Showing posts with label Fonolojia ya Kiswahili. Show all posts
Showing posts with label Fonolojia ya Kiswahili. Show all posts

Wednesday, July 21, 2021

SWALI NA JAWABU: Fonolojia arudhi katika lugha ya Kiswahili

 


SWALI  : Kwa kutumia mifano kuntu onesha fonolojia arudhi inavyojitokeza katika lugha ya Kiswahili huku ukionesha uamilifu wa kila kipengele


            Fonolojia arudhi,(Mgullu 2010),ni tawi linaloshugulikia maswala mengine ya sauti ambayo huathiri vipashio vikubwa zaidi kuliko fonimu moja, pia huchunguza namna ya kuweka mkazo katika maneno na tungo katika lugha fulani kama vile kiimbo na muundo wa silabi. Fonolojia arudhi ya Kiswahili huchunguza  sifa za kiarudhi ambazo huathili vipashio vikubwa kuliko fonimu na alofoni zake.

          Kiujumla fonolojia arudhi ni tawi linalochunguza sifa za kiarudhi ambazo huathiri vipashio vikubwa kuliko fonimu na alofoni zake.Katika lugha ya Kiswahili fonolojia arudhi inajitokeza kwa namna mbalimbali kama ifuatavyo;

            Lafudhi, ni sifa ya kimasikizi inayohusiana na kusikika kwa sauti wakati wa kutamkwa na msemaji binafsi ambayo humpa utambulisho wa kijamii(kijiografia). Lafudhi ni athari ya lugha ya kwanza kwa lugha ya pili, na kwakuwa lugha ni zao la jamii huwa na mazingira yake ya kijiografia au kieneo inamopatikana, ndio maana suala la mazingira ya kijiografia limehusishwa na lafudhi mfano,

                                    Nakwenda kurara badala ya kulala ( mkurya)

                                    Fyatu fyangu fimeharibika  ( mnyakyusa)

                                    Ntoto nchanga analia( mmakonde)

Katika lugha ya Kiswahili lafudhi ina uamilifu wa kuonesha sehemu ambapo mtu anatoka, mazingira alimo au lugha yake ya kwanza, athari ya lafudhi sio lazima iwe athari ya lugha mama kwa lugha ya pili pia inaweza kuwa athari ya lugha zinazomzunguka  mtu.

            Wakaa, ni mda unaotumika wakati wa utamkaji wa sauti au silabi,kuna baadhi ya wazungumzaji wanaweza kutambulishwa lafudhi yao kutokana na uvutaji au urefushaji wa sauti. Mfano wabena wakiwa wanauliza swali husema,

 Mfano(a)                     kwani huyu mtoto ni wan:ani,?

                         yeye ni mt:oto?

Pia katika lugha ya Kiswahili wakaa hujitokeza katika idadi ya maneno kadhaa  ambayo ni;

Mfano(b)         Majini(mashetani)    _      m:ajini(ndani ya maji)

            Wake  (wanawake walioolewa)        _      w:ake(umiliki)

Uamilifu wa wakaa katika lugha ya kiswahili ni kuonesha tofauti ya maana baana ya maneno,  pia husaidia kubaini lafudhi ya mzungumzaji mfano wabena kwenye mfano(a) hapo juu.

            Kidatu, ni kiwango cha sauti kinachosikika wakati wa utamkaji wa maneno. Kidatu ni sifa ya msikiko wa sauti ambayo humwezesha msemaji kubadili kiwango chake cha sauti kwanzia chini kati hadi juu bila kijali kasi ya mawimbi yake anayoyatoa, katika lugha ya Kiswahili kuna aina tatu za vidatu kuna kidatu juu, kati na chini kwamfano.

                                    Njoo

                                    Njoo

                                    ‘ˉNjoo

Uamilifu wake katika jamii ni kupamba lugha, husaidia kutumia lugha kulingana na mazingira na hetegemea zaidi uhusiano wa wazungumzaji.

            Kiimbo, ni umbo la sauti linalotokana na mpando-mshuko wa sauti za lugha wakati wa usemaji. kila lugha ina utaratibu wake wa kupanda na kushuka kwa mawimbi sauti lakini katika lugha ya Kiswahili kiimbo kimegawanyika katika makundi manne ambayo ni;

(a)kiimbo maelezo – hutoa maelezo, mfano; amefika leo asubuhi kutoka safari.

(b)kiimbo swali  -  kuuliza swali,  mfano; kwanini hujaja?

(c)kiimbo amri  -  kuamuru, mfano;  njoo haraka

(d)kiimbo mshangao – kushangaa, mfano; amekufa !

 kiimbo katika lugha ya Kiswahili huwa na uamilifu wa kubaini lengo la msemaji kama vile kuuliza maswali, kuamuru, kutoa maelezo na kushangaa, kwa kurejelea mfano hapo juu (a-d), pia husaidia kuonesha hisia za msemaji na hali mbalimbali kama vile hali ya masharti, mazoea, uyakinifu na ukanushi

            Mkazo, Ni nguvu inayotumika wakati wa  utamkaji wa sauti za lugha, kila lugha huwa na utaratibu wake wa ujitokezaji wa mkazo lakinikatika lugha ya Kiswahili mkazo hutokea katika silabi ya pili kutoka mwishoni upande wa kushoto mwa neno. Wasemaji wa Kiswahili sanifu walioathiriwa na matamshi ya lugha ya kiarabu huwa wanaweka mkazo katika silabi ya kwanza au ya pili badala ya silabi ya mwisho kasoro moja kama ilivyo kawaida ya utamkaji wa maneno ya Kiswahili sanifu, Huonesha kwamba katika lugha ya kiarabu maneno huwa na mkazo katika silabi ya kwanza au ya pili ya neno.

Mfano(a)                                 Fahamu badala ya fahamu

                                   Mustafa badala ya mustafa

                                    Kubariki badala ya kubariki

Mfano(b)                  Barabara (njia)

                                 Barabara(sawasawa)

Uamilifu wa kiimbo katika lugha ya Kiswahili ni kuonesha utofauti wa maana za maneno kulingana na mkazo wa sauti.

Hitimisho,Vipengele arudhi hupatikana katika lugha zote za mwanadamu ijapokuwa kuna baadhi hupungua kwa baadhi ya lugha mfano katika lugha ya Kiswahili na kinyakyusa kipengele arudhi cha toni hakipo. Pia kukosekana kwake katika lugha husababisha kutokea kwa utata katika maneno au neno ya lugha husika.

 

 

 

 

 

 

    MAREJEREO

Massamba, D, KihoreY na MsanjilaY, (2004), Fonolojia ya Kiswahili sanifu. TUKI: Dar es salaam.

Mgullu, R.S.(2010). Mtaala wa isimu: Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi:Phoenix.

TUKI(2004) Kamusi ya Kiswahili sanifu. Dar ea salaam: TUKI.

Featured Post

 SOMA SIMULIZI ZENYE KUSISIMUA HAPA A. UTAJIRI WENYE UCHUNGU     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-1     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-2      UTAJIRI WENYE UCH...