Saturday, October 30, 2021

ADILI NA NDUGUZE -sehemu ya 2

 

ADILI NA NDUGUZE - 2

  


Simulizi : Adili Na Nduguze 

Sehemu Ya Pili (2)




Mwenyeji na mgeni waliondoka vitandani. Baada ya kuoga na kuvaa walikwenda sebuleni kustaftahi. Walipokwisha walikwenda mazizini kutazama wanyama waliokusanywa. Siku ile moyo wa Ikibali ulikuwa mzito kwa mawazo, lakini hakuuliza neno juu ya siri aliyogundua. Ilikaa moyoni mwake mwenyewe. Siku ya pili , usiku wa manane vile vile, Adili alifanya tena mambo aliyofanya jana. Siku ya tatu mambo yalikuwa yaleyale. Katika muda huu wote Ikibali hakuacha siku hata moja kumfuata na kutazama matendo yake. Siku ya nne alipewa hesabu aliyojia akarudi ughaibu. Kwa kesha ya siku tatu hakuweza kuongoza vema farasi kwa usingizi. Laiti asingalikuwa mzoefu wa kupanda farasi angalitupwa chini njiani amelala.



Alipofika Ughaibu alitoa habari za ujumbe wake. Alitaka sana kuficha siri ya manyani ya Adili na adhabu yao, lakini hakuweza. Alifikiri kama Adili aliyaadhibu kwa ukatili tu asingalijisumbua kuyafuga, kuyalisha na kuyanasihi. Mtu hawezi kutunza kitu asichokijali. Zaidi ya umahiri, werevu na usuluhifu, Ikibali aliweza kufahami upandw wa pili wa neno. Aliona dhahiri kuwa Adili hakupenda adhabu ile kuendelea. Kama aliitenda kwa kulazimishwa alikuwa na haki ya kusaidiwa. Yamkini mfalme aliweza kumsaidia. Kwa sababu hii alitoa siri aliyokuwa nayo. Rai aliposikia nywele zake zilisimama kichwani, na damu yake ikasisimka mwilini. Ikibali alitumwa tena Janibu kumleta Adili pamoja na manyani yake mbele ya mfalme.



Adili Mbele ya Rai



Uso wa Ikibali ulikuwa na haya na moyo wake ulijaa hisani. Alikuwa tayari kutumika kama alivyotakiwa na mfalme, lakini alichelea kuwa haini kama siri aliyotoa ilikuwa maangamizi ya Adili. Alijuta ulimi wake haukuwa na nadhari. Hapana roho mbinguni wala duniani isiyopatwa na majuto. Tuna busara nyingi sana baada kuliko kabla ya neno kufanyika. Kama taratibu ya msaada haikufaulu, Ikibali hakupenda kumkabili Adili. Wakati ule ule hakuweza kughairi dhima yake. Ugomvi baina ya hiari na dhima ulianza moyoni mwake. Mambo haya mawili hayatimiziki mara moja. Hapana mtu awezaye kwenda njia mbili wakati mmoja. Kwa hivi, Ikibali alitii mahitaji ya dhima yake akaenda janibu.



Adili alipoona Ikibali amerudi alishtuka. Alisema moyoni mwake ataokolewa katika uovu aliolazimishwa lakini hakuupenda kuutenda. Baada ya hayo alimuuliza Ikibali neno lililomrudisha ghafla Janibu. Ikibali alijibu asingalirudi ghafla vile, lakini katika jitihada yake ya kutenda wema ametenda nuksani. Alikuwa hana udhuru wa kujitetea katika lawama lake. Ulimi wake mwenyewe umemponza. Aliungama alipofika Janibu mara ya kwanza alishawishika kumpeleleza Adili siku tatu. Kila usiku alipokwenda kuadhibu manyani, yeye alimfuata nyuma. Aliporudi nyumbani kulala, yeye alitangulia mbele. Mambo aliyotenda kwa manyani yalikuwa ajabu kwake. Hakupata kuuliza sababu yake. Aliporejea Ughaibu alizungumza habari zile kwa mfalme. Mfalme aliposikia alimrudisha janibu kumchukua Adili na manyani yake.



Adili alikuwa mwema na msamehevu. Alibaini kama Ikibali alilaumika kwa kufichua siri, kadhalika yeye mwenyewe alilaumika kwa ukatili. Tafakuri ilimwonyesha Adili kuwa ukali wa mbwa huyokana na msasi. Mbwa wa msasi mkali ni wakali pia. Rai alikuwa mfalme mwadilifu. Ilijuzu Ikibali, mjumbe wake, kuwa mchunguzi hodari. Mambo yaliyogunduliwa yalikuwa kweli. Mambo yenyewe hayakumpendeza Adili mwenyewe, licha ya mfalme na mjumbe wake. Kipawa kimoja katika vipawa bora kwa mwanadamu ni ujuzi wa maovu. Adili alibarikiwa kipawa hiki. Alishukuru kuwa siri iliyogunduliwa imefika katika masikio ya mfalme. Adili mwenyewe alitaka ijulikane, lakini alichelea kuwa haini kwa mfadhili wake. Madhali imefichuka alikuwa tayari kuithibitisha.



Adili alijiandaa kwa safari ya kuitika mwito wa mfalme. Farasi watatu walitandikwa matandiko mazuri. Yeye alipanda farasi mmoja na mmoja kwa kila nyani. Ikibali alipanda farasi wake mwenyewe. Farasi wa Adili na yule wa Ikibali walikwenda sambamba njiani. Nyuma yao yaliandama manyani juu ya farasi. Kila mtu aliyeona manyani yamepanda farasi alistaajabu. Mnyama kupandwa na mnyama ilikuwa upeo wa miujiza kwa watu. Vinywa vya umati wa watu vilikuwa wazi kwa kivumo cha Lo salala! Wakati umefika wa mawe kusema, miti kujibu na wanyama kuwa watu! Ikibali aligeuza uso wake kwa Adili akasema kwa ucheshi. "Mbwa wanatubwekea kama walionusa mtara wa windo." Adili alikubali kwa kuinamisha kichwa akatabasamu, walisafiri hivi mpaka Ughaibu. Baada ya kutua Adili alipelekwa mbele ya mfalme na manyani yale.



Manyani yalipomwona mfalme yalifanya ishara mbili. Kwanza yaliinua juu mikono yao kama yaliyokuwa yakiomba, pili yalilialia kama yaliyodhurumiwa. Ishara ya kwanza ilionyesha ombi la msaada, na ile ya pili ilionyesha mashtaka. Licha ya Rai, hata mimi na wewe tungalifasiri hivi kama tungalikuwa katika baraza hiyo. Mfalme alipoona vile alitaka kujua kwa Adili sababu ya kuadhibiwa, kulishwa na kunasihiwa manyani yale kila usiku. Katika sababu zake alionywa kusema kweli tu. Adili alijibu kuwa waungwana hawasemi uongo. Atasema kweli, na manyanai yatakuwa mashahidi. Maneno yake yakiwa uongo, yatakanushwa na manyani kwa mguno, lakini yakiwa kweli, manyani yatayathibitisha kwa kuziba nyuso kwa viganja vya mikono yao. Sasa kisa baada ya kisa juu ya manyani kilisimuliwa.




Ndugu Zake




Katika kisa cha kwanza Adili alisema manyani yale mawili yalikuwa ndugu zake. Baba yao alikuwa mmoja na mama yao mmoja. Baba yao aliitwa Faraja. Faraja alikuwa mtoto wa pacha. Wakati wa kuzaliwa pacha huyo mtoto mmoja alikufa pakabaki mmoja. Huyu aliyebaki aliitwa faraja kwa sababu aliwafariji wazazi wake katika msiba wa ndugu yake. Alipokuwa wazazi wake walimwoza mke, yaani mama yao. Mama yao alichukua mimba ya kwanza akazaa mwana aliyeitwa Hasidi. Alichukua mimba ya pili akazaa mwana vile vile aliyeitwa Mwivu. Alichukua mimba ya tatu akazaa mwana tena aliyeiywa Adili. Walilelelewa mpaka wakawa watu wazima wenye vichwa vilivyofunzwa lakimi mioyo iliyosahauliwa. Busara kubwa kichwani haina faida kama moyoni hamna chembe ya wema.



Baba yao alipokufa aliacha shamba zuri, duka kubwa, mifugo mbalimbali na nakidi shilingi hamsini elfu. Walimzika kama desturi wakafanya matanga. Siku arobaini zilipopita, Adili alikaribisha matajiri na watu maarufu wa janibu karamuni. Karamu ilipokwisha Adili alitamka kuwa maisha ni safari, na dunia ni matembezi kwa wanadamu. Maskani yao ya milele yako peponi. Hapana mtu ambaye atabaki duniani. Baba yake amekufa akiacha mali nyingi. Alichelea kuwa walikuwako watu waliomdai au walioweka amana kwake. Alitaka kila mtu apate kulipwa ili aindoe lawama la baba yake ulimwenguni. Baada ya kusema hivyo kimya kikubwa kilitokea. Watu walinyamaza kama waliokuwa wamenyang'anywa ndimi zao.



Halafu walijibu kwa umoja kuwa hawakuweza kuuza pepo kwa dunia. Walikuwa wacha Mungu na wafuasi wa haki. Walifahamu halali na haramu. Jambo moja katika mambo waliyokimbia kabisa lilikuwa mali ya yatima. Walimfahamisha Adili kuwa mali ya baba yake ilikuwa imebaki mikononi mwa watu. Bila shaka watu hao watamlipa. Hapakuwa na mtu hata mmoja miongoni mwao aliyedai kitu kwa marehemu. Walithibitisha kuwa walimsikia mara nyingi baba yake Adili akisema kuwa alichelea sana deni. Katika uhai wake alizoea kuomba asife na deni. Tabia ya baba yake ilikuwa kamili. Kila karadha aliyochukua alilipa kabla ya kudaiwa. Alipokopesha kitu kwa mtu hakudai kwa fadhaa. Wadeni wake walimlipa pole pole. Mtu aliyekuwa hana njia ya kulipia alisamehewa.



Adili aliwashukuru kwa kuhudhuria karamuni na kwa kumpa hakika ya ukamilifu wa baba yake. Wageni walipokuwa wanakwenda zao waliambiana njiani,

"Mwana wa mhunzi asiposana huvukuta. Adili atakuwa mwema kama baba yake."



Sasa Adili aliwaambia ndugu zake kuwa kwa ushahidi uliotolewa alitosheka kuwa baba yao alikuwa hadaiwi na mtu. Urithi walioachiwa ulikuwa mkubwa sana. Warithi walikuwa watoto watatu tu. Aliuliza kama ndugu zake walipenda urithi ule ugawiwe kila mtu achukue sehemu yake, au uachwe kama ulivyokuwa ili watumie shirika. Ndugu zake walitaka urithi ugawiwe kati yao.



Adili alikwenda kumwita kadhi. Kadhi alipokuja aligawa urithi wao katika mafungu matatu. Mafungu yote yalikuwa sawasawa kwa thamani. Kila mmoja alipata fungu lake. Adili alichukua shamba na duka. Mali nyingine walioewa ndugu zake.



Basi Adili alifungua duka lake. Alinunua bidhaa akatia dukani mpaka likajaa tele. Alikaa kitako akafanya biashara. Ndugu zake walinunua marobota ya ngozi na bidhaa nyingine wakafanya safari ya kwenda nchi ngeni kufanya biashara. Siku ya kuagana nao, Adili aliomba Mungu awabariki ndugu zakw ugenini, naye ampe riziki yake kwao. Alifanya biashara kwa muda wa mwaka mmoja. Hakuacha kuhesabu kitu alichonunua wala alichouza. Vitu vyote, kilichoingia ndani na kilichotoka nje , vilitiwa daftarini kwa uangalifu. Mali bila ya daftari hupotea bila habari. Adili alikuwa macho sana juu ya neno hili. Aliweka hesabu ya kila siku na ya kila mwezi. Mwisho wa mwaka alipolinganisha faida na hasara aliona amepata mali kama ile iliyoachwa na baba yake. Hakika mtu anayehesabu mapato na matumizi yake hafi maskini.



Siku moja Adili alikuwa amekaka dukani pake. Ulikuwa wakati wa baridi. Alikuwa amejifunika mablanketi mawili. Moja lilikuwa la sufu na jingine la pamba. Aliona ghafla watu wawili wanakuja dukani. Walikuwa hawana kitu. Kila mmoja alivaa kanzu mbovu bila ya nguo nyingine ndani. Midomo yao ilibabuka kwa baridi. Alipotambua kuwa walikuwa ndugu zake, moyo wake uliwaka moto kwa huzuni. Watu aliowapenda walikuwa katika hali mbaya sana. Aliondoka kitini akaenda kuwakumbatia. Mitiririko ya machozi ya moto ilitoka machoni mwake. Hakuweza kujizuia kulia kwa sababu ya mapenzi makubwa aliyokuwa nayo juu ya ndugu zake. Mapenzi yakw yalitoneshwa na hali mbaya waliyokuwa nayo.



Adili Alikuwa tayari siku zote kugawana na mtu yeyote tonge moja la chakula lililokuwa mikononi mwake. Alipoona ndugu zake katika matambaa hakuweza kuhimili. Uchi wao ulikuwa uchi wake. Alivua mablanketi yake mwenyewe akampa kila mmoja lake.



Maji ya moto yalitengenezwa akawapeleka msalani kuoga. Kisha alitoa sandukuni vikoi viwili, fulana mbili, kanzu mbili, jozi mbili za viatu na kofia mbili akawapa. Vitu hivyo vilikuwa vizuri na thamani yake ilikuwa kubwa sana. Baada ya kuvaa nguo walikaribishwa sebuleni. Wakati ule hali yao ilikuwa bado dhaifu sana kwa uchovu na njaa. Chakula kililetwa katika sinia moja ya dhahabu iliyonakshiwa kwa fususi. Walitafadhalishwa kula chakula wakala mpaka wakashiba.



Adili aliyageukia manyani akauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea. Manyani yaliziba nyuso kwa viganja vyq mikono yao kwa aibu.




Mgawo Mwingine



Katika kueleza msiba wao, ndugu zake Adili walisema walipoondoka Janibu walikwenda Gube. Walianza kuuza bidhaa zao huko. Ngozi iliyonunuliwa Janibu kwa shilingi moja iliuzwa kwa shilingi kumi, na ile ya shilingi mbili kwa shilingi ishirini. Walipata faida kubwa sana. Baadaye walinunua viatu kwa bei ya shilingi kumi jozi moja. Viatu hivyo vingalifika Janibu vingaliuzwa kwa shilingi arobaini kila jozi. Walipotoka Gube walikwenda mji wa Gharibu wakafanya biashara kubwa kuliko ya mara ya kwanza. Walishindwa kujua hesabu ya fedha waliyoipata, walisifu uzuri wa miji waliyokwenda, usitawi wa biashara na fauda iliyopatikana huko.



Mtu kushindwa kujua pato lake mwenyewe huonyesha uchache wa uangalifu. Lakini Adili hakusema neno juu ya hili. Ulikuwa si wakati wa kusema makosa. Ndugu zake walitaka huruma wakati ule siyo kulaumiwa.



Kisha waliendelea kusema kuwa msiba wao ulikuwa hausemeki. Walipoona wamepata mali nyingi hawakufurahi kukaa ugenini tena. Iliwatokea dhahiri kuwa mtu huchuma juani akala kivulini. Kwa kila mtu kwao ni kivulini na ugenini ni juani. Fikira hii ilipowatopea walifanya safari ya kurudi kwao. Basi walijipakia chomboni. Kwa muda wa siku tatu safari yao ilikuwa njema, lakini siku ya nne bahari ilichafuka. Mvua ilianza na giza lisilopenywa na nuru lilifunika bahari. Mchana ulikuwa kama usiku. Palitokea radi na umeme. Dhoruba kali iliandama nyuma. Mawimbi makubwa kama milima katika bahari isiyopimika kina yaliwakabili. Jahazi yao ilipeperushwa kama jani mwambani ikavunjika. Shehena ya mali ilikuwa chomboni ilitota. Fikira ya mali yao haikuwajia. Waliomba wokovu wa maisha yao tu. Kwa msaada wa mbao chache zilizopatikana katika chombo kilichovunjika, walielea baharini mchana na usiku kwa muda wa siku sita.



Siku ya saba, walipokuwa karibu kukata tamaa, jahazi ilipita karibu yao. Mabaharia wa jahazi hiyo waliwaokoa. Jahazi iliyowaokoa ilikuwa na safari ya kwenda nchi nyingine. Iliwapasa kuwa katika safari zile na kufanya kazi bila ijara chomboni. Waliposhuka katika kila bandari waliyofika waliomba chakula katika baadhi ya miji walipewa chakula, lakini katika miji mingine hawakupata kitu. Kwa hivi, waliuza nguo walizovaa wapate fedha ya kununulia chakula. Uchi wao uliweza kungojea nguo, lakini njaa yao haikuweza kungoja chakula. Waliapata robo tatu za mashaka ya dunia toka siku waliyokufa maji mpaka siku waliyofika kwao. Laiti waaingalipatwa ma bahati mbaya wangalirusi Janibu na utajiri mkubwa.



Ndugu zake walikuwa masogoro katika kusema. Walijifunza sana kutumia ulimi na midomo. Adili alivutwa na maneno yao siku zote. Hakujua kama tumaini lake juu ya ndugu zake lilikuwa kazi bure. Walikuwa waovu katika kila inchi ya miili yao. Baada ya kuwasikiliza aliwapa pole. Alisema kuwa mali hufidia roho lakini roho haifidiwi na kitu. Salama ya maisha yao ilikuwa bora kuliko faida iliyopotea. Umaskini umetengana hatua moja tu na utajiri. Kwa kuwa vitu vile vimekaribiana sana, wako watu katika dunia waliopata kuonja uchungu wa umaskini na ladha ya utajiri. Madhali ndugu zake wameonja uchungu wa umaskini, aliwakuza moyo kutazamia ladha ya utajiri wakati ujao.



Siku ya pili Adili aliwachukua ndugu zake kwa kadhi. Alipofika aliomba mali yake igawanywe mafungu matatu sawasawa kati yao. Alifanya hivyo kwa kuwaambia mali ile pia ilitokana na baba yao. Kila mtu alichukua fungu lake akafungua duka. Adili aliomba dua kuwa ndugu zake na yeye wote wabarikiwe. Aliwaonya wenziwe hatari ya uvivu na hasara ya ulevi. Aliwapa chakula na haja nyingine za lazima bure siku zote. Walikaa nyumbani mwake raha mustarehe. Mara kwa mara walipokuwa pamoja, Adili aliambiwa sifa za nchi ngeni. Ndugu zake walikumbuka mali yao na usitawi wa biashara walioona. Walimvuta Adili kusafiri pamoja nao tena kwa sababu faida za safari, yaani kufarijika katika hamu, kujua namna ya kuendesha maisha, kupata elimu mpya, kuelewa tabia za watu mbalimbali, kukutana na marafiki wa kweli kushinda ndugu, na mtu mwenye bahati mbaya kwao huweza kupata bahati njema ugenini.

Adili aliyageukia manyani akauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea. Manyani yaliziba nyuso kwa viganja vya mikono yao kwa aibu.





Tandu na Nyoka



Moyo hauhimili mshawasha wa mfululizo. Hasa mshawasha wenyewe ukitokana na mtu unayempenda au tamaa ya utajiri. Moyo wa Adili ulikuwa na mapenzi makubwa juu ya ndugu zake. Aliwapenda kama pumzi ya maisha yake mwenyewe. Aliposikia maneno yao alisema haikuwezekana katika maisha yake kukataa haja iliyotakiwa na ndugu zake. Alikubali kusafiri pamoja nao walikopenda.



Fedha ya kuchanga kwa ajili ya safari iliyokusudiwa ilikisiwa. Mafungu matatu sawasawa yalitakiwa. Fungu la kila mtu lilipokusanywa jumla kubwa sana ya fedha ilipatikana. Walinunua ngozi na bidhaa nyingine. Halafu walikwenda bandarini wakaajiri jahazi kubwa. Walipakia mali yao na vyakula mbalimbali. Siku ya pili walipakia chomboni wakasafiri.


ITAENDELE

No comments:

Featured Post

 SOMA SIMULIZI ZENYE KUSISIMUA HAPA A. UTAJIRI WENYE UCHUNGU     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-1     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-2      UTAJIRI WENYE UCH...