Saturday, October 30, 2021

ADILI NA NDUGUZE -sehemu ya 3

 

ADILI NA NDUGUZE - 3

  


Simulizi : Adili Na Nduguze 

Sehemu Ya Tatu (3)





Adili alisumbuka safarini kwa sababu ilikuwa mara yake ya kwanza kusafiri baharini. Baada ya safari ya siku tatu walifika bandarini. Bandari yenyewe ilikuwa ya kwanza katika bandari walizokusudia kwenda. Walishuka wakafanya biashara. Kwa faida iliyopatikana pale, Adili alisadiki maneno yaliyosemwa na ndugu zake. Waliondoka pale wakaenda mji wa pili. Huko walifanya biashara vile vile wakapata tija kubwa kuliko ya kwanza. Walikwenda mji wa tatu wakauza bidhaa zao kwa faida kubwa pia. Kabla ya kufika miji yote waliyokusudia kwenda, waliona wamekwisha rudisha thamani ya mali yao, na faida iliyopatikana ilikuwa kubwa sana. Nusu moja ya mali waliyokuwa nayo ilikuwa imeuzwa. Palibaki nusu ya pili kuuzwa. Walikwenda miji mingine.





Baada ya safari siku moja walifika jabalini. Nahodha aliamuru kutua tanga na kutia nanga. Kisha mabaharia walitakiwa washuke jabalini kutafuta maji kwa sababu jahazini mlikuwa hamna maji hata tone moja. Pipa la maji jahazini lililotosha kwa mwezi mmoja lilitoboka. Maji yake yalivuja bila ya kujulikana na mtu. Mabaharia wote walishuka wakatafuta maji chini ya jabali. Adili alipanda juu ya jabali. Huko aliona tandu linakimbia. Rangi yake ilipendeza sana. Iling'ara kama kioo. Nyuma yake lilifuatwa mbio na nyoka aliyetisha kabisa. Nyoka alipolifikia aliliuma kichwani. Kisha alilibana jiweni. Tandu lilitoa mlio wa kusikitisha. Kwa mlio ule Adili alijua kuwa tandu lilikuwa hatarini. Mara ile moyo wake uliingiwa na huruma. Hakuweza kuvumilia. Aliokota jiwe liliokaribia uzito wa ratili moja akamtupia nyoka. Jiwe lilimpiga nyoka kichwani. Ilikuwa shabaha nzuri sana. Kichwa chote kilipondeka kwa pigo moja akafa mara ile.



Ghafula tandu lilijigeuza mwanadamu, yaani, msichana mzuri. Uso wake ulivuta macho ya Adili kwa haiba yake kubwa. Mbele ya wanawake mia moja wazuri, msichana huyo angalitokea, wote wangalijichukia wenyewe kwa kujiona hawakulingana nae kwa uzuri. Tazamo la mwanamume yeyote lingalivutwa kama angalitokewa na msichana huyo. Alikwenda kwa Adili akampa mkono. Alimshukuru kwa wema aliomtendea. Adili aliombewa dua na msichana apate himaya mbili. Himaya ya dunia na himaya ya ahera. Ya kwanza imfae katika maisha yake, na ya pili imwokoe siku ambayo mtu hatafaliwa na kitu kingine ila wema aliotenda. Kama alivyookolewa msichana aliahidi kutenda neno lolote jema kwa Adili katika wakati ujao.



Baada ya hayo msichana alielekeza kidole chake cha shahada chini. Mara moja ardhi ilipasuka akaingia ndani yake. alipokwisha jitia ndani ardhi ilijifunga sawia. Msichana hakuonekana tena. Adili alifahamu kuwa alikuwa si mwanadamu ila jini. Kitambo kidogo aliona nyoka aliyemwua anawaka moto. Mara moja alikuwa majivu matupu. Kufumba kope na kufumbua mahali palipokuwa na majivu palitokea chemchemi ya maji safi. Mambo haya yalikuwa mwujiza mkubwa sana kwa Adili. Alirudi kwa wenziwe na habari za ugunduzi wa maji. Adili alishangiliwa sana kwa ugunduzi wake. Walipkwisha chota maji ya kutosha walilala. Asubuhi walitweka wakasafiri baharini mchana na usiku kwa muda wa siku thelathini. Walikuwa hawaoni bara wala kisiwa. Maji yao yalikwisha tena.



Nahodha alipotangaza chomboni kuwa maji yamekwisha mabaharia waliomba chombo kielekezwe upande wa bara. Lakini nahodha aliapa kuwa hakujua upi ulikuwa upande wa bara toka mahali walikokuwako. Aliposema hivyo mioyo yao ilihuzunika machozi yakawatoka machoni njia mbili mbili. Walikuwa hawana neno la kutenda ila kuomba hifadhi ya Mungu. Siku ile walilala na kihoro. Kulipokucha waliona jabali refu sana baharini. Walianza kufurahi tena.



Tanga liligeuzwa wakaenda jabalini. Walipolikaribia walitua. Kisha walishuka chomboni wakapanda jabalini kutafuta maji. Hali zao zilikuwa dhaifu kwa kiu. Walitafuta hiku na huko lakini hawakuona maji. Adili alipanda juu zaidi. Huko alitazama upande wa pili wa jabali akaona kwa mbali sana akaona ukuta umezunguka. Ilipata mwendo wa robo saa toka jabalini mpaka ulikokuwa ukuta. Aliwaita wenziwe waliokuwa chini ya jabali.



Walipokuja aliwaonyesha ukuta alioona. Alidhani ndani yake ulikuwako mji mkubwa ambako maji na vitu vingine viliweza kupatikana. Basi aliwashauri wenziwe kwenda kule. Wenziwe wote walikataa kwenda. Walichelea kuwa mji wenyewe usije kuwa wa watu wabaya. Wakikamatwa utakuwa mwisho wa maisha yao. Kwa vile walivyokuwa katika hatari ya kiu, hawakuweza kujasiri katika hatari nyingine kwa tamaa ya maji. Walikataa kwenda wakajitolea wenyewe kufa kwa kiu, Lakini Adili hakukubali. Moyo wake ulikuwa imara sana. Alitaka kujaribu kujiokoa kwanza kabla ya kujitolea kushindwa. Ilikuwa idhilali kwake kujilegeza mbele ya shida iliyowezekana kushindwa. Kwa hivi, alisema kuwa hakua na mamlaka juu ya mabaharia wote, lakini alitaka kwenda na ndugu zake. Lo, ndugu zake waliruka wakakataa kufuatana naye. Walionywa na Adili kuwa mwanadamu ameumbwa kwa heri na shari, na hasa kwa heri.



Ilikuwa hasara iliyoje kutazamia shari tu katika maisha! Juu ya onyo hili ndugu zake hawakuwa tayari kwenda naye. Basi aliwaomba wamngoje jabalini. Walipokubali kufanya hivyo alikwenda zake peke yake kujaribu bahati yake.



Adili aliyageukia manyani akauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea. Manyani yaliziba nyuso kwa viganja vya mikono yao kwa aibu.




Mji wa mawe



Adili alikwenda mpaka ulikokuwa ukuta alioona. Kimo cha ukuta wenyewe kilikaribia futi arobaini. Juu ulikuwa na upana wa futi kama ishirini. Wote ulikuwa wa mawe yaliyowekwa kwa imara na ustadi. Mivule , mikangazi, mibuyu na miti mingine ya magogo manene iliota juu yake. Miti yote iligeuka mawe, lakini rangi ya majani yake ilikuwa ya kijani. Maki ya ukuta wote ilikuwa futi ishirini. Duara kubwa sana ilikuwa katikati ya ukuta huo. Katika duara hiyo ulikuwako mji uliokuwa na majengo mazuri sana . Milango mia moja ilikuwa ukutani, na kila mlango ulitengana na mwingine kwa umbali wa maili hamsini. Milango yote ilikuwa ya chuma kilichokuwa na maki ya futi saba. Ulikuwa mji mzuri na wenye ngome bora duniani.



Milango yake ilikuwa wazi. Adili alipotaka kuingia ndani aliona mtu amesimama mlangoni. Kichaka kikubwa sana cha funguo kilikuwa mkononi mwake. Adili alidhani mtu yule alikuwa bawabu. Alikwenda karibubyake akamwamkia. Hakujibu neno. Alimwamkia mara ya pili na ya tatu lakini hakujibu hata kidogo. Adili alishangazwa na adabu ya mtu aliyemwamkia.



Alidhani hakuelewa lugha yake. Lugha ni pingamizi kubwa kwa watu duniani. Kwa hivi alimwamkia kwa ishara. Hili liliposhindwa kufaulu alimsogelea akamshika begani. "Bwana umelala nini?" Hakujibu wala hakutikisika. Alizidi kumtazama na kumshika mwilini. Alipofanya hivyo aliona kwamba alikuwa si mtu ila jiwe lililokuwa halina maisha. Ugunduzi huu ulitia mzizimo wa hofu katika moyo wa Adili lakini alijikaza. Adili alikuwa si mtu wa kukata tamaa. Tamaa kwake ilikuwa gurudumu la maisha naye alijua namna yakuitawala. Mzizimo wa hofu iliyotambaa moyoni mwake uliyeyushwa na udadisi wake mkubwa.



Aliondoka aliposimama akaingia ndani kidogo. Huko aliona mtu mwingine amesimama barabarani. Alimkaribia akamtazama. Lilikuwa jiwe vilevile. Alizungukazunguka barabarani. Kila alipokwenda alitazama huku na huko. Mabarabara yote yalikuwa yamejaa watu waliosimama, Lakini wote walikuwa mawe matupu. Alipofika sokoni aliona umati mkubwa wa watu. Baadhi yao walikuwa wamekaa kitako na wengine walikuwa wamesimama wima. Mbele ya watu waliokaa palikuwa na vikapu vya nafaka iliyogeuka chngarawe, unga uliokuwa vumbi, matunda yaliyobadilikia komango, na vitu vinginw vya biashara vilivyogeuzwa mawe. Vyote vilikuwa katika hali iliyokuwa haifai kwa chakula. Sababu iliyoweza kueleza mabadiliko yale ilikuwa bado kuonekana. Kwa hivi, Adili aliazimu kuitafuta kwa kila hali. Adili alikuwa na uchunguzo uliomwongoza katika ugunduzi mkubwa.



Alipoondoka sokoni aliona nyumba moja kubwa barabarani . Milango yake ilikuwa wazi. Hili lilikuwa duka la tajiri mkubwa. Alipoingia ndani aliona mwenyewe amelala juu ya kitanda cha dhahabu. Kitanda chenyewe kilitandikwa nguo nzuri na matakia ya zari teule. Mbele yake palikuwa na kabati lililokuwa na kimo cha futi kumi na upana wa futi tano. Tajiri mwenyewe alikuwa mgumu na baridi kama jiwe; na vitu vyake vyote kadhalika. Adili alitazama kabatini akaona mifuko imepangwa safu. Alishika mfuko mmoja lakini kitambaa chake chote kilikuwa vumbi. Vitu vilivyokuwa katika mifuko hiyo ilikuwa sarafu ya dhahabu tupu. Hii haikubadilika mawe wala vumbi. Alijaribu kuchukua dhahabu, lakini hakuweza kama alivyopenda. Moyo wake uliingiwa na fikira kwamba kama angalikuja na ndugu zake wangaliweza kuchukua dhahabu ya kutosha.



Alipotaka kutoka nje aliona makabati yaliyotiwa nguo za hariri na sufu. Nguo hizo zilikuwa za rangi mbalimbali na za almaria bora. Aliponyoosha mkono wake kuzishika zilikuwa vumbi kama vitambaa vya mifuko ya dhahabu. Alitoka akaingia duka jingine. Huko aliona mali nyingi sana kuliko alizoona katika duka la kwanza. Ah, maskini! Mali ilipatikana lakini haikuwa na wachukuzi. Watu waliokuwa na njaa na jahazi yao iliyotaka shehena walikuwa wamesimama kando kwa zembe. Jahazi ilifika nchi ya dafina ya ajabu, lakini mabaharia wake hawakushuka pwani kuipakia. Kula uhondo kwataka matendo. Asiye matendo hula uvundo.



Adili alikuwa kama chura kilichofurahia mvua lakini kilikuwa hakina mtungi wa kuwekea maji. Alitamani kuwa na nguvu za ndovu ili achukue dhahabu ya kutosha lakini haikuwezekana. Basi aliingia hapa akatoka. Alikwenda pale akaondoka na fikira ya mwujiza alioona.



Kila barabara aliyopita ilikuwa na watu, ng'ombe , farasi, nyumbu, punda na mbwa , lakini wote walikuwa mawe matupu. Hofu kubwa ilitambaa moyoni mwake kuwa naye asijegeuzwa jiwe. Lakini alijifariji kuwa labda ilikuwako sababu ya mji ule, wanyama na vitu vyake kuwa mawe, na kuwa lile lilikuwa fundisho kwake. Wazo hili lilimpa nguvu akaendelea kupeleleza. Alipoingia katika maduka ya masonara aliona wenyewe wamegeuka mawe. Mikono yao ilikuwa imeshika vito vilivyokwisha tengenezwa. Vito vingine vilikuwa ndani ya mikebe. Alipoona vile alitupa mbali dhahabu aliyokuwanayo kwanza akarukia vito kwa pupa . Lakini mara moja alisimama kwa mshangao. Alijiona amekaliwa na uzito wa vitu alivyopapia. Juu ya uzito huo hakuweza kuongeza hata pini moja ya shaba. Vitu vilivyobaki vilimtazama kama vilivyokuwa vikimsimanga kwa choyo yake. Tamaa ya mali ni kubwa. Mioyo mingi haitoshwi na mali. Walakini, kwa kweli fikira ya mali isiyo kadiri ni mzigo usiochukulika.



Alipotoka pale aliingia katika maduka ya majohari. Huko aliona wenyewe wamekaa vitini. Mbele ya kila tajiri lilikowako bweta. Mabweta hayo yalijaa yakuti, almasi, fususu, lulu, feruzi na majohari mengine. Matajiribwote walikuwa mawe. Alitupa chini vito vilivyotengenezwa akachagua yakuti; aliacha yakuti akashika almasi; alikataa almasi akatwaa fususi; alitaka lulu badala ya fususi na feruzi kwa majohari mengine.



Alikuwa hana nguvu ya kuchukulia majohari yote. Kiasi cha majohari aliyoweza kuchukua hakikupunguza wingi alioukuta. Majonzi yalimjia akasikitika juu ya ndugu zake kwa kukosa kufuatana naye. Ndugu zake walikuwa na miguu ya kwendea bali hawakuitumia; walikuwa na nguvu za kuchukulia tunu zilizotosha kwa utajiri wao lakini hawakuwapo. Hili lilimwonyesha Adili kuwa maumbile yalikuwa si bahili. Yalikuwa karimu katika kugawa vipawa. Lakini zaidi ya nusu ya hasara za wanadamu hutokea kwa sababu wenyewe hawataki kutumia vipawa vyote walivyopewa. Basi alichukua alichoweza akaendelea mbele. Moyo wake ulijaa majuto juu ya ndugu zake aliopenda kushiriki nao furaha ya ugunduzi, fahari ya usitawi wa utukufu wa matendo bora.



Alipozunguka nyuma ya maduka alitokea kulikokuwa na nyumba moja kubwa kabisa. Nyumba yenyewe ilikuwa na milango mingi. Miongoni mwa milango hiyo mmoja ulikuwa mkubwa sana. Kwanza hakufaham kwa nini mwenyewe alipata gharama kubwa juu ya milango mingi kama ile. Kisha aliona kuwa gharama yake ilikuwa na maana kwa mtu mwenye akili. Si nyumbani tu lakini hata katika jambo lolote hadhari hukataza mtu kujitia ndani yake kama halina milango ya kuingilia na kutokea. Milango ya nyumba ile ilitosha kwa salama. Baada ya kuwaza hivyo alipita kwa mlango mkubwa uliokuwa wazi akaona mabawabu na askari waliokuwa na sura za kuogofya. Lakini walikuwa mawe.



Ndani kulikuwa na uwanja mkubwa uliozungukwa na viti pande zote. Aliendelea mbele kidogo akatokea katika halmashauri kuu. Juu ya nusu ya halmashauri hiyo palijengwa ulingo. Ulingo wenyewe ulikuwa umejengwa kwa ustadi mwingi. Juu yake palizunguka watu aliodhania kuwa mawaziri, makadhi, mashehe, wanajimu, washauri na madiwani wengine. Kati yao palikuwa na kiti cha dhahabu kilichotonewa kwa majohari mbalimbali. Juu ya kiti hicho alikaa mfalme aliyevaa lebasi za fua zilizokuwa hazitamaniki kwa kumetameta. Kichwani mwake alivaa taji. Taji hilo lilipangiliwa kwa majohari ali ali. Kwa mng'ao mkubwa wa majohari mfalme mwenyeww alikuwa hatazamiki. Alipopanda juu ya ulingo kutazama aliona kuwa hadhara yote ilikuwa mawe matupu.



Alishuka chini akaingia katika halmashauri nyingine. Hiyo kadhalika ilikuwa sawasawa na ile ya mfalme ila ilikuwa na madiwani wanawake watupu. Baadhi ya madiwani walikuwa wamesimama mbele ya malkia na mikono yao vifuani, na wengine walikuwa wamepiga magoti chini yake kwa unyenyekevu. Walakini halmashauri hiyo ilikuwa na mapambo bora kuliko ile ya kwanza. Ilikuwa na meza ya pembe na viti vya mpingo. Juu ya meza palikuwa na bilauli za johari memetevu. Halmashauri nzima ilikuwa imejaa wanawake waliokuwa na uzuri wa sifa kubwa sana. Malkia mwenyewe alikuwa amekaa kitako kati yao. Mabibi wote walikuwa mawe matupu. Utulivu wa akili ya Adili ulichafuka. Alitupa chini majohari yote yaliyokuwa katika miliki yake. Moyo wake ulisimama juu ya bilauli zilizokuwa mezani. Alichukua zilizotosha kuwa mzigo wake akaondoka pale kabla moyo haujarogwa na uzuri wa mabibi waliogeuka mawe.



Mrithi wa Mji wa Mawe



Baada ya kwenda mbele hatua chache Adili aliona mlango mdogo. Kizingitini pake palikuwa na ngazi iliyoongoza juu. Alipopanda vidato vichache aliona dalili za mtu au watu walioishi mle. Kwanza alikuwa akipanda kwa kusitasita, lakini sasa dalili zile zilimvuta akafululiza kupanda. Aliendelea mpaka orofani. Alifuata zilikoongoza dalili mpaka akafika kulikokuwa na chumba kidogo. Mlango wake ulikuwa wazi, kwa hivi aliingia ndani. Huko aliona pazia la hariri lililotariziwa kwa vito vya dhahabu, lulu na yakuti linaning'inia mbele yake. Fusuai hizo zilimeremeta kama nyota. Dalili alizoona ziliendelea nyuma ya pazia hilo. Alijipa moyo mkuu akafunua pazia. Alipofanya hivyo macho yake yaliona mlango wa tarabe.



Mlango huo ulikuwa mzuri sana. Mbao zake zilikuwa za mpingo, nazo zilinakshiwa kwa johari na pembe. Mtu yoyote angaliona mlango huo angalistaajabu sana. Adili alibisha hodi akaingia katika chumba kikubwa. Chumba chenyewe kilikuwa kimepambwa vizuri sana. Katikati yake palikuwa na meza na kiti. Msichana wa fahari alikuwa amekaa kitako pale juu ya kiti. Usonwake ulikuwa umetukuka. Kwa uzuro uliokuwa haumithiliki. Bila shaka yeye alikuwa malkia wa wazuri katika dunia nzima. Libasi alizovaa zilikuwa nzuri na za thamani kubwa sana. Katika miji yote mingine aliyopata kufika katika safari zake, Adili alikuwa bado kukutana na mtu yeyote mwingine aliyevaa libasi nzuri kama zile.



Kama uzuri ulio peponi wamejaaliwa malaika; karibu uzuri wote ulio duniani alijaaliwa msichana huyo. Uzuri wake ulikuwa haulingani kwa uzuri na mwanamke mwingine yeyote aliyesifiwa kuwa mzuri katika zamani zake. Msichana mwenyeww alikuwa anasoma kitabu kitakatifu. Matamko yake yalikuwa kama mafuatano ya muziki. Moyo wa Adili ulitekwa na mapenzi ya tamasha hiyo. Akili yake ilipotea na nuru ya macho yake ilizimika kitambo. Ile ilikuwa mara ya kwanza mshale wa mapenzi kupenya moyoni mwake. Ulipenya katikati ya moyo wake. Haukuacha nafasi ya mapenzi ya mwanamke mwingine. Licha ya Adili hata mtu mwingine aliyekuwa hajui mapenzi angalikutana na mwanamke huyo moyo wake ungalitekwa pia.



Akili ya Adili iliporudi alimwamkia mwenyeji wake. Mwenyeji aliyeamkiwa hakuitikia tu, lakini alitaja jina la aliyemwamkia vile vile akamkaribisha kwa furaha. Adili alimwuliza alilijuaje kina lake, yeye alikuwa nani na miujiza gani iliyopita pale hata viumbe wa mji mzima wakageuka mawe. Bila ya kusema neno msichana aliondoka akaenda kuchukua kiti. Alikiweka karibu yake akamwomba Adili kukaa kitako. Mwendo aliotumia katika kwenda na kurudi wakati wa kuchukua kiti ulichukua pumzi zoye za Adili. Alikwenda kwa hatua za kupendeza , na mikono yake ilipunga kama upepo. Uzuri wake wa fahari ulikuwa na madaha makubwa. Chumba chake kilikuwa kama mahali pa faraja panapotafutwa na wanadamu.





Miguu ya msichana


Na mwendo aliokwenda,


Adili alipoona


Moyowe ulimshinda.



Alikuwa na miguu


Mfano wa charahani,


Wala ulimwengu huu


Hajatokea kifani.



Alipendeza hatua


Wakati alipokwenda,


Chini viatu vyalia


Mithali kama kinanda.


Alikwenda kwa madaha



Mwanamke mwenye enzi,


Yaliyompa furaha


Kila mwenye kubarizi.



Mji Ulivyogeuka Mawe



Sasa msichana alieleza kwamba yeye alikuwa binti mfalme, na jina lake lilikuwa Mwelekevu. Baba yake, Mfalme Tukufu alikuwa yule aliyeonekana kitini katika halmashauri ya madiwani wanaume. Mama yake, malkia Enzi, alikuwa yule aliyeonekana katika halmashauri iliyohudhuriwa na madiwani wanawake. Ufalme wao ulikuwa na utukufu na nguvu nyingi. Labda dola yao ilikuwa ya kwanza duniani iliyokuwa na miji laki moja. Isipokuwa, Fahari, mji uliogeuka mawe, miji mingine ilizama baharini. Raia chini ya bendera yao walikuwa lukuki. Mawaziri walikuwa laki tano. Kila waziri alikuwa na umati wa watu. Amirijeshi mmoja alikuwa na majemedari elfu moja na sufufu ya majeshi. Hazina za nchi zilikuwa na mali zisizohesabika kama machimbo ya Tanganyika.

ITAENDELEA

No comments:

Featured Post

 SOMA SIMULIZI ZENYE KUSISIMUA HAPA A. UTAJIRI WENYE UCHUNGU     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-1     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-2      UTAJIRI WENYE UCH...