KF: FALSAFA YA KIAFRIKA NA NADHARIA YA FASIHI
SWALI LA : Kwa mifano kutoka Pambazuko Gizani (Mboneka) au utungo wa Al-inkishafi (Sayyid Abdallah), jadili umuhimu wa maudhui ya kazi hizo katika kuadilisha jamii. Nini changamoto za waandishi katika uwasilishaji wa maudhui hayo
Maudhui ni mojawapo ya mambo mawili
yanayokamilisha kazi ya sanaa, jambo likamilishalo kazi ya sanaa ni fani au
umbo. Kwa mujibu wa senkoro (1982) “Maudhui hujumuisha mawazo na pengine
mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma mtunzi ama msanii hadi kutunga kazi fulani ya
sanaa”.Pia Wamitila( 2003) anasema “Maudhuini yaliyomo au jumla ya masuala
yanayozungumziwa katika kazi ya fasihi yoyote”. Riwaya ya Pambazuko Gizani imeandikwa na Karumuna Mboneka, mwaka 2004. Riwaya
hii imeelezea safari ya Klaus Mahyofer ambaye anatokea ujerumani na kuja
kutafuta ndugu zake Afrika hususani bubako ambao waliachwa na babu yake Klaus
wa White Fathers. Katika safari yake anakutana na kijana wa kiafrika aliyeitwa Kalinguliza
ambaye alikuwa ni padre.Katika safari yao (Klaus na Kalinguliza ) waliweza
kupita katika parokia mbalimbali zilizokuwa zinamilikiwa na dini na kupitia
safari yao hiyo wameweza kuibua maudhui mbalimbali ambayo yameiadilisha jamii,
Athari za uhujumu uchumi katika jamii. Mwandishi wa Pambazuko Gizani amekemea suala la uhujumu uchumi kwani hupelekea
athari mbalimbali kwa watu wa hadhi ya chini. Mwandishi amemtumia mhusika
Askofu Yona Kyalemile ambaye anaishi jimbo la Bishuba. Askofu huyu anamiliki
jumba kubwa la thamani ambalo lina kila kitu cha kisasa, milango ya umeme ya
kumchukua Askofu kutoka maegesho ya ya gari hadi chumbani mwake, nyumbani kwake
kuna maji ya kutosha, umeme na simu za mikononi, chombo cha kunasia habari za
televisheni za dunia nzima, mashine za kufua na mambo mengine mengi. Lakini
watu wake wa jimbo la Bishuba ni watu mafukara kabisa ambao wanaishi maisha ya
shida. Wanaishi kwenye nyumba za wasiwasi kiasi kwamba wakati wa kipindi cha
mvua hakuna tofauti ya kuwa ndani au kuwa nje. Pia wana tatizo la maji kwani
hutembea umbali mrefu takribani kilometa kumi kuyafuata maji. Mwandishi
anaeleza katika uk.52 kuwa “Pesa
anazozitumia Askofu Yona Kyalemile kuitunza bustani yake kubwa zingeweza
kuwapatia watu wote huduma ya maji.” Pia mwandishi anaeleza suala hili la
uhujumu uchumi pale anapomtumia Klausi akiwa anaelekea Kibona. Alikuwa
anajibizana na kijana mchangamfu ambapo waliongea mambo mbalimbali ikiwemo
suala la viongozi. Klausi anasema kuwa baadhi ya viongozi wa nchi wanasomesha
watoto zao nje ya nchi ambapo huo ni ubadhilifu wa mali. Pia Klausi katika (uk.
29) anasema “Hasa nyinyi mnajibana zaidi.
Juzi tulielekezwa kwamba barabara hii imefanyiwa ukarabati sasa ona
inavyoonekana! maana yake ni kwamba pesa za ukarabati zimeingia kwenye mifuko
ya watu!” Hivyo basi mwandishi amesukumwa kuiandikia jamii kuhusu athari
zitokanazo na uhujumu uchumi kwani ni kikwazo cha maendeleo katika jamii ndio
chanzo kikubwa cha matabaka kwani wale wenye mamlaka watawanyonya wanyonge na
watazidi kuendelea na wanyonge watazidi kudidimia. Kwa hiyo viongozi hawanabudi
kuachana na suala la kuhujumu mali za nchi ili maendeleo yaweze kupatikana.
Athari za ulevi katika jamii. Ulevi ni suala ambalo
linasababisha athari au matatizo mbalimbali katika jamii, Mfano wa matatizo ni
kama kutowajibika kikazi au kifamilia, kufutwa kazi au hata kudharaulika. Hivyo
katika riwaya hii Ya Pambazuko Gizani
mtunzi ameweza kuonesha au kueleza namna ambavyo ulevi unasababisha watu
kutosikilizwa mawazo yao hata kama wanachoongea ni cha msingi na kina manufaa
kwa watu. Kwa mfano amemtumia Padre Prudence ambaye ni msaidizi wa Bwana Mkubwa
katika kanisa katoliki. Padre huyu alikuwa ni mlevi kupindukia na hakupata
nafasi ya kusikilizwa na Bwana Mkubwa alipokuwa akitoa mawazo yake kama
msaidizi wake. Hii inadhihirika katika (uk, 15), Padre Prudence anasema “......ona huyu padre mkubwa ana madaraka
yote. Yeye ni kila kitu hapa. Hatupi nafasi ya kuleta mawazo mapya katika
kanisa letu.” Lakini pia ulevi ulipelekea au ulisababisha padre Prudence
kupangiwa majukumu kama mtoto na malipo yake ni pombe. Mfano katika ukurasa wa
16, Prudence anasema “......kazi
ninapangiwa kama mtoto mdogo, kitulizo pekee ni pombe. Ninakunywa na kulewa na
kama mjuavyo pombe ni pombe tu nikishakunywa inanituma pengine.” Kutokana
na hili, ilimpelekea kufumaniwa, Pia katika jamii zetu ulevi umekuwa changamoto
kubwa ambapo jopo kubwa la vijana ndio wahanga wa ulevi, watu hukosa kazi,
hudharauliwa na kushushwa thamani yote hii ni kutokana na ulevi. Hivyo suala la
ulevi sio zuri kwani lina madhara makubwa kwa mtu binafsi na kwa jamii nzima.
Hutusaidia kujua athari
za uongozi mbaya katika jamii. Mwandishi wa riwaya ya Pambazuko Gizani ameweza kuelimisha jamii juu ya athari za uongozi
mbaya katika jamii. Mwandishi ameelimisha jamii kwa kuonesha namna viongozi
wanavyo watumikisha watu wanaowaongoza bila kujali utu wao bali hujali maslahi
yao. Mfano katika (uk. 14) Padre alipokea mapendekezo ya kuwajengea nyumba
wafanyakazi walio kuwa wakisomba miti na kusaidia ujenzi, lakini padre kama
kiongozi hakukubaliana nalo alisema “Sisi
tumetumwa kueneza neno la Mungu, kujenga nyumba ya Bwana na wala si nyumba za
wapagani hawa ambao bado wanaishi gizani.” Padre mkubwa alikuwa
akiwatumikisha watu na kuwaacha katika giza nene. Suala hili linajitokeza
katika jamii zetu kwa wenye mamlaka au wadhifa fulani kutumia nguvu yake dhidi
ya wale anaowaongoza mfano, kuwatishia kuachishwa kazi. Hivyo, mwandishi anaidhihirishia
jamii ya kuwa ili tuweze kusonga mbele lazima viongozi watumie nafasi zao
vizuri kwa kuleta maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Hutusaidia kuelewa
athari za matabaka katika jamii. Mwandishi wa riwaya ya Pambazuko Gizani amefanikiwa kuonesha matabaka na athari
zinazotokana na matabaka hayo katika jamii. Kwa mfano, mwandishi amemtumia
mhusika Klausi ambaye alikuwa anashangaa meli ya MV-Viktoria kugawanywa katika
matabaka matatu. Daraja la kwanza ni sehemuya wtu wenye pesa, viongozi wa serikali,
na viongozi wa dini. Daraja la pili ni la watu wa kati ambao si maskini na
daraja la mwisho hubeba mizigo pamoja na watu bila tofauti. Mfano wake ni sawa
na jehanamu. Mwandishi ameweza kufanikiwa kuyasawiri vyema maisha halisi ya
waafrika ambayo yamejaa matabaka ambapo matajiri wanapata huduma zote za
kijamii, wanapewa wadhifa mkubwa wa kimadaraka serikalini lakini tabaka la
chini huwa ni tabaka lililosahaulika, hakuna huduma za kijamii kama umeme,
hospitali, maji safi na ni nadra sana kuwapata viongozi wa juu katika tabaka
hili la chini. Mwandishi wa riwaya ya “Pambazuko
Gizani” katika (uk. 8) anazungumzia hilo “......jinsi meli ilivyotegwa, hivyo hivyo na miji kuna mitaa ya daraja
la kwanza, kama Mikocheni, Msasani, na Mbezi. Mitaa ya daraja la pili,
Kijitonyama na Sinza, na daraja la tatu, Tandika na Magomeni.” Hivyo
matabaka haya husababisha watu wengi wasiojiweza kutaabikana hatimaye kufariki
kabla ya kupatiwa msaada husika. Hivyo mwandishi amesisitiza kuwa matabaka ni
kikwazo katika maendeleo.
Athari za mapadri
kubariki ndoa. Mapadre ni viongozi ambao wanapewa dhamana ya kuliongoza kanisa
na kusimamia watu katika suala zima la imani katika parokia mbalimbali. Ambapo
katika kuhudumia jamii katika suala la imani kupitia dini ya kikristo
wanaapizwa kuwa wasiwe na mke au kuoa ikiwa ni pamoja na kutofanya tendo la
ndoa yaani kuwa seja(maseja). Lakini kuna baadhi ya mapadri wanaojiongezea
majukumu mbalimbali tofauti na lengo lao la kufanyika maseja na kuanza
kuwaingilia wanawake na kusababisha watoto wasiotarajiwa. Mfano katika riwaya
yetu ya Pambazuko Gizani katika
ukurasa wa 49, mwandishi anaeleza na kuonesha ni jinsi gani watoto wengi wa
kwanza kuwa ni matokeo ya mapadri kuwaingilia(kufanya tendo la ndoa na wanawake)
wake wa waumini wao kwa kisingizio cha kubariki ndoa. Mwandishi anasema “Inasemekana kwamba, watoto wengi wa kwanza
kwenye familia za kiparokia hiyo enzi hizo walikuwa ni matunda ya baraka za
huyo padre.” Pia suala hili linapelekea baadhi ya watoto kufa ambayo ni
matokeo ya mapadre kufanya tendo la ndoa na waumini wao (uk. 19-20) ambapo
watoto hao wanakufa bila kutajwa majina ya baba zao ikiwa ni nyenzo mojawapo ya
kuficha siri ya mapadre waliokuwa wakifanya tendo la ndoa na wanawake ikiwa kinyume cha maadili ya kazi
yao. Hivyo ni muhimu kila mtu katika jamii yake kufanya kazi sahihi na
kuzingatia maadili ya kazi na maadili ya jamii kwa ujumla ili tuweze kupiga
hatua za kimaendeleo.
Umuhimu wa umoja na
mshikamano katika jamii. Mwandishi wa Pambazuko
Gizani ameonesha kuwa umoja na mshikamano ndio ngao ya maendeleo katika
jamii. Umoja na mshikamano huo unaweza kuwa baina ya watu walio katika ngazi
moja au ngazi tofauti (viongozi na wanaoongozwa). Mwandishi anawatumia wahusika
kama vile Klaus Mahyhofer na Kalinguliza Kamuhanda ambao wameshirikiana haswa
tangu walipokutana katika meli ya MV Viktoria. Mwandishi amesema katika (uk. 8)
“wawili hao walishirikiana na kutokata tamaa, ingawa walinyanyaswa na mapadri,
walinusurika kuuawa, walitembea umbali mrefu hawakukata tamaa. Kupitia wawili
hawa ndio waliofichua uovu unaofanywa na viongozi wa dini kwa kushirikiana na
Ma Paulina. Mfano mwandishi anasema katika (uk. 47) “…….haikuwa kazi rahisi kumtafuta Makokuleba na kumpata. Ilichukua
mwezi mzima, kwani kilikuwa kigumu cha mvua na barabara zilipitika kwa shida
sana. Wakati mwingine tulilala barabarani……” Hii inadhihirisha kwamba Klaus
na Kalinguliza walipitia maisha ya taabu hadi kufanikisha kuipata familia ya
Klaus. Suala hili la umoja na mshikamano linaendana sambamba na jamii zetu za
kiaafrika hususani nchini Tanzania ambapo kwamba kuwepo kwa maelewano, umoja na
mshikamano baina ya viongozi na wananchi kumesababisha kuwepo kwa maendeleo katika nyanja mbalimbali. Hivyo
mwandishi anasisitiza suala hili lazima liendelezwe kwa ajili ya manufaa ya
jamii na taifa kwa ujumla.
Mbali na maudhui ambayo yamejitokeza katika
riwaya ya Pambazuko Gizani, pia kuna
changamoto mbalimbali zinazowakumba waandishi katika uwasilishaji maudhui na
maudhui hayo, nazo ni;
Changamoto katika
lugha, hii ni moja ya changamoto za mwandishi wa kitabu hiki katika
uwasilishaji wa maudhui. Changamoto hii inajidhihirisha katika misamiati
aliyoitumia mwandishi kama vile Majina, inaonekana kuwa majina mengi
yanayotumika kwenye hadithi yamebeba taswira na maana kubwa ndani yake. Kwa
Wahaya hadithi inakuwa na ujumbe mzito kwa kuelewa maana inayobebwa kwenye
majina. Pia kufahamu maana ya majina kunaongeza utamu wa hadithi yenyewe na
kama mtu hajui Kihaya atapata ujumbe nusu wakati majina aliyotumia mtunzi ya
hao wahusika yangetafsiriwa ujumbe ungewafikia watu wengi katika jamii
mbalimbali. Mfano wa majina ya wahusika na maeneo mbalimbali aliyotumia mtunzi
bila kutafsiri kama kalinguliza maana yake ni mtu “anayechunguza chunguza” Kabanga maana ni “mlima”, Mushenyele lina maana “Askofu”,
Bishuba lina maana “uongo”. Hivyo hii
ni changamoto kubwa kwa kuwa ametumia
jamii ya wahaya sana sio watu wote ni Wahaya. Changamoto
ya kimtazamo wa mtunzi. Katika riwaya hii, mtunzi ameonekana kujikita sana
katika suala la dini hasa dini ya kikristo katika dhehebu la kikatoliki. Kwa
kuonesha ni jinsi gani mapadre wa kanisa hilo walivyokuwa wanafanya maasi, kama
kuwa na watoto machotara, kuzaa na wanawake wa kiafrika, kudidimiza dini ya
kijadi, kunyang’anya ardhi na kadhalika. Hivyo hatuelezei wazi kuhusu masuala
ya kiuchumi, kihistoria na kisiasa yanavyopelekea pia kutokea kwa hayo maasi
kama mauaji, na vipi kuhusu huduma za afya kwa hiyo jamii iliyomzunguka, kama
maji, hospitali, elimu, barabara hajafafanua vizuri na hajalieleza kiupana
zaidi. Hivyo hii ni changamoto katika uwasilishaji wa maudhui kwani mtunzi
anautafsiri mwenendo wa kihistoria ya kidini zaidi, na hivyo kushindwa
kuangalia ulimwengu katika nyanja mbalimbali na hata hiyo dini kazungumzia dini
moja ilhali dini ya kiislamu, mtunzi hajaizungumzia.
Kwa
kuhitimisha,mwandishi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuadilisha jamiii katika
kuzungumzia mambo mbalimbali ambayo yanadhoofisha maendeleo ya jamii kama vile
ulevi,kijilimbikizia mali pamoja na matabaka , lakini pia mwandishi amefanikiwa
kuanzisha mjadala juu ya mambo mbalimbali ambayo wengi wetu tunaogopa kuyagusia
,mambo ya imani ambayo wengi wetu tunaamini tu bila kutumia akili mfano mwandishi anaweka wazi kuwa wamishonari
walipokuja watu walippenda maendeleo ya vitu kama vile shule,madawa na nyumba
kuliko walivyotamani dini hiyo ya kigeni ukweli ni kwamba wamishonari walitumia
vitu hivyo walivyotamani watu kama chambo,pia mwandishi anazungumzia swala la
useja na athari zake
Marejeleo
MBONEKA K (2004), Pambazuko Gizani.E & D Limited
WAFULA
R & NJOGU K, (2007). Nadharia ya
uhakiki wa fasihi. Sai Industri Ltd. Nairobi
WAFULA
K.W (2003).Kichocheo cha fasihi Simulizi
na Andishi.Focus Publication Ltd:Nairobi, Kenya