Saturday, October 30, 2021

ADILI NA NDUGUZE - sehemu ya 5

 

ADILI NA NDUGUZE - 5

  


Simulizi : Adili Na Nduguze 

Sehemu Ya Tano (5)



Adili alipelekwa katika hazina ya majini iliyokusanya utajiri wote wa ulimwengu. Johari ndogo katika hazina hiyo ilikuwa na uzito usiochukulika kwa Adili. Alipochaguzwa kuchukua alichopenda hakuweza kuchagua kitu chochote.


Malkia alisikitika akasema, "Haidhuru!" Alishika simu akauliza" Naweza kusema na mfalme wa majini?"


Jibu lilikuja , " Naam, Kisasi huyu! Nani mwenzangu?" " Mjeledi , Malkia wa majini ndiye asemaye. Adili amechaguzwa apendacho katika hazina yetu, lakini ameshindwa kuchukua hata kitu cha uzito wa sindano moja. Wanadamu hawajaweza kutumia uwezo waliopewa kama Majini. Nataka msaada wako."


" Vema. Mlete hapa," kengele iliishilia.



Adili alikwenda katika halmashauri ya Majini. Alipofika mfalme alikuwa amekaa kitini kwa juu kuelekea hadhara kubwa ya mawaziri. Joho la mfalme lilikuwa la rangi ya fua, na kichwani alivaa taji la zari. Mawaziri walivaa majoho meusi, na vichwa vyao vilikuwa wazi. Hadhara nzima ilisimama Adili alipotokeza . Ilipokaa kitako tena alipewa kitabu cha hawala ya hazina ya majini. Kwa kila hawala iliyoandikwa na kutiwa sahihi ilipochomwa Adili aliweza kupata alichotaka katika hazina ya majini. Alifurahi kwa zawadi ile. Ilikuwa nyepesi kuwekeka, rahisi kutumika, nayo si nzito kuchukulika. Alimshukuru mfalme wa majini akarudi kwa Huria.



Adili aliyageukia Manyani akauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea . Manyani yaliziba nyuso zao kwa viganja vya mikono yao kwa aibu.



Nduguze kuwa Manyani



Baada ya Adili kutoswa, nahodha alishtuka akauliza nini kilichotumbukia baharini kwa kishindo kikubwa. Kusikia vile ndugu zake walianza kujiliza uongo kuwa ndugu yao amepotea. Nahodha alikwenda kutazama akaona Adili hayuko. Aliamuru kutua tanga na kuteremsha mashua. Lakini sasa dhoruba kali ilianza, na chombi kilichokuwa katika mrama mkubwa, kwa mawimbi makubwa ya upepo na umande, kilipakia maji, omo na tezi, na kulia ja kushoto. Giza kuu lilinyemelea roho za mabaharia. Palikuwa hapatiliki nanga. Kwa hivi tamaa ya kumuokoa Adili ilikatika.



Nahodha alipotaka kujua Adili alivyopotea, ndugu zake walimwambia kuwa ndugu yao aliamka akaenda msalani. Ghafula walisikia anguko kubwa majini. Watu wote jahazini walisikitika kupotelewa na Adili. Ndugu zake walilizana kitambo wakanyamaza. Kilio cha kujisingizia hakina machozi wala matanga.



Hasidi na Mwivu walichukua sanduku la Adili wakalifungua. Walitoa majohari yote wakagawana mafungu mawili usiku ule ule. Sasa ugomvi kati yao ulianza juu ya yule msichana mzuri aliyekuwa chomboni. Hasidi alitaka kumwoa, na Mwivu kadhalika alitaka kumwoa. Asiyefurahia heri ya mwenziwe, shari yake kumghadhibikia. Walimsahau ndugu yao aliyepotea dakika chache zilizopita kama aliyekufa miaka kumi iliyopita. Walikuwa na mioyo migumu iliyoje!



Mwelekevu, yule msichana mzuri, alikuwa hana tabasamu. Uzuri wake ulisawazika kwa machozi ya njia mbili usoni. Huzuni ilimshika vibaya, lakini alikuwa imara kutetea heshima yake. Aliwaambia wale ndugu wawili wasigombane bure. Hakuwa tayari kuolewa na yeyote kati yao. Na kabla ya sauti ya maneno aliyosema haijaishilia masikioni mwao, alijitosa baharini akatoweka vile vile.



Hasidi na Mwivu hawakujua la kutenda. Atakaye makaa ya mgomba hapati kitu ila jivu tupu. Ndugu hawa wawili walimtosa ndugu yao kwa tamaa ya kupata msichana , lakini walipata aibu tupu. Walikaa kitako wamefedheheka, walipokuwa katika hali hiyo na jahazi inakwenda mbio, Huria na Adili walitua ghafula kama ndege chomboni.



Marejeo ya Adili yalishangaza watu chomboni. Macho ya ndugu zake yalisutana. Kwa kutahamaki walimkumbatia wakajifanya kumfariji. Walisema hatari yake ilitisha, na msiba wao ulikuwa mkubwa. Watu wengine wote chomboni waligeuza macho yap kando waliposikia uongo wa ndugu zake. Walakini Adili aliwashukuru akisema bahari haiweki amana ya kitu kieleacho, kwa kuwa alielea aliokoka.



Kwa hasira kubwa Huria alinena, "kama mngalijua hatari ya kumtosa mtu baharini, au mngalikuwa na fikira za msiba, msingalijaribu kumtumbukiza ndugu yenu baharini alipolala. Wauaji ninyi hamstahili kuishi," aliwashika shingoni pamoja na mkono wa kushoto akawabana kwa nguvu ya ajabu. Mkono wake wa kulia uliinua ngumi juu tayari kuwaangukia kwa uzito mwingi. Ndimi vinywani na mboni machoni mwao zilitoka kwa hofu wakataka kuombewa.



Damu nzito kuliko maji. Hasidi na Mwivu walikuwa damu kwa Adili . Hakuvumilia kuona hilaki yao akamwomba Huria kuwasamehe. Walimtosa tu, hawakumwua. Huria alibisha kuwa walistahili kifo. Jaribu la jinai lilitosha kuhalalisha adhabu ha kifo ujinini. Adili alitaradhia kuwa jaribu la jinai halikutosha kuhalalisha kifo duniani. Kama walikufa kwa sababu yake angalikuwa mnyama wa mwitu mbele ya macho ya watu. Huria aliposikia maneno hayo alinena sheria ya wanadamu ilitatiza. Kwa sababu hiyo walikuwa hatarini milele. Walakini alikubali kuwasamehe kwa sharti ya kuwageuza wanyama. Aliwalaani watoke katika umbo la uanadamu. Mara ile ndugu zake walikuwa manyani.



Kisha Huria aliwakabili watu waliokuwa chomboni akasema. Adili alikuwa rafiki yake mkubwa. Alimjali na kumheshimu juu ya marafiki zake wote. Alipata upendo wake kwa sababu alikuwa salihi na mstahiki wa kuajabiwa na dunia nzima. Ataonana naye mara kwa mara. Mtu yeyote akifitini ataona nguvu ya mkono na uwezo wa ulimi wake. Atampatiliza kama alivyofanya kwa waovu wale wawili. Wajihadhari wapatw kujiokoa kwa sababu alikusdia kutimiza alivyosema. Aliwaonya pia watakapofika kwao wasisemw habari ile. Mtu yeyote atakayejaribu kunong'ona habari ile atakoma kusema milele.



Aliagana na Adili akasema, "Funga manyani haya kwa kamba . Ukifika Jannibu utayafunga kwa minyororo viunoni mbalimbali. Utayatia chumbani na kila moja lifungwe peke yake. Kila usiku wa manane utachukua kiboko ukafungue kila nyani ulipige mpaka lizimie. Utayapa posho na kuyaadhibu hivi daima. Kama amri hii haikutiiwa utaadhibiwa wewe." Alipokuwa akitoa amri hii alijibadilisha sura za ajabu kila dakika moja. Watu wote jahazini walishikwa na mshangao mkubwa kwa mabadiliko yake ya mfululizo, wakatosheka kuwa aliweza kubadili kitu chochote katika umbo alilotaka.



Adili aliyageukia manyani akauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea. Manyani yaliziba nyuso kwa viganja vya mikono yao kwa aibu.





Adhabu ya Kwanza.


Baada ya kutoweka kwa Huria. Adili alikwenda ngamani kumtazama Mwerekevu. Hakiona mtu. Alipouliza aliambiwa alijitosa baharini ndugu zake walipomkalifu kumuoa. Adili hakuweza kujizuia, akaanguka chini kwa huzuni. Moyo wake ulifumwa kwa msiba akalia kama mtoto mdogo.


Uzuri aliotetea kwa thamani ya maisha yake ulipotea. Aliona wokovu wake haukumfaidia. Bahati ilikuwa mbaya na katili sana kwake. Alifikiri kwamba yeye peke yake ndiye aliyepatwa na ajali mbaya kama ile tangu kuumbwa kwa dunia. Adili aliwaza hivyo, haijulikani mtu mwingine angewazaje.


Kulipokucha chombo chao kilitia nanga Janibu. Matajiri walipanda chomboni wakaamkiana na Adili. Walizungumza mambo mengi, lakini hapakuwa na mtu hata mmoja aliyeuliza habari za ndugu zake. Hili lilimshangaza akamaizi kuwa walio aili walikuwa hawana nafasi katika kumbukumbu za dunia.


Alishuka pamoja na manyani yake akaenda zake nyumbani kwake. Baada ya kuyaweka chumbani alijishughulisha na kupakuwa mali yake. Hakuwahi kutafuta minyororo ya manyani siku ile, na usiku alisahau kuyapiga akalala. Saa saba usiku Huria alitokea na hasira imemjaa tele. Alisema kuwa alikuwa jini. Neno la jini halirudi. Kwa kukosa kutii amri yake adhabu ya kwanza ilimpasa Adili.


Kabla Adili hajajibu neno, mikono yake miwili ilikuwa katika mkono wa kushoto wa Huria. Hakuweza kuponyoka. Kwa mkono wa kulia Huria alimpiga Adili kibao mpaka akazimia. Ndipo alipokwenda yalipokuwa manyani akiyapiga kiboko vile vile mpaka yakakaribia kufa.


Alimrudia Adili aliyekuwa anaanza kupata fahamu akasema, “Twaa kiboko hiki, utayapiga manyani haya kesho usiku kama nilivyofanya. Siku moja ikipita bila kuyapiga, kiboko hiki kitaishia mwilini mwako.” Macheche ya moto yaliyoka kinywani mwake alipokuwa akiamuru hili, na mara neno la mwisho lilipotamkwa alitoweka.


Siku iliyofuata Adili alikwenda kwa sonara akatengeneza minyororo miwili ya dhahabu. Aliileta nyumbani mwaka akaifunga viunoni mwa manyani yake. Usiku alipokwenda kuyapiga na kuyaposha machozi yalimlengalenga machoni.


Katika ini alifumwa na mshale, na moyoni mwake michomo ya maumivu makali. Hakupendelea kuadhibu wanyama waliokuwa kwanza ndugu zake. Huruma yake ilikuwa lakini ilikalifiwa na amri.


Huria alijua huruma ya Adili na kuwa alimkalifu sana. Lakini ndugu zake walikuwa waovu, katili, hiani na wauwaji wa kutisha. Walikosa fikra wakawa duni Kama wanyama wa porini. Adhabu kali kwa waovu ilikuwa ndiyo ulinzi peke yake ya wema. Jini ililiona hivyo, haijulikani mtu angalionaje.


Siku nyingi zilipita, Adili alidhani labda adhabu ya Huria ilikwisha. Siku moja hakuyapiga manyani yake. Loh salale! Dhahama gani? Alijuta kuzaliwa akatamani ardhi ipasuke ajitie ndani yake. Alipigwa kiboko siku hiyo kuliko siku ya kwanza. Mwili wote ulienea makato ya kiboko akavuja damu mpaka akazirai.


Aliteremsha mavazi aliyovaa mpaka kiunoni akaonesha makovu ya mapigo ya Huria. Wepesi wa maumbile wa kuondoa alama haukuweza kufuta makovu ya Adili. Yalijionyesha wazi wazi mwilini mwake.


Toka siku ile na baadaye, hakusahau maumivu ya mapigo yale. Kwa muda wa miaka kumi hapakupita tena hata siku moja aliyoacha kuyapiga manyani yake. Kwa huruma yake kila baada ya kuyapiga aliyanasihi akilia:-


“Nala sumu ndugu zangu

msambe naona tamu,

Takalifu kubwa kwangu,

Kuadhibu yangu damu,

Sina raha ndugu zangu,

Neno hili kwangu gumu.”


Mwisho wa ushahidi, Adili aliyageukia manyani akauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea.

Manyani yalijiziba nyuso kwa viganja vya mikono yao kwa aibu.




HARUSI


Adili alipolala mtingisho mkubwa ulitokea chumbani mwake sakafu ikapasuka. Kuzinduka uso wake ulikutana na uso wa Huria. Wa kwanza ulijaa matumaini, wa pili ulituna kwa hasira. Nyuso zao zilisomana. Kila uso ulijaribu kuzua mzungu wake.


Adili alivunja amri aliyopewa mara tatu. Alionekana alizoea kuhalifu. Kukomeshwa mazoea yake alipasa kugeuzwa nyani kama ndugu zake. Walakini, kabla ya hili kuwa Huria alitaka kusikia kama Adili alikuwa na udhuru wa kujitetea.


Adili hakusema, lakini tabasamu ya mvuto mwingi ilikuwa ikicheza usoni mwake. Alichukua barua ya Rai akampa Huria. Huria aliposoma barua hakuweza kufanya alilokusudia. Alitoweka akaenda ujinini kumshauri baba yake.


Barua ya Rai ilipowekwa mbele ya Kisasi, kuopolewa kwa ndugu zake Adili kuliridhiwa. Huria alimwuliza Mfalme wa majini labda haja ya Mfalme wa wanadamu isingakubaliwa ingalikuwaje. Baba alieleza.


Mfalme wa wanadamu aliweza kufanya dhara aliyotaka kwa majini. Alikuwa mwanadamu. Mwanadamu alikuwa bora kuliko jini. Majini katika Jua, Mwezi, Mushtara, Zebaki, Zuhura, Mirihi, Sumbla, Zohali, Sarateni, Kausi na Utaridi hayakuweza kushindana na watu katika ardhi.


Majini yaliweza kugeuza watu watu katika umbo lolote, lakini watu waliweza kufunga majini yote katika chupa moja. Magereza yao yalikuwa mabaya sana. Kama mtu asingalikuwa mzembe mwenyewe, busara ya jini ingalikuwa busara yake. Alipasa kuheshimiwa kama alitaradhia heshima yake.


Mara ile Huria alirudi kwa Adili akatangaza kuwa haja ya Rai ilifaulu. Mfalme wa majini alikubali ndugu zake kuwa watu tena.


Aliyabadili manyani akasema, “Tokeni katika uhayawani mrudi katika utu.” Walikuwa watu tena, wakajiangusha miguuni mwa ndugu yao kuomba radhi. Adili alimshukuru Huria, na punde wakaagana.


Asubuhi watumishi walimwona bwana wao na watu wawili. Waliwatambua kuwa walikuwa ndugu zake. Walipouliza kuwa walikuwa wapi kwa muda mrefu, bwana alijibu kuwa walikuwa manyani yaliyoonekana jana yakila naye. Walifurahi kumuona bwana wao si mkichaa, wakamwombea azidishiwe furaha katika maisha yake.


Baada ya kustaftahi aliwavika ndugu zake nguo ali ali, akapanda nao farasi kwenda Ughaibuni. Liwali Adili alipofika Ughaibu na habari kuwa manyani yake yalikuwa watu tena palikuwa na furaha kubwa sana. Jitihadi na kufaulu kwa Rai kuliandikwa katika kumbukumbu za dunia. Hasidi na Mvivu walipoletwa barazani kila mtu aliajabia sura zao. Walikuwa wazuri ajabu.


Mfalme wa Ughaibu alimsifu Adili kuwa alikuwa sababu kubwa ya wokovu kwa ndugu zake katika dhima ya wanyama.


Mateso yaliyompata yalishinda uvumilivu wa mtu. Alivumilia mateso mengi kwa ajili yao. Alikuwa mwanamume barabara na fahari ya Ughaibu. Nchi yake ilimsifu hivi, haijulikani nchi yangu au yako ingalimsifiaje mtu wa namna ile.


Alipogeuka kwa ndugu zake Adili, Rai alionya kama wavivu wajitahidi kuwa hodari, ilikuwa kinyume hodari kuwa mvivu. Kama waovu walitaka kuwa wema, ilichukiza wema kuwa waovu. Kama masikini walitafuta utajiri, ilikuwa ujinga matajiri kufuja walichokuwa nacho. Kama mbegu kidogo iliongezwa mchanga, ilikuwa uharabu mtu kuua ndugu yake. Pia ilikuwa aibu kubwa sana kwa wazuri kutenda maovu.


Wakamilifu walikuwa na nafasi kubwa duniani kuliko wapungufu. Maonyo ya Mfalme yalikuwa mwanana, lakini yalishinda mioyo ya watu waliokusudiwa kuonywa.


Walimshukuru wakaahidi kuwa walikoma kutenda dhara kwa ndugu yao, na kwa kitu chochote kilichokuwa na maisha. Ahadi hii haikuvunjwa.


Mawe huwa dhahabu,

au johari na chuma.

Na mtu anapotubu,

dhambi yake kukoma.

Nidhani zake thawabu,

na heshima ya daima.


Adili alipanda farasi akarudi Janibu na ndugu zake. Njiani alikutana na mabibi watatu waliopanda farasi vile vile.


Mabibi wenyewe walikuwa wazuri na watanashati sana. Wa kwanza alikuwa Mwelekevu aliyeokolewa na Mrefu. Macho ya Adili na ya Mwelekevu yalipokutana mioyo ya giza ilijaa nuru tena. Wote wawili walishuka chini wakaamkiana.


Aha, ilikuwa furaha kubwa iliyoje! Mioyo miwili ya mapenzi iliyopoteana ilikutana tena. Neno halikuwezekana kusemeka. Walitazamana wakachekana. Walishikana mikono wakabusiana. Walikuwa katika siku bora ya maisha yao.


Adili alipomwambia Mwelekevu kuwa wavulana wawili watanashati aliokuwa nao walikuwa ndugu zake, Mwelekevu kadhalika alisema kuwa wasichana wawili warembo aliofuatana nao walikuwa marafiki zake.


Watu wote wanne walishuka chini wakaamkiana vile vile. Kisha wote walipanda farasi wao wakashika njia kuelekea Janibu.


Walipofika palifanywa harusi tatu siku moja. Siku hiyo ilikuwa kubwa kuliko yoyote iliyopita Janibu.


TAMATI


No comments:

Featured Post

 SOMA SIMULIZI ZENYE KUSISIMUA HAPA A. UTAJIRI WENYE UCHUNGU     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-1     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-2      UTAJIRI WENYE UCH...