo zake. Hulka njema sawa na mali. Fundisho hili linakwenda duniani mpaka sasa.



Jioni Ikibali na Adili walipokuwa peke yao mazungumzo juu ya kodi yalianza. Hapakuonekana upungufu wowote. Hesabu haikuwa kamili tu, lakini ilionyesha ziada vile vile. Ikibali alihakikishwa kuonyeshwa ziada hii asubuhi. Sababu ya kuchelewa ilihusiana na makusanyo ya ziada. Kama Adili hakutanguliwa na Ikibali siku moja, Adili alikusudia kupeleka hesabu yake Ughaibu siku ya pili. Ikibali alifikiri habari hizi njema zilitosha kutuliza wasiwasi wa mfalme. Kwa hivi, aliazimu kurudi Ughaibu kesho yake. Adili alitaka kutajamali na Ikibali. Hamu yake ilikuwa kubwa sana. Kama haja hii haikumkalifu Ikibali, Adili aliomba sana jamala ya kutafaraji naye kwa muda wa siku tatu. Kwa kuwa waungwana hawanyimani neno lisilokalifu Ikibali alikubali kuahirisha marejeo yake.



Sasa Adili na mgeni wake waliingia sebuleni. Sebule hiyo ilikuwa imesakifiwa na marmar za rangi tatu, yaani, nyeupe, nyekundu na samawati. Dari yake iliikizwa vizuri sana. Ilisaki sawasawa juu ya kuta nne zilizopakwa sherezi ya manjano. Katikati ya dari hii ilining'inia chini karabai moja iliyozungukwa na matovu ya almasi. Kuta mbili katika hizi nne zilikuwa na madirisha mazuri. Katikati ya sakafu palitandikwa mazulia ya thamani kubwa. Juu ya mazulia hayo palikuwa na meza moja ya mkangazi na viti viwili vya henzirani. Vyakula na vinywaji mbalimbali viliandaliwa juu ya meza. Walikaa kitako hapo kwa kuelekeana wakala chakula cha usiku. Baada ya kula na kunywa walizungumza mpaka wakati wa kulala.



Malazi ya Ikibali yalifanywa katika chumba kilichokuwa na sakafu ya marmar nyeupe tupu. Dari ilipakwa sherezi ya samawati na kuta zilikuwa na sherezi ya zari. Kila ukuta ulikuwa na dirisha la kioo kilichosimama juu ya mihimili ya johari. Vitanda viwili vya pembe vilivyokuwa na viwambo vya ngozi na matandiko ya pamba vilitandikwa humo.. Mihimili ya vyandarua ilikuwa ya dhahabu. Siku ile Adili alilala katika chumba kimoja na mgeni wake. Baada ya kupanda vitandani wote wawili walinyamaza kimya. Kila mtu alidhani mwenzake amelala, lakini wote wawili walikuwa macho. Ikibali alikuwa akisanifu mashairi, kama ilivyokwisha semwa kuwa alikuwa mshairi mashuhuri. Alipoendelea hivyo mpaka usiku wa manane alimwona Adili ameondoka ghafula kitandani. Chumbani lilikuwamo bweta. Adili aliokwisha vaa nguo zake aliliendwa bweta akalifungua. Alitoa mjeledi na mshumaa. Mshumaa ulipowashwa nuru kubwa sana ilitokea. Sasa Adili alifungua mlango wa chumbani akatoka nje. Hakujua kama Ikibali alikuwa macho.



Ikibali alishangaa usanifu wake ukachafula. Hakujua Adili alikusudia kwenda wapi na mjeledi usiku ule. Alijua kwamba ilikuwa si murua kunyemelea mambo ya watu, lakini alijua pia kwamba ilikuwa wajibu kujiweka tayari kusaidia katika haki. Kwa sababu ya msaada aliona haifai kulala kama mvivu nafasi ya kutenda wajibu wake ilipotokea. Wazo hili lilimwondoa kitandani akatoka nje.. Alimfuata Adili nyuma polepole. Karibu ya nyumba moja ndogo Ikibali alisimama kando. Adili alifululiza mpaka mlangoni. Aliufungua akaingia ndani. Alipotoka nje alikuwa na sinia moja. Siniani mlikuwa na sahani za chakula na birika la maji. Alijibandika begani sinia akaenda zake. Ikibali alimfuata nyuma vile vile.



Adili alipofika nyimba nyingine, kubwa kuliko ya kwanza, alifungua mlango akaingia ndani. Nyuma yake mlango ulifungwa kwa nguvu. Ikibali alinyata mpaka mlangoni akasimama kimya. Alichungulia ndani katika ufa wa mlango akaona ukumbi. Katikati ya ukumbi palikuwa na kitanda kizuri na meza moja. Manyani mawili yaliyofungwa viunoni minyororo ya dhahabu yalikuwa yamelala kitandani. Adili aliweka sinia juu ya meza. Nyani moja lilipofunguliwa lilirukaruka likalialia kinyonge. Adili alilikamata akalifunga miguu ya mbele na ya nyuma kwa kamba. Alipolitupa chini alishika mjeledi kwa mkono wa kulia akalipiga mpaka likazirai. Nyani jingine lilipigwa likazirai vile vile. Manyani yalipizinduka yalinasihiwa. Adili aliapa kuwa hakufurahi kuyaadhibu, na kwamba alitazamia faraja yao kutokea karibu.



Sasa manyani yalichukuliwa mezani kula chakula kwa vijiko na nyuma. Yaliposhiba yalinyweshwa maji. Midomo yao ilifutwa kwa leso za hariri. Kisha yalifungwa minyororo kama yalivyokuwa. Mambo haya yalipotendeka Ikibali alikuwa amesimama kimya anachungulia. Adili Alipokusanya vyombo ili atoke nje, Ikibali alitangulia kuondoka mlangoni. Alikwenda mpaka kitandani pake akajilaza kimya kama aliyekuwa hajui lililotokea. Kitambo kidogo Adili alirudi akaweka mjeledi na mshumaa bwetani. Hakushuku neno, na baada ya kuvua nguo zake alilala tena. Lakini tangu wakati ule mpaka asubuhi, Ikibali hakupata usingizi kwa mawazo mbalimbali. Kila njia ya fikra aliyokwenda haikumfikisha katika tafsiri ya mwujiza ule. Adili Alikuwa mtu wa maana. Hakutazamiwa kufanya ukatili kwa wanyama.


ITAENDELEA....

No comments:

Featured Post

 SOMA SIMULIZI ZENYE KUSISIMUA HAPA A. UTAJIRI WENYE UCHUNGU     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-1     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-2      UTAJIRI WENYE UCH...