UTAJIRI WENYE UCHUNGU - 1


 IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI 

*********************************************************************************

Simulizi : Utajiri Wenye Uchungu 

Sehemu Ya Kwanza (1)



“All people who live at the beach have to leave immediately because tsunami will come. Once you hear this announcement, tell your colleague,” (Watu wote mnaoishi katika ufukwe mnatakiwa muondoke haraka iwezekanavyo kwa sababu tsunami itakuja. Unaposikia tangazo hili mtaarifu na mwenzako,)” ilisikika sauti ya mwanamke aliyekuwa akitangaza katika Kituo cha Redio cha Orange Fm nchini Marekani.

Watu wote waliokuwa wakiishi katika fukwe mbalimbali katika Jiji la New Orleans nchini Marekani walitakiwa kuondoka haraka iwezekanavyo kwani tayari mamlaka ya hali ya hewa ya nchini humo (National Weather Service) ilitangaza hali ya hatari ambayo ingelipata jiji hilo pamoja na majiji mengine yaliyokuwa katika fukwe mbalimbali ikiwemo Miami.

Hakukuwa na mtu aliyepuuzia taarifa hiyo, wengi wakaanza kuondoka kwa ajili ya kuyaokoa maisha yao kwani bado kumbukumbu juu ya kimbunga cha Katrina ambacho kilipiga miezi michache iliyopita bado ziliendelea kubaki vichwani mwao.

Mitaani kulikuwa na purukushani, kila mtu alitaka kuyaokoa maisha yake. Kumbukumbu juu ya tsunami zilikuwa vichwani mwao, walisoma kwenye historia miaka ya nyuma kwamba balaa hilo liliwahi kuikumba China na Japan na matokeo yake watu wengi walifariki dunia.

Serikali ya Marekani ikaagiza magari makubwa na kuwataka watu wote waondoke katika sehemu za ufukwe na kukimbia umbali wa kilometa ishirini kutoka ufukweni kwani pasipo kufanya hivyo ilikuwa ni lazima tsunami iwakumbe na kufariki dunia.

Watu waliondoka, helkopta zilipita kila kona ndani ya jiji hilo, mtu mmoja aliyekuwa akitangaza kwenye kipaza sauti alisikika akiwaambia watu kwamba huo ulikuwa ni muda wa kuondoka, kulikimbia jiji hilo kutokana na maafa ambayo yalitarajiwa kulikumba jiji hilo, tena saa mbili zijazo.

“Where is Catherine?” (Catherine yupo wapi?) alisikika mwanamke mmoja akiuliza.

“I don’t know . She told me that she would go to James, maybe she went there (Sifahamu. Aliniambia kwamba angekwenda kwa James, labda alikwenda huko) alijibu mwanaume mmoja.

Hakutaka kujali sana, kwa kuwa aliambiwa kwamba msichana huyo alikwenda kwa mwanaume aitwaye James, hakutaka kuuliza zaidi ya kuendelea na safari yao ya kuyaokoa maisha yao kwani lilikuwa limebaki saa moja kabla ya janga hilo kulikumba Jiji la New Orleans na miji yote ambayo ilikuwa karibu na bahari.

Mamlaka ya hali ya hewa nchini Marekani haikukaa kimya, bado iliendelea kutoa onyo kwamba watu wote waliokuwa wakiishi pembezoni mwa bahari ya Atlantic walitakiwa kuondoka kwani tsunami liliendelea kuja kwa kasi kwa kipimo cha 4.11 ambacho kilikuwa ni kikubwa mno huku mawimbi yake yakiwa na urefu wa mita mia moja kwenda juu ambayo yalikuwa yakienda kwa kasi ya kilometa 2 kwa dakika tano.

Huko lilipoanzia nchini China, Thailand na nchi nyingine barani Asia, liliacha vilio, zaidi ya watu milioni mbili walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya huku makazi ya watu wengi yakiharibiwa mno.

Maafa yaliyotokea nchini China kipindi hicho waliyaona kwenye televisheni, waliogopa na kuhisi kwamba inawezekana tsunami hilo lingefika mpaka nchini Marekani kwani hata wao kulikuwa na miji ambayo ilikuwa pembezoni mwa bahari, kweli ikawa hivyo.

“Mnatakiwa kuchukua vitu vilivyokuwa muhimu kwenu, ambavyo havina umuhimu viacheni na serikali itawasaidia kwa kila kitu,” bado tangazo lilikuwa likitolewa kutoka kwa mtu aliyekuwa kwenye helkopta ambaye alitumia kipaza sauti kilichosikika vizuri kabisa na kila mtu.

Muda ulizidi kwenda mbele, dakika arobaini na tano baadaye, ukimya mkubwa ulitawala kila kona ndani ya jiji hilo, hakukuwa na sauti yoyote iliyosikika, si binadamu tu bali hata wanyama hawakuwepo, watu walikimbia na kwenda katika Mji wa Gonzales uliokuwa kilometa ishirini kutoka hapo New Orleans.

“Jamani naomba mnisaidie, namtafuta binti yangu...” alisema mwanamke mmoja, kwa kumwangalia tu alionekana kuwa na hofu moyoni mwake, alikuwa akimwambia mmoja wa wanajeshi ambao waliwachukua watu kutoka New Orleans.

“Anaitwa nani?”

“Catherine, mara ya mwisho kabla tangazo halijatolewa, alikwenda kwa mpenzi wake, sijui kama yupo naye kwa sababu hata wazazi wa mpenzi wake tulionana nao wakasema kwamba hata kijana wao hayupo nao,” alisema mwanamke huyo.

Hiyo ilikuwa kazi nyingine kabisa, alichokifanya mwanajeshi huyo ni kuonana na wazazi wa huyo kijana ambaye alikuwa mpenzi wa Catherine aitwaye James na kuanza kuzungumza nao.

Kama alivyoambiwa na mama yake Catherine ndivyo alivyoambiwa hata na wazazi hao kwamba kijana wao aitwaye James hakuwa akionekana. Hiyo ikawatia hofu kwa kuhisi kwamba japokuwa mahali hapo waliona kwamba kila mtu alikuwa hapo kumbe kuna wawili ambao hawakuwa hapo.

Walichokifanya ni kuanza kuyaita majina yao kila kona kwa kupitia kipaza sauti. Kila aliyesikia, akabaki akimwangalia mwenzake kwa kuhisi labda huyo ndiye aliyekuwa akihitajika.

Zaidi ya watu milioni nne waliokuwa wamekimbia katika jiji hilo, ni watu wawili tu ndiyo ambao hawakuwa wakionekana, kwani familia zote zilikuwepo na kila moja walitimia isipokuwa familia mbili ambazo watu wawili hawakuonekana.

Tayari kukaonekana kuwa na tatizo sehemu, mwanajeshi yule akawapa taarifa wenzake kwamba watu wawili hawakuwa wakionekana mahali hapo hivyo walitakiwa kwenda kuwatafuta katika jiji hilo, hata kama kuwaita walitakiwa kufanya hivyo ilimradi wawapate na kuwaleta pale walipokuwa.

“Zimebaki dakika ngapi kabla ya Tsunami kuipiga New Orleans?” aliuliza mwanajeshi mmoja.

“Dakika ishirini!”

“Chukueni helkopta haraka muende kuwatafuta...”

Hicho ndicho kilichofanyika, hakukuwa na muda wa kupoteza mahali hapo, kwa haraka sana wanajeshi sita wakaingia katika helkopta moja kubwa na kuanza kurudi ndani ya jiji hilo kwa ajili ya kuwatafuta watu wawili tu, msichana mjauzito aliyeitwa Catherine na mwanaume aliyeitwa James.

Walipofika katika jiji hilo, wakachukua darubini na kuanza kuangalia, kila kona, hakukuwa na mtu yeyote, hakukuwa na mnyama, ni nyumba na magari machache ndivyo vilivyokuwa vimebaki.

Hawakukata tamaa, waliendelea kuwatafuta huku wakiita kwa sauti kubwa tena kwa kutumia kipaza sauti lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyeitikia au hata kutoka na kuwapungia mikono kuonyesha kwamba alitaka msaada.

Dakika ziliendelea kukatika, zilipofika dakika kumi na tisa tu, kwa mbali baharini likaanza kuonekana wimbi kubwa na zito likija kwa kasi. Waliliangalia wimbi lile, lilikuwa kubwa zaidi ya mita mia moja ambayo ilitangazwa na mamlaka ya hali ya hewa.

Lilikuwa likija kwa kasi mno na hata muungurumo wake ulikuwa mkubwa. Halikuwa likija peke yake bali lilikuwa likija na meli kadhaa kubwa zilizokuwa baharini ambazo nazo zilisombwa na tsunami hiyo.

“It is coming...it is coming...” (Linakuja...linakuja..) alisema mwanajeshi mmoja, rubani akageuza helkopta ile na kuanza kuondoka kwani kwa jinsi wimbi lile lilivyokuwa likija kwa kasi, tena huku likiwa kubwa namna ile, walijua kabisa wangeweza kupata tatizo, hivyo wakaondoka huku wakiahirisha kuwatafuta watu hao ambao ukweli wenyewe ni kwamba walikuwa hai, tena msichana Catherine akiwa kwenye uchungu mkubwa wa kujifungua mbele ya mpenzi wake, James.


Catherine alikuwa na tumbo kubwa, ujauzito huo tayari ulikuwa umetimiza miezi tisa na muda wowote kuanzia siku hiyo angeweza kujifungua. Kila alipokaa, alionekana kuwa na furaha mno, hakuamini kama siku chache au saa chache zijazo naye angeitwa mama.

Mwanaume aliyempa mimba alikuwa James Carthbert, mwanaume mwenye sura nzuri aliyekuwa na mchanganyiko wa rangi kwa maana ya baba kuwa mtu mweusi na mama Mzungu.

Siku hiyo Catherine hakutaka kukaa nyumbani kwao, alichokifanya ni kuondoka kuelekea nyumbani kwa kina James, alitaka kuonana na mwanaume huyo ili hata pale atakapoanza kujisikia uchungu basi apelekwe hospitali kwani mahali alipokuwa akiishi James kulikuwa karibu na Hospitali ya Cambodia Medical Center.

“I have come, I want you to take me to the hospital,” (Nimekuja, ninataka unipeleke hospitali) alisema Catherine huku akiteremka ndani ya gari.

“What time?” (Muda gani)

“Once I feel labor pains,” (Mara nitakapojisikia uchungu wa kuzaa) alisema Catherine.

“No hay problema mi ángel,” (hakuna tatizo malaika wangu) alisema James kwa Kihispania.

Akamchukua msichana wake na kuingia naye ndani. Wakaenda chumbani na kutulia kitandani. Walikuwa wakizungumza mambo mengi kuhusu maisha yao, walikwishajua kwamba mtoto ambaye angezaliwa alikuwa ni wa kiume hivyo walianza kupanga mipango yao namna ya kumlea na kumfanya kuwa miongoni mwa watoto waliokuwa na bahati duniani.

Waliyaandaa maisha yake angali yupo tumboni, wakajipanga vilivyo na kuhakikisha wanampa furaha ambayo hatoweza kuipata kutoka kwa mtu mwingine yeyote yule.

Walijifungia chumbani, hawakutaka kuingiliwa na mtu yeyote na kitu walichokisubiri wakati huo kilikuwa ni maumivu ya uchungu wa kuzaa kutoka kwa Catherine ambaye angekimbizwa katika Hospitali ya Cambodia ambayo wala haikuwa mbali kutoka hapo walipokuwa.

Baada ya kukaa kwa saa moja chumbani tena huku redio ikisikika, wakaanza kusikia tangazo kwamba watu wote walitakiwa kuondoka kwani tsunami ilikuwa njiani kulipiga Jiji la New Orleans.

Kwanza hawakuamini walichokisikia, Alichokifanya James ni kuifuata redio, akaongeza sauti kwa ajili ya kusikia vizuri kilichokuwa kikitangazwa, hakukuwa na mabadiliko, ni kweli mamlaka ya hali ya hewa ya nchini Marekani ilitangaza kuwepo kwa hali ya hatari dakika chache zijazo hivyo watu wote walitakiwa kuondoka.

“All people who live at the beach have to leave immediately because tsunami will come. Once you hear this announcement, tell your colleague,” (Watu wote mnaoishi katika ufukwe mnatakiwa muondoke haraka iwezekanavyo kwa sababu tsunami inakuja. Unaposikia tangazo hili mtaarifu na mwenzako,) ilisikika vizuri sauti ya mtangazaji huyo.

“We have to run,” (Inatupasa tukimbie) alisema James.

“I can’t James...” (Siwezi James..)

“Why?” (Kwa nini?)

“My time has come,” (Muda wangu umewadia) alisema Catherine huku akianza kujisikia uchungu kwani hata pale kitandani alipokuwa, alianza kujinyonganyonga.

Kitu cha kwanza kabisa alichokifanya James ni kuchungulia dirishani, akaona watu wakianza kuondoka tena kwa kukimbia huku wengine wakitumia magari yao, alitamani kuomba msaada kwani kwa hali aliyofikia mpenzi wake ilionyesha kwamba muda wowote ule angeweza kujifungua.

Catherine akaanza kupiga kelele za maumivu, James akachanganyikiwa, alishindwa kuwaita hata watu waliokuwa nani ya nyumba hiyo kwani kila mmoja alianza kukimbia kufuatia tangazo lililotolewa kwamba watu wote walitakiwa kuondoka.

Hakutaka kukubali kirahisi, hakutaka kujiona akishindwa, hakuamini taarifa hizo japokuwa tayari helkopta zilianza kupita na kuwatangazia watu kwamba walitakiwa kuondoka kutokana na tsunami ambayo ilikuwa njiani kulipiga jiji hilo.

Dakika kumi mbele, ukimya mkubwa ulitawala, alipochungulia tena dirishani hakumuona mtu yeyote yule hali iliyomfanya kumsogelea Catherine pale alipokuwa na kuanza kuongea naye.

“Nitapambana mpaka unajifungua salama,” alisema James huku akimwangalia msichana huyo machoni.

“Nisaidie, naumia, nisaidie James...” alisema Catherine, tayari kijasho chembamba kikaanza kumtoka.

Alichokifanya James ni kuipanua miguu yake, na kuiingiza mikono yake katika njia ya kutolela mtoto na kumwambia aanze kusukuma. Hicho ndicho alichokifanya Catherine, akaanza kusukuma kama alivyoambiwa.

Alijitahidi, alipiga kelele, alisukuma kadiri alivyoweza lakini bado mtoto hakutoka, aliendelea kuambiwa asukume zaidi. Hakuacha, japokuwa alikuwa akisikika maumivu makali lakini aliendelea zaidi na zaidi.

Baada ya dakika kadhaa, James akaanza kusikia mlio wa helkopta kwa mbali, si mlio wa chombo hicho tu bali akaanza kumsikia mtu mmoja akiongea kwenye kipaza sauti akimtaka yeye na mpenzi wake wajitokeze kwani tsunami ilikuwa ikija.

“Siwezi kuondoka na kumuacha mpenzi wangu hapa,” alisema James huku tayari mtoto alianza kutoa kichwa.

James hakuacha, aliendelea kumvuta mtoto huyo huku Catherine akipiga kelele za maumivu makali. Ghafla kwa mbali akaanza kusikika sauti kubwa ikija kule walipokuwa, alijua fika kwamba hiyo ndiyo ilikuwa tsunami ikija lakini hakukimbia, kama kufa, alikuwa radhi kufa na familia yake lakini si kuiacha.

“Tunakufa James...” alisema Catherine kwa sauti ya chini, tayari mtoto alitolewa, alionyeshewa, japokuwa alikuwa mdogo lakini alionekana kufanana sana na James.

“Hatuwezi kufa....nitakulinda, kama utakufa, basi tufe wote,” alisema James huku akikikata kitovu cha mtoto.

Kwa haraka akakimbilia kabatini, akachukua taulo lake na kumfunikia mtoto, akamuweka pembeni, akalifuata friji lake dogo la chumbani na kuliangusha chini, akatoa vitu vyote na kisha kumuingiza mtoto wake.

“Catherine mpenzi....”

“Nipo hapa mpenzi...” aliitikia Catherine kwa sauti ya chini kabisa, sauti iliyosikika kama mtu aliyechoka mno.

“Kama tutakufa, acha mtoto wetu awe hai...”

“Yupo wapi?”

“Nimemuweka kwenye friji, tsunami inakuja, nitataka yeye aelee na anusurike,” alisema James huku akimshika mkono mpenzi wake. Muda wote huo mtoto yule alikuwa akilia tu.

Wala hazikupita dakika nyingi, maji yakawafikia, nyumba ikasombwa na maji hayo. Catherine, tena huku akiwa kwenye maumivu makali na mchoko mkubwa akaanza kupiga kelele za kuomba msaada, alikuwa akimuita mpenzi wake lakini hakuwa karibu naye na wala hakumuona.

Yeye na nyumba, vyote vikasombwa na maji na kuanza kupelekwa sehemu nyingine kabisa, maji mengi yenye urefu wa kwenda juu zaidi ya mita mia moja yakamchukua.

Kwa upande wa James, alijitahidi kupiga mbizi, kushikilia vyuma vya meli zilizosombwa na maji kutoka baharini, kote huko ilikuwa ni mishemishe ya kuyaokoa maisha yake.

“Catherine...Catherineeee...” alianza kuita mara baada ya kugundua kwamba alikuwa peke yake.

Alichanganyikiwa, aliangalia kila kona kumtafuta mpenzi wake, hakuweza kumuona. Maji yale yalikuwa na nguvu mno, yalimpeleka huku na kule, alijigonga kwenye vyuma, magari yaliyokuwa yakielea kiasi kwamba yakamfanya kuwa hoi, baada ya muda fulani, mikono yake ikaishiwa nguvu, hakuweza kushikilia hata vyuma vilivyokuwa vikielea.

“Bora nife...” alijisemea huku mikono yake ikiwa imeishiwa nguvu, akaangalia huku na kule, kote kulijaa maji, hata maghorofa makubwa yenye floo zaidi ya mia moja nayo yote yalizamishwa na maji hayo.

Alijiona akiwa baharini, hakuwa na nguvu tena, alikosa msaada hivyo kitu alichokiona ilikuwa ni lazima akubaliane na ukweli hivyo azame. Akaulegeza mwili wake, akajiweka tayari kwa kufa.

“Pokea roho yangu Mungu! Mlinde na mtoto wangu kwenye friji pasipo kumsahau mpenzi wangu, Catherine ambaye sijui yupo wapi,” alisema James huku akiwa hoi. Sasa akawa tayari kwa kufa.


Alikubaliana na ukweli kwamba siku hiyo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya uhai wake, akakubali kufa kwani hakukuwa na chochote alichoweza kufanya zaidi ya kumruhusu Israeli achukue roho yake naye kuwa miongoni mwa watu waliokufa katika balaa la mafuriko la tsunami.

Wakati akiwa amekata tamaa kabisa, ghafla akaliona jengo moja refu, lenye floo zaidi ya mia moja na hamsini na lilijengwa katikati mwa Jiji la New Orleans, hilo lilikuwa ghorofa la vioo ambalo ndani yake kulikuwa na ofisi nyingi ikiwemo Studio ya Murder Inc ambayo ilikuwa ikivuma sana nchini Marekani kwa kurekodi nyimbo za wasanii wengi akiwemo Ashanti.

Akajikuta akipata nguvu mwilini mwake, hakutaka kuchelewa, huo ndiyo ulikuwa msaada wake wa mwisho, kama angeshindwa, basi alikuwa tayari kufa. Alichokifanya ni kuanza kupiga mbizi kulifuata ghorofa hilo.

Ilikuwa kazi kubwa lakini hakutaka kukata tamaa, aliendelea zaidi, alichoka lakini akajilazimisha kwani aliamini kwamba kama angefanikiwa kulifikia jengo lile basi angekuwa salama,asingekufa kama alivyotegemea.

Jengo lile lilikuwa mbali kama wa hatua mia moja kutoka pale alipokuwa, tena likiwa linaonekana kidogo sana, akakazana kupiga mbizi mpaka alipoanza kulifikia, akaongeza kasi kidogo, akalifikia na kudandia juu.

Akakaa kileleni, aliishiwa nguvu na hivyo kulala kwanza. Baada ya dakika kadhaa akapata nguvu na kuangalia kule alipotoka, maji yalijaa kila sehemu, ilikuwa ni vigumu sana kugundua kwamba sehemu hiyo iliyokuwa imejaa maji kulikuwa na mji, ilionekana kuwa moja ya bahari kubwa.

Hakutaka kuondoka katika jengo hilo, aliendelea kutulia huko juu huku macho yake yakiangalia huku na kule. Hilo ndilo lilikuwa jengo kubwa kuliko majengo yote kwa maana hiyo kwa kipindi hicho yeye ndiye alikuwa kileleni kuliko mtu yeyote katika jengo hilo.

Hapo ndipo kumbukumbu juu ya Catherine zilipomjia, moyo wake ulimuuma mno, alikuwa na lengo la kumsaidia mpenzi wake huyo lakini kitu cha ajabu, baada ya tsunami kupiga, hakuweza kubaki naye, akajikuta akitenganishwa yeye na mpenzi wake.

Mawazo yake hayakuishia kwa mpenzi wake tu bali hata kwa mtoto wake wa kiume aliyefikiria kumpa jina la Leonard. Alimkumbuka, alimuona mara moja tu, baada ya hapo akamuingiza ndani ya friji, kilichoendelea hakukijua, hakujua kama kweli alinusurika katika friji lile au la.

Siku hiyo ilikuwa ya mateso tele, alishinda katika jengo hilo, baridi lilimpiga sana na hakukuwa na dalili zozote za msaada kutoka sehemu yoyote ile kwani hata meli zenyewe ambazo zilitakiwa kutoa msaada, zilikuwa zimegeuzwa, chini juu, juu chini.

Muda ulizidi kwenda mbele, hakukuwa na dalili zozote zile za maji hayo kupungua, alipigwa na baridi usiku kucha, alikesha huku akiwa amelala katika jengo hilo juu kabisa, katika kila upande alioangalia, aliona maji, maji kila sehemu.

Siku hiyo ikakatika pasipo msaada wowote ule, kulipokucha, kidogo maji yakaanza kupungua, kutoka kwenye floo ya mia na hamsini aliyokuwepo mpaka mia na ishirini. Hapo akamshukuru Mungu, alichokifanya ni kuanza kushuka kwenda kwenye floo za chini, alifanikiwa kuvunja zaidi vioo vilivyovunjika na kuingia humo.

Hizo zilikuwa ofisi za Kampuni ya Madini ya Americanite ambayo ilikuwa ikipokea madini ya Tanzanite kutoka nchini Tanzania. Kwanza alipoona maneno yakiwa yameandikwa Americanite Company Limited, hakuamini, akaanza kusogea kulipokuwa na mlango wa kuingilia.

Akaingia kwenye mlango mmoja ambao ulikuwa kama sehemu ya kuingia katika mlango wa siri wa sehemu ya kuhifadhia madini ya bei kubwa. Kweli alipoufikia mlango huo, akaukuta ukiwa umefunguka kidogo kutokana na kupigwa sana na maji, akaufungua na kuingia ndani.

“Ooh! My God!” (Mungu wangu!) alijikuta akisema kwa mshtuko.

Kilichokuwa kikionekana mbele yake kwenye kabati kilikuwa ni madini ya almasi ya Americanite, alishtuka, yalikuwa mengi ambayo yangemfanya kuwa bilionea wa kimataifa. Aliyaangalia kwa tamaa lakini hakuwa na nguvu ya kuyachukua, kitu peke alichokihitaji kwa wakati huo ni chakula tu.

“Kwanza chakula, la sivyo nitakufa...” alijisemea huku akianza kuzungukazunguka humo ndani, bahati mbaya kwake, hakukuta chakula chochote kile.

****

Hali ilitisha, dunia ilitingishika, kile kilichotokea jijini New Orleans nchini Marekani kilimshangaza kila mmoja. Hilo halikuwa tsunami kama walivyolitegemea, lilikuwa kitu kingine ambacho kilikuwa tofauti na tsunami.

Hakukuwa na tsunami la hivyo, yaani la maji kusimama sehemu moja na kutengeneza mafuriko makubwa. Kitu kama hicho walizoea kukiona kwenye filamu mbalimbali za Kimarekani, ila leo hii, zile filamu zilionekana kuwa kweli, mafuriko yakaja na mali nyingi kuharibika.

New Orleans ikageuka na kuwa bahari kubwa, majengo hayakuonekana zaidi ya jengo moja tu ambalo lilikuwa refu kuliko majengo mengine jijini hapo. Waandishi wa habari wote walikwenda katika Jijini la Gonzalez ambalo lililokuwa kilometa ishirini kutoka katika Jiji la Orleans.

“Hii ni bahari,” alisema mwanaume mmoja, alionekana kushangaa, maji yalianzia hapo aliposimama mpaka ndani ya jiji hilo.

Taarifa zikatolewa kwamba miongoni mwa watu wote waliokuwa wakiishi katika jiji hilo, wote waliokolewa isipokuwa watu wawili tu, mwanaume aliyekuwa na mpenzi wake aliyekuwa mjauzito.

Hakukuwa na mtu aliyejua mahali watu hao walipokuwa kwani hata wanajeshi wa mwisho kabisa kwenda katika jiji hilo kuwatafuta, hawakuwapata japokuwa walikuwa na helkopta na kutangaza huku na kule lakini bado kulikuwa kimya.

Wazazi wao walikuwa wakilia tu, hawakuamini kama kweli watoto wao walikuwa wamekufa au la. Watu wengine waliwafariji kwa kuwaambia kwamba watoto wao walikuwa hai lakini hilo hawakukubaliana nalo hata kidogo, walichokuwa wakikiona mbele yao ni kwamba watoto wao walikufa katika maji yale.

Usiku hawakulala, sehemu waliyowekwa ambayo ilikuwa na maturubai mengi ilionekana kuwa salama na ndiyo sehemu ambayo serikali ya Marekani ilitoa kwa wahanga hao.

Ilipofika usiku wa saa nane, mwanaume mmoja akaingia katika turubai lao na kuwaita, mwanaume huyo alikuwa na taarifa mbaya ambayo alitaka kuwapa.

“Kuna nini?” aliuliza mama Catherine.

“Njooni huku,” alisema mwanaume huyo ambaye alikuwa mwanajeshi.

Hawakujua kuna nini lakini wakahisi kwamba inawezekana binti yao alikuwa amepatikana hivyo wakakaza miili yao kumfuata mwanaume huyo. Wakaenda katika turubai jingine alilokuwa akiishi baba yake James na kuwachukua wazazi wa mwanaume huyo na kuondoka nao.

Huko walipokwenda ilikuwa ni kwenye turubai la huduma ya kwanza ambapo wakaambiwa wasubiri kwani kulikuwa na mwili wa mtu mmoja ulipatikana.

“Ni mwanaume au mwanamke?” aliuliza mama yake Catherine.

“Subiri wala msijali, mtajua tu,” alisema mwanaume huyo na kuingia ndani.

Baadaya dakika chache akatokea mwanaume mwingine, alikuwa daktari aliyevalia koti refu jeupe, akawataka kuingia ndani na kuutambua mwili uliokuwa umepatikana, walipoingia, wakachukuliwa na kupelekwa katika chumba kimoja, huko kulikuwa na maiti iliyofunikwa kwa shuka la kijani. Wakaufuata mwili huo na kulitoa shuka.

Hawakuamini walichokiona mbele yao, shuka ile ilipofunuliwa na kuuangalia mwili huo, ilikuwa maiti ya binti yao, Catherine. Wakashindwa kuvumilia, hapohapo wakaanza kulia na hivyo wazazi wa James kuanza kuwabembeleza.

“Na kijana wetu yupo wapi?”

“Hatujui mpaka sasa! Huu mwili uliletwa na maji, kwa hiyo mwingine hatujui,” alijibu mwanajeshi mmoja.

Walipoambiwa kwamba binti huyo alikuwa mjauzito hata kabla ya tsunami kupiga, ndipo walipoanza kumchunguza na kugundua kweli alionekana kuzaa muda wa saa chache zilizopita kutokana na sehemu zake za siri zilivyokuwa.

“Inaonyesha kwamba alijifungua...” alisema daktari huyo.

“Mtoto wake yupo wapi?”

“Hatujui yupo wapi! Tulimpata mwanamke tu, mtoto hatufahamu chochote kile kama yupo hai au alikufa...” alijibu daktari huyo maneno yaliyowafanya watu hao kuanza kulia mahali hapo.


Utajiri mkubwa ulikuwa mbele yake lakini hakuwa na muda wa kuuchukua, kitu pekee alichokiangalia kilikuwa ni chakula tu. Hakujua afanye nini, alibaki akizunguka kwa kwenda huku na kule, yaani apande ngazi, mara ashuke, alikuwa akijifikiria tu ni kitu gani alitakiwa kufanya kuiokoa nafsi yake.

Wakati akizunguka huku na kule katika floo hiyo ya mia moja na ishrini ndipo akakumbuka kwamba katika floo ya mia na kumi na nane kulikuwa na mgahawa wa McDonald ambao ulitumika kwa watu waliokuwa wakifanya biashara katika jengo hilo.

Akaelekea kwenye dirisha na kuchungulia, maji yaliendelea kupungua na katika kipindi hicho ndiyo yalikuwa yakienda katika floo hiyo. Hakutaka kuchelewa, akaanza kuteremka kuelekea katika floo hiyo.

Alipoifikia, kulikuwa na maji yaliyomfikia kiunoni, hakutaka kurudi nyuma, tumbo lake lilikuwa tupu hivyo pasipo kufanya harakati za kutafuta chakula, basi angeweza kufa kwa njaa na si kwa mafuriko.

Kulikuwa na vyakula mbalimbali, vyote hivyo vilikuwa vimelowanishwa na maji. Kulikuwa na pizza, bugger, sandwich na vyakula vingine lakini vyote hivyo havikutamanika hata kidogo.

Mbele kabisa macho yake yakatua katika friji moja lililokuwa limepachikwa ukutani, akaanza kulifuata huku akiwa na kiu ya kutaka kunywa hata vinywaji vilivyokuwa humo ndani, alipolifikia, akalifungua na kuangalia ndani.

Kulikuwa na vinywaji vingi, mbali na vinywaji hivyo, pia kulikuwa na biskuti. Hakutaka kuchelewa, aliona kama angekosa, haraka sana akaanza kuchukua vinywaji na biskuti hizo na kuanza kula.

Alikula kwa fujo, hakumeza kilichokuwa mdomoni, akakiweka kingine. Ulaji wake tu ulionyesha ni jinsi gani alikuwa na njaa. Kula tu, alitumia muda wa dakika kumi na tano, tumbo lake likawa afadhali.

Kumbukumbu za mpenzi wake zikamjia tena, akapanda kwenye floo ile aliyotoka, yenye almasi nyingi na kutulia. Machozi yakaanza kumwagika, hakuamini kama mwisho wa siku angekosa kila kitu, yaani mtoto wake na mpenzi wake, hakika moyo wake ulimuuma mno.

“Ni lazima niondoke, siwezi kukaa hapa,” alisema James.

Kitu kilichokuwa kichwani mwake ni kwamba ilikuwa lazima achukue almasi zile na kuondoka nazo kwani bila kufanya hivyo asingeweza kuzipata tena kwani endapo maji yangepungua, ulinzi ungeimarishwa tena, ilikuwa ni bora kuzichukua kwani hata wamiliki wangekuja, wangehisi kwamba maji yalizihamisha almasi hizo.

Alichokifanya ni kurudi kulekule alipokuta chakula na kisha kuling’oa friji lile na kutoa kila kitu, kwa kutumia nguvu zake, akalibeba na kupanda nalo kwenda juu. Huko, akaufungua mlango wa chumba kile kilichokuwa na almasi, akaziangalia kwa tamaa kubwa kisha kuanza kuzitoa na kuziweka ndani ya friji lile.

Zilikuwa nyingi zenye uzito wa kilo tano ambazo kwa hesabu ya harakaharaka iliyokuja kichwani mwake, ilikuwa ni zaidi ya kupata dola bilioni hamsini, kiasi kikubwa sana cha fedha ambacho kingemfanya kuwa miongoni mwa mabilionea kumi wakubwa katika ulimwengu huu.

Alipomaliza kuzipakia, hakutaka kupoteza muda, ilikuwa ni lazima kuondoka, akaingia ndani ya friji, akachukua mbao kubwa ambayo alitaka kuitumia kupigia kasi kuelekea sehemu isiyokuwa na maji.

Kwa sababu tayari giza lilianza kuingia, akajipa uhakika kwamba sehemu ambayo angekwenda ingekuwa salama kwani kote huko kulikuwa na maji, yaani Jiji la New Orleans halikuonekana, lilikuwa bahari tu.

Naye akaingia ndani ya lile friji, hakutaka kuendelea kukaa ndani ya jengo hilo, akaanza kupiga kasi huku akiwa ameutoa mlango wa friji, almasi zilikuwa humo ndani tena huku akiwa amezifunika kwa nguo.

Hakujua alipokuwa akielekea, kitu pekee alichokijua ni kwamba upande aliokuwa akielekea ni ule usiokuwa na bahari. Alikuwa akipiga kasia, tena huku kukiwa na giza tayari, hakutaka kuangalia alipotoka, macho yake yalikuwa mbele tu.

Majengo marefu ambayo nayo yalifunikwa na maji yalikuwa yakionekana vizuri machoni mwake, hali ilitisha sana, alijikuta moyo wake ukiumia na machozi kuanza kumbubujika.

Hakutaka kusubiri, aliendelea na safari yake. Safari hiyo ilianza saa moja usiku, alijikuta akienda, akipiga kasia zaidi, saa nne baadaye, bado hakuwa amefika sehemu yoyote ya nchi kavu, bado alikuwa sehemu yenyemaji mengi.

Wakati akiendelea na safari yake, ndipo alipoanza kusikia muungurumo wa helkopta, hakutaka kuomba msaada, alichokifanya ni kujifunika na zile nguo zilizokuwa zimefunika almasi na kutulia.

Aliisikia helkopta ile ikipita juu yake, hakutaka kufungua, hakutaka kuonekana kwani aliamini kwamba kama angeonekana na kuokolewa basi zile almasi ambazo alikuwa nazo zingechukuliwa na hivyo yeye kubaki mikono mitupu.

“Siwezi kutamani kuokolewa na wakati nina utajiri mkubwa...” alisema James huku akiwa chini ya nguo zile.

Aliendelea na safari yake kama kawaida. Akafika sehemu ambayo maji yake yalionekana kupita kwa kasi kidogo. Hakutaka kusumbuka kufikiria sehemu hiyo kulikuwa na nini, alijua jinsi hali ilivyokuwa hivyo akagundua kwamba sehemu hiyo kulikuwa na mto.

“Mto Mississippi...” alijikuta akijisemea.

Huo ndiyo ulikuwa ukweli wenyewe, japokuwa maji yalikuwa yamejaza sana lakini aligundua kwamba sehemu iliyokuwa ikipitisha maji hayo kwa kasi kulikuwa na Mto Mississippi. Hakutaka kugeuza, akataka aelekee mbele huku akijua kwamba ili kuyaokoa maisha yake na utajiri mkubwa aliokuwa nao, ilikuwa ni lazima kuvuka eneo hilo. Akapiga moyo konde.

Akaendelea kupiga kasia, japokuwa alikuwa amechoka lakini hakutaka kupumzika, hakutaka kukata tamaa, aliendelea mbele zaidi tena kwa sababu alikuwa akivuka sehemu yenye mto uliokuwa ukipeleka maji kwa kasi, hata nguvu zake za kupiga kasi ziliongezeka.

Friji likaanza kupelekwa huku na kule, hakutaka kukata tamaa, aliendelea zaidi lakini maji yale yalionekana kuwa na nguvu kubwa. Hakuacha, kama kufa, ilikuwa lazima afe lakini si kuuacha utajiri ule kupotea mikononi mwake.

Akaendelea kupiga kasia, ikafika kipindi akashindwa kabisa kuendelea, akajikuta akiacha na kuona mto huo ungempeleka wapi. Alikwenda mbele mpaka sehemu ambayo maji ya bahari ile yalipoanza kupungua na mwisho kuishia kabisa hivyo kubaki kwenye maji ya mto tu.

Pembeni yake hakukuwa na majengo yoyote, ni pori kubwa lililokuwa likizinguka mto Mississippi. Alitamani kulipeleka friji lile pembezoni mwa mto ule ikiwezekana hata kutulia katika pori hilo lakini hakuwa na nguvu za kufanya hivyo.

Aliendelea kusonga mbele huku akiwa hoi. Alichoka, usingizi ulimkamata lakini hakutaka kulala kabisa, aliendelea kusonga mbele lakini mara ghafla akaanza kusikia sauti kubwa ya maji.

Akashtuka, akaangalia mbele yake, umbali kama hatua mia moja za miguu ya binadamu akaona maji yakielekea chini, yaani kulikuwa na maporomoko ya Mto Mississippi yaliyoitwa St. Antony yaliyopo Kaskazini mwa Jiji la New Orleans.

“Mungu wangu!” alijikuta akisema.

Kitu cha kwanza kabisa kilichokuja akilini mwake ni kwamba kama angeruhusu friji hilo lidondoke katika maporomoko hayo yaliyokuwa na urefu wa mita mia moja basi ingekuwa rahisi kwake kupoteza almasi hizo kwani friji lingeanguka, wakati linafiki chini lingejipindua na hivyo almasi zote kutoka ndani ya friji.

Hakutaka kuona hilo likitokea, alihangaika sana, alipambana kuzipigania almasi hivyo, kwa nafasi aliyokuwa nayo, japokuwa alichoka lakini hakutaka kuruhusu jambo hilo litokee. Nguvu zikamjia upya, friji lilizidi kusogea kule kulipokuwa na maporomoko, alichokifanya ni kupiga kasia kurudi nyuma, tena kwa kasi, ila kutokana na nguvu za maji ya mto ule, akajikuta akifanya jambo lisilosaidia, friji lile likazidi kupelekwa kule kulipokuwa na maporomoko yale, ndoto za kuwa bilionea zikaanza kupotea kichwani mwake.

Akabakiza kama hatua thelathini tu kuyafikia maporomoko yale, maporomoko ambayo yangeupoteza utajiri aliokuwa nao ndani ya friji lile.

****

“Lord have mercy on us...” (Mungu utuhurumie...)

Hayo yalikuwa maneno machache yaliyotoka kinywani mwa mchungaji wa Kanisa la Water of Life lililokuwa Mji wa Kenner, pembezoni mwa Jiji la New Orleans. Washirika wote walitoka kanisani huku wakionekana kuwa na majonzi mazito, hali iliyokuwa ikionekana iliwatisha wote, hawakuamini kama kweli maji yalihama kutoka baharini na kulifunika jiji la New Orleans.

Hapo Kenner ilionekana kama ufukweni kwani maji yote ya bahari yaliyoifunika New Orleans, yaliishia ndani ya jiji hilo. Walipoangalia kule yalipoanzia, hakukuwa na jengo lolote lililoonekana, kote huko kulifunikwa na maji na kulifanya eneo lote kuonekana kama bahari moja kubwa.

Hilo lilionekana pigo kubwa lililowahi kuikumba nchi ya Marekani, achana na lile shambulizi la septemba 11 mwaka 2001 ambapo majengo mawili ya WTC yalipolipuka baada ya kugongwa na ndege.

Washirika hao wakarudi kanisani kwani bado walikuwa kwenye maombi mazito katika kipindi hicho cha mkesha wa mwisho wa mwaka, kilichofuatia ni kuanza kuomba, walimuomba Mungu awanusuru na kile kilichokuwa kimetokea. Siku hiyo ilikuwa ni ya huzuni kubwa, vyombo vya habari viliendelea kutangaza hali iliyokuwa ikiendelea katika Jiji la New Orleans japokuwa taarifa za awali zilisema kwamba hakukuwa na mtu aliyekufa, ila majengo na vitu vingine viliharibika sana.

Vitu vinavyoweza kuhamishwa vilihama na vingi vilionekana juu ya maji vikielea, vingi vilipelekwa na maji mpaka huko Kenner, na vitu ambavyo vilipelekwa na maji hayo mpaka Kenner lilikuwa lile friji alilowekwa mtoto.

Friji hilo lilipokuwa likifika katika sehemu hiyo pembeni ya kanisa, hakukuwa na mtu aliyegundua kwamba ndani ya friji lile kulikuwa na mtoto. Kama vilivyokuwa vitu vingine, hata lile friji washirika wa kanisa hilo wakaamua kulipuuzia na wao kuingia kanisani.

Maombi yaliendelea, huku kila mmoja akiwa kwenye uwepo wa Mungu, ghafla wakaanza kusikia sauti ya mtoto ikilia. Hawakujua sauti hiyo ilitoka wapi, wakabaki wakiangaliana tu, kila mwenye mtoto, alimwangalia mtoto wake, alikuwa kimya, sasa hiyo sauti ya mtoto ilitoka wapi?

Ilikuwa ni usiku sana, saa zao zilionyesha kwamba tayari ilikuwa ni saa sita usiku, sasa sauti ya mtoto hiyo ilitokea upande gani na wakati watoto wote ndani ya kanisa walikuwa wamelala.

“Who is that baby?” (Mtoto gani huyo?) aliuliza mchungaji kwa sauti ya chini.

Mwanaume mmoja akatoka akaelekea nje, alitaka kumuona huyo mtoto aliyekuwa akilia, alipofika nje, hakuweza kuisikia sauti hiyo, alijaribu kuangalia huku na kule, ukimya mkubwa ulitawala, ni vitu vilivyoletwa na maji ya bahari ndivyo vilivyoonekana.

Akarudi ndani na kutoa taarifa kwamba hakukuwa na mtoto yoyote yule. Huku mchungaji akijiuliza ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, sauti ya mtoto huyo ikaanza kusikika tena.

Mchungaji akaamua kutoka yeye mwenyewe, mkononi mwake alikuwa na rozali na kila hatua aliyokuwa akipiga, alikuwa akimuomba Mungu. Alipofika nje, akaanza kuangalia huku na kule, bado sauti ya mtoto yule ilikuwa ikisikika lakini kila alipoangalia huku na kule, hakumuona.

“Huyo mtoto yupo wapi?” aliuliza mshirika mmoja.

“Hata mimi sijui, sauti naisikia, ila mahali alipokuwa, sijui yupo wapi,” alijibu mshirika mmoja.

Mchungaji aliendelea kusogea mpaka kulipokuwa na friji moja, humo ndipo sauti ilipotoka, kwa haraka pasipo kupoteza muda mchungaji akalifungua friji hilo, alichokutana nacho hakuamini, macho yake yakatua kwa mtoto mdogo ambaye alionekana kuzaliwa siku hiyohiyo, alikuwa wa kiume, harakaharaka akamtoa kutoka ndani ya friji hilo.

Washirika wote waliokuwa nje ya kanisa hilo ambao macho yao yalikuwa yakimwangalia mchungaji huyo walibaki kushangaa, wakasogea mpaka mchungaji alipokuwa na kuanza kumwangalia mtoto huyo.

Alikuwa mzuri wa sura lakini kila mmoja akaanza kumuonea huruma, bado mwili wake ulikuwa na damu nyingi zilizoganda. Walichokifanya ni kumchukua na kwenda naye kanisani, kitu cha kwanza kabisa walichomfanyia ni maombezi kisha kujadiliana mtu ambaye alitakiwa kumchukua mtoto huyo kwa ajili ya kumlea baada ya kutoa taarifa polisi.

“Naomba nikamlee mimi,” alisema mwanamke mmoja, alikuwa mtu mwenye uwezo wa kifedha humo kanisani.

“Naomba nikamlee mimi,” alisema mwanamke mwingine, mjane ambaye mtoto wake pekee alikufa baada ya kuugua ugonjwa wa polio.

Alichoamua mchungaji ni kumgawia mwanamke yule mjane mtoto huyo na kwenda kuishi naye kwani maisha ya upweke aliyokuwa akiishi waliamini kwamba mtoto huyo angempa furaha. Mwanamke yule mjane akamchukua mtoto huyo na kumpa jina la Dylan.


Kitu kilichomjia kichwani mwake ni kwamba alikuwa akienda kupoteza utajiri wote aliokuwa nao katika maporomoko yaliyokuwa mbele yake. Alijitahidi sana kupiga kasia kurudi nyuma lakini bado friji lile liliendelea kupelekwa kule kulipokuwa na maporomoko yale.

Akashindwa kujua ni kitu gani alitakiwa kufanya kwani kwa jinsi hali ilivyokuwa ikilikuwa ni lazima almasi zile zitumbikie ndani ya mto na hivyo kuibuka na mikono mitupu.

“Haiwezekani....” alisema James.

Alichokifanya ni kuvua suruali yale aliyoivaa kisha kuchukua zile almasi na kuzitumbukiza ndani ya miguu ya suruali ile kisha kuifunga vilivyo. Hakuridhika, alichokifanya kama nyongeza ni kuvua fulana yake, akaichukua ile suruali na kuiingiza ndani ya fulana yake kisha kuifunga vilivyo, alipomaliza, akawa tayari kwa kutumbukia ndani ya maporomoko yale.

Friji lilizidi kusogea, akaanza kumuomba Mungu kwamba hata kama friji lile lingeanguka katika maporomoko yale basi huko chini asikutane na jiwe lolote lile ambalo lingemuumiza na hata kumuua. Wakati sala ikiendelea na hata kabla hajasema ‘Amen’ tayari friji lilifika katika maporomoko hayo na kuanza kuanguka chini.

James hakupiga kelele, alitulia ndani ya friji ambalo liliendelea kwenda chini na baada ya kufika umbali fulani, likajigeuza, James akatolewa ndani ya friji kwani tayari lilikaa juu-chini.

“Mungu nisaidie...” alisema maneno hayo, hakuwa na sentensi nyingine ambayo angeisema zaidi ya kumwambia Mungu amsaidie na kumuokoa katika hilo.

Alipotua chini, hakuwa ndani ya friji, yeye alikuwa upande mwingine na friji lilikuwa upande mwingine kabisa. Japokuwa alikuwa kwenye purukushani lakini hakuuachia mzigo wake wa almasi, aliushikilia vizuri kwani huo ndiyo ulikuwa kila kitu.

Akaulegeza mwili wake, akaanza kupelekwa na maji mpaka alipofika sehemu ambayo kulikuwa na watu wengi, hasa wasichana waliokuwa wakiogelea. Walipomuona tu, kitu cha kwanza kilikuwa ni kutoka mtoni huku wakipiga kelele, walihisi kwamba ilikuwa ni maiti.

Huko nje ya mto, walisimama na kuanza kumwangalia James ambaye bado aliulegeza mwili wake kama mtu aliyekufa hivyo kumfanya kuelea juu ya maji.

“Ni maiti au?” aliuliza msichana mmoja.

“Labda ni mhanga wa maji yaliyojaa huko New Orleans...” alijibu msichana mmoja.

Walichokifanya ni kuendelea kusimama mpaka pale James alipoanza kukurukakukuruka pale majini. Hali hiyo ikawafanya wasichana hao kugundua kwamba mtu huyo hakuwa amekufa kama walivyofikiria bali alikuwa hai kabisa.

Ingawa alikuwa amechoka lakini kwa kutumia miguu yake, James akaanza kupiga mbizi kuelekea nchi kavu, hakuchukua muda mwingi, akafika na kutulia pembeni kabisa huku akionekana kuchoka mno.

Almasi zile alizozitoa New Orleans, alikuwa nazo katika nguo ile, hakutaka mtu yeyote afahamu kilichokuwa ndani ya suruali ile. Wasichana wale waliogopa, wakati mwingine walimuona James kama mzimu ambao ulikuja kwa ajili ya kuwamaliza tu.

Hakukuwa na aliyemsogelea, wote wakajikaushia pembeni kabisa tena huku wengine wakiwa wanatetemeka.

“Where am I? (nipo wapi hapa?) aliuliza James huku akiwaangalia mmoja baada ya mwingine.

“St. Antony....” alijibu msichana mmoja huku akionekana kuwa na hofu usoni mwake.

Aliposikia hivyo, James hakutaka kubaki mahali hapo, akasimama na kuanza kuondoka zake tena huku akiwa na kipensi tu mwilini mwake. Kwa sababu ilikuwa ni alfajiri, hakutaka kuwa na haraka ya kuuza madini hayo, kitu alichokitaka ni kupata sehemu ya kuishi, hata kama ni ya muda, hiyo ingekuwa nafuu kwake.

*****

Safari yake ikaishia katika eneo lililokuwa na nyumba chache zilizojengwa kwa mpangilio mzuri. Sehemu hiyo ilionekana kama kijiji, alichokifanya ni kuifuata nyumba moja ambapo mbele kulikuwa na trekta moja kubwa, akaufuata mlango na kuanza kuugonga.

Wala haukuchukua muda mrefu, mlango ukafunguliwa na mzee mmoja aliyeshika mgobole, alipomuona James, akashtuka kwani mtu aliyesimama mbele yake alionekana kuwa dhaifu, mtu aliyechoka mno.

“Who the helll are you?” (Wewe ni nani?) aliuliza mzee yule huku akimnyooshea gobole lile.

“A Young Bilionaire...” (bilionea kijana) alijibu James huku akiuweka vizuri mzigo wake wa almasi.

Mzee yule alipomwangalia mwanaume huyo aliyejitambulisha kwa jina la Bilionea Kijana akabaki akimshangaa, kwake, mwanaume huyo alionekana kuwa dhoofu, masikini ambaye alihitaji msaada mkubwa kutoka kwake.

Akamkaribisha ndani ambapo James akahitaji kuletewa chakula kwani alikuwa amechoka mno na njaa ilimkamata. Wakati ameletewa chakula na kuanza kula, mke wa huyo mzee akafika huku akiwa na binti yake, wakabaki wakimshangaa James, alikuwa mgeni ambaye hawakuwa wakimfahamu, je kwa nini alifika hapo? Na kama alitoka sehemu, yeye alikuwa nani? Hawakuwa na jibu.

“Huyu ni nani?” aliuliza mwanamke huyo.

“Ni mtu aliyekuja kuomba msaada wa chakula, anaonekana kuchoka sana, nikaamua kumsaidia...” alijibu mzee huyo.

Wote walitulia huku wakimwangalia James ambaye alikuwa akila mfululizo hali iliyoonyesha kwamba alikuwa na njaa mno. Mzigo wake wa madini bado ulikuwa mkononi mwake, hakutaka mtu yeyote yule auguse kwani kwa kipindi hicho hiyo ndiyo ilikuwa roho yake.

“Wewe ni nani?” aliuliza mwanamke huyo.

“Naitwa Carthbert....” alidanganya James.

“Umetoka wapi?”

“Nimetoka mbali sana, ni mbali mno...”

“Ni wapi huko?” aliuliza mzee huyo.

“Harvey...nilikuwa nikiogelea mtoni, ghafla maji yakaanza kujaa, nikazama, nilipokuja kuibuka, nikaibukia huku,” aliendelea kudanganya.

“Pole sana...na nyie mlikumbwa na tsunami?”

“Kidogo sana, yaani sijajua kama wenzangu niliokuwa nikiogelea nao ni wazima au la kwani maji napo yalitukumba ingawa si sana,” alisema James.

Hakutaka kuzungumza ukweli hata kidogo. Kitu alichoogopa ni almasi zake kugundulika tu. Kwa sababu alikuwa nyumbani kwa watu hao, walichokifanya ni kumsaidia kwa kumwambia aishi nao mpaka pale ambapo angepata nafasi ya kurudi nyumbani kwake.

Hiyo ilikuwa furaha yake, hicho ndicho kitu alichokitaka, hakutaka kurudi, huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa safari yake ndefu. Katika nyumba hiyo, walikuwa watu wanne tu, yeye, mzee aliyejitambulisha kwa jina la Bellamy, mkewe Bellamy na binti yao, Claire aliyekuwa na miaka ishirini.

Akaonyeshwa chumba alichotakiwa kukaa, kwa sababu ilikuwa ni kijijini na hata nyumba zilizojengwa huko hazikuwa zile zenye ubora mkubwa, akatafuta sehemu nzuri na kuyaficha madini yale, sehemu ambayo alihakikisha kwamba kusingekuwa na mtu yeyote yule ambaye angeyaona.

Muda mwingi James alikuwa chumbani kwake, huko, alikuwa akilia tu, hakuamini kitu kilichotokea, tsunami ile iliyopiga New Orleans iliharibu kila kitu. Aliamini kwamba mpenzi wake, Catherine alifariki dunia lakini pia kitu kilichomuuma zaidi ni kwamba mtoto wake wa kwanza kabisa katika maisha yake naye alifariki dunia.

Moyo wake ulimuuma mno, alijisikia maumivu makali moyoni mwake, kuna kipindi hakuwa akilala, alikesha usiku mzima akiwa analia tu. Kwa kuwa nyumba hiyo ilikuwa na televisheni, alichokifanya ni kufuatilia kuona kama kulikuwa na mtu mwingine aliyepona katika tsunami ile.

Maji hayakuwa yamekauka vya kutosha, maghorofa yalianza kuonekana na kadiri upepo ulivyopiga ndivyo maji yalivyopungua kwa kurudi baharini. James alitia huruma, kwa kumwangalia tu ilikuwa rahisi kujua kwamba mtu huyo alikuwa kwenye matatizo makubwa.

Msichana Claire ndiye alikuwa mfariji wake, mara kwa mara alikuwa pamoja naye, alizungumza naye mambo mengi na ndiye alikuwa mtu wa kwanza kumwambia ukweli juu ya kile kilichotokea.

“Mungu wangu! Pole sana....” alisema Claire, alihuzunika, stori ya James ikaanza kumtoa machozi.

“Usijali Claire, namshukuru Mungu nipo hai japokuwa ninaumia sana,” alisema james.

“Kwa hiyo hujajua kama Catherine alinusurika au la?”

“Sijajua...”

“Na mtoto je?”

“Naye sijajua Claire...”

Kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo watu hao walivyozidi kuwa karibu. Muda mwingi msichana Claire alikuwa chumbani kwa James, huko walizungumza mengi huku msichana huyo naye akitumia muda mwingi kuelezea uhusiano wake na mwanaume wake aliyempenda lakini mwisho wa siku kuumizwa vibaya na mwanaume huyo kwa kumuoa msichana mwingine.

Wawili hao wakabaki wakifarijiana lakini mwisho wa faraja hiyo ikaishia kwenye kubadilishana mate na mwisho wa siku kujiangusha kitandani na kuanza kuvunja amri ya sita.

Hiyo ndiyo ikawa tabia yao, kila siku ilikuwa ni lazima kwa Claire kwenda chumbani kwa James na kulala naye kisiri pasipo wazazi wake kugundua lolote lile. Walijisahau, kila mmoja akajikuta akimpenda mwenzake, baada ya kukaa kwa mwezi mmoja, wakashindwa kuvumilia na mwisho wa siku mapenzi yao yakaanza kuonekana hata mbele ya wazazi wa Claire.

“Nini kinaendelea kati yenu?” aliuliza mama yake.

“Ninampenda James mama...”

“Unasemaje?”

“Ninampenda James, nataka tuoane...”

“Una uhakika unampenda?”

“Ndiyo mama! Ninampenda kwa moyo wa dhati na sidhani atafanya kama alivyofanya Stephen...James ni wa tofauti sana...” alisema Claire huku akianza kububujikwa na machozi ya hisia kali ya mapenzi.

Mama yake akaja kumwambia mzee Bellamy ambaye wala hakuwa na kipingamizi chochote kile, tena kwa sababu sehemu yenyewe ilikuwa kijijini, wanaume wachache, akakubaliana naye na hatimaye kujiweka wazi kabisa, kuwa pamoja kila sehemu huku wakionyeshana mapenzi ya mnato kama njiwa.

“James....”

“Sema mpenzi...”

“Kuna kitu nataka kukwambia.”

“Kitu gani?”

“Nahisi nina mimba...”

“Unahisi una nini?”

“Mimba....”

“Unahisi au unayo?”

“Ninayo..sijaona siku zangu, pia ninaziona dalili zote...” alisema Claire.

“Kweli?”

“Kweli tena!”

James akashindwa kuvumilia, hapohapo akamsogelea Claire na kilichofuatia ni kumkubatia kwa furaha. Baada ya kumpoteza mtoto wake ambaye mpaka kipindi hicho hakujua kama alikuwa hai au alikufa, hatimaye Mungu alimuona kwa jicho jingine kwa kumpa mimba Claire, hivyo akatarajia kupata mtoto baada ya miezi tisa. Furaha aliyokuwa nayo, haikuweza kuelezeka.


Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kila kitu, maisha yao yakabadilika na James hakuwa radhi kuondoka, alizoeleka ndani ya nyumba hiyo na kitu pekee alichokibakiza ni kufunga ndoa na msichana Claire ambaye alikuwa na mimba yake.

Hakuwakumbuka wazazi wake, kichwa chake kilimwambia kwamba tayari wazazi wake nao walikuwa marehemu kutokana na tsunami lilivyopiga na hivyo vingi vingi kuharibika.

Hakutaka kujali sana, mtu ambaye alikuwa akimfikiria kwa wakati huo alikuwa msichana wake tu. Siku zikaendelea kukatika, hakutaka kumwambia Claire kuhusu zile almasi alizokuwa nazo, alikuwa msiri na alitaka kuzungumza naye kuhusu hilo mpaka pale atakapomuoa na kuwa mke wake wa ndoa.

Maisha hayakuwa mepesi, yalikuwa magumu lakini akavumilia sana, kuna wakati alitamani kumwambia msichana huyo juu ya kile kilichofichika nyuma ya pazia lakini wakati mwingine aliona kwamba muda haukuwa tayari.

Siku zikaendelea kukatika, katika kipindi chote hicho alikuwa mtu wa kukaa kimya, japokuwa alikuwa na msichana Claire ambaye alimpa mimba lakini bado kumbukumbu za Catherine ziliendelea kukisumbua kichwa chake.

Miezi ikakatika kwa kasi na baada ya miezi tisa, msichana Claire akajifungua mtoto wa kike na kumpa jina la Catherine kama kumbukumbu ya msichana wake aliyekufa kwenye janga la tsunami.

Kwake ilikuwa furaha tele, kila alipomwangalia mtoto huyo, alifanana naye sana. Muda wote James alikuwa na furaha tele, alimshukuru Mungu kwa kile kilichotokea na kila Jumapili alihakikisha anakuwa mtu wa kwenda kanisani tu.

“Ninakupenda, ninataka kukuoa,” alisema James, kwa kumwangalia tu ingekuwa rahisi kugundua kwamba mtu huyo alichanganyikiwa kwa furaha.

Hayo ndiyo maneno aliyokuwa akimwambia mara kwa mara. Kwa Claire, hiyo ilikuwa furaha tele, alijua ni kwa jinsi gani wasichana wa hapo kijijini walitamani kuolewa ila hawakuwa na bahati ya kupata wanaume kutokana na idadi ndogo ya wanaume mahali hapo.

Ili kumuonyesha msichana huyo kwamba alimaanisha, baada ya mwezi mmoja, wawili hao walikuwa kanisani, mchungaji alisimama mbele yao huku kukiwa na idadi ya watu ishirini ambao walifika kwa ajili ya kuishuhudia harusi hiyo.

“Ndiyo nimekubali...” alijibu Claire huku akiachia tabasamu pana.

Jioni ya siku hiyo wakaondoka na kuelekea mjini ambapo wakachukua chumba katika hoteli moja na kutulia huko. Usiku wa siku hiyo walikesha huku wakiwa wamekumbatiana, hawakuamini kwamba mwisho wa kila kitu hatimaye wangekuwa pamoja na kufunga ndoa na kuwa mume na mke.

Kwa kuwa alipanga kwamba angemuweka wazi Claire siku ambayo angemuoa, siku hiyo ndiyo aliuona wakati muafaka wa kumwambia ukweli juu ya utajiri mkubwa aliokuwa nao ambao aliuficha ndani kwa kipindi cha miezi kumi.

Alipomwambia mke wake kwamba kulikuwa na kitu alitaka kuzungumza naye, mwanamke huyo akaonekana kuogopa kwa kuhisi kuwa inawezekana kulikuwa na jambo baya lilitokea na hivyo alitaka kumpa taarifa.

“Mbona unaonekana kuogopa?” aliuliza James.

“Unataka kuzungumza nami kuhusu nini mpenzi?”

“Usiogope, ni habari njema!”

“Ipi?”

“Nikuulize swali?”

“Niulize...”

“Unakumbuka baba yako aliponiuliza siku ya kwanza nilimjibu mimi ni nani?” aliuliza James huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.

“Ulimwambia wewe ni bilionea kijana...”

“Unaamini hilo?”

“Hapana!”

“Kwa nini?”

“Tumeishi kwa kipindi kirefu, sijauona huo ubilionea wako hata kidogo...”

“Leo nataka kukwambia kile nisichowahi kukwambia....”

“Kitu gani?”

“Kwamba mimi ni bilionea, tena bilionea wa kumi Marekani...”

“Unasemaje?”

“Huo ndiyo ukweli...”

Kwanza Claire akabaki kimya, akamwangalia mume wake huku akionekana kutokuamini kile alichomwambia, mara ya kwanza alifikiri ni utani lakini kila alipomwangalia mume wake huyo alionekana kumaanisha alichokuwa akikisema. Akajiweka vizuri kitandani na kumwangalia vizuri mume wake.

“Sijakuelewa....”

“Mimi ni bilionea, kuanzia kesho, tutanunua nyumba nzuri na kubwa, tutaendesha magari ya kifahari, tutafungua biashara nyingi na kubwa, nitakufanya uwe malkia wangu maisha yangu yote....” alisema James.

“Yote yanawezekana vipi haya?” aliuliza Claire.

Hapo ndipo James alipoanza kumuhadithia mke wake kile kilichotokea nyumba wakati tsunami ilipopiga. Hakutaka kumficha kitu, alimhadithia ukweli wa mambo na hakutaka kudanganya hata neno moja.

Claire alibaki kimya akimsikiliza, hakuamini kile alichokisikia. Aliukumbuka mzigo ambao aliubeba mwanaume huyo, alikuja nao nyumbani na hakumuachia mtu yeyote aone kile kilichokuwa ndani.

Moyo wake ukawa na furaha mno, hakuamini kama huo ndiyo ulikuwa mwisho wa umasikini waliokuwa nao, akamsogelea mumewe na kumkumbatia.

Huko katika fungate yao walikaa kwa muda wa wiki moja na ndipo wakarudi. Walipofika nyumbani, jambo la kwanza kabisa alilolifanya James ni kumuonyeshea mke wake ule mzigo aliokuwa nao, alipoufungua, Claire hakuamini alipoona madini ya Americanite, moja ya madini ghali zaidi duniani.

Huo nao ukawa mwanzo wa utajiri wao. Alichokifanya James ni kuwasiliana na watu waliohusika na madini kisha kuyauza kwa gharama kubwa. Hakuyauza yote, mengine alibaki nayo kwani yalikuwa mengi mno, kilo mbili hayakuwa madogo hata mara moja.

Mpaka robo ya madini yale yanamalizika, tayari alijitengenezea zaidi ya dola bilioni ishirini, zaidi ya trilioni arobaini. Maisha yake yakabadilika, akaanza kuingia kwenye utajiri mkubwa, akanunua majumba ya kifahari na kuanzisha biashara mbalimbali, akanunua ndege, akaanzisha kampuni zake mbalimbali.

James akawa bilionea, hakuwa masikini, akaanza kujulikana kwa Wamarekani kwamba alikuwa bilionea kijana ambaye alibadilisha maisha yake baada ya kuuza madini ya Americanite. Heshima ikawa kwake, wazazi wa Claire hawakuwa masikini tena, walinukia pesa, alihakikisha anabadilisha maisha ya kila mtu aliyehusika naye mara baada ya maafa makubwa kutokea jijini New Orleans.

“Where did this guy come from?” (Huyu jamaa ametoka wapi?) aliuliza jamaa mmoja.

“I don’t know where he came from,” (Sijui ametoka wapi)

Hilo ndilo lilikuwa swali la Wamarekani wengi, utajiri wake ulikuwa ni wa kushtukiza sana, wengi wakajiuliza juu ya mahali James alipotoka lakini hakukuwa na aliyejua. Akawaajiri wafanyakazi wengi katika kampuni zake ambazo kwa mwaka zilionekana kumuingizia zaidi ya dola bilioni ishirini, zaidi ya shilingi trilioni arobaini.



Wote walishtuka baada ya kupewa taarifa na dada wa kazi kwamba Catherine alikuwa amepoteza fahamu chumbani kwake. Wazazi wake wakatoka chumbani na kwenda chumbani kwake, walichoambiwa ndicho walichokutana nacho.

Kompyuta yake ilikuwa mbele yake, hawakutaka kujali sana, walichokiangalia ni afya ya binti yao hivyo walichokifanya ni kumchukua na kuanza kumpa huduma ya kwanza huku dada wa kazi akipewa jukumu la kumpigia simu daktari wa familia ili aweze kufika mahali hapo haraka iwezekanavyo.

Catherine alikuwa kimya kitandani alipolazwa, hakukuwa na aliyejua kitu gani kilikuwa kimetokea, walichanganyikiwa, huyo ndiye alikuwa binti yao wa kwanza, walimpenda mno kwa hiyo kitendo cha kupoteza fahamu hakika kiliwashtua na kuwauma mno.

Wote wakatulia wakimsubiri daktari wa familia aweze kufika, hawakuondoka chumbani humo, walikuwa pembeni yake huku kila mmoja akiwa na hofu moyoni mwake kwa kuhisi kulikuwa na jambo baya lilitokea kwani haikuwa rahisi hata kidogo kwa Catherine kuzimia, hakuwa na historia mbaya au ugonjwa wowote ule, sasa ni kitu gani kilimpekea kuzimia?

Kila walichojiuliza, hawakupata jibu, waliendelea kumsubiria daktari ambaye baada ya dakika kumi na tano, akawa ndani ya nyumba hiyo. Kwa haraka sana akaanza kuchukua vipimo kwa Catherine na kugundua kwamba msichana huyo alikuwa amepata mshtuko ambao uliupelekea moyo wake kupokea damu nyingi, tena kwa haraka sana hivyo kuzimia.

“Ila hana historia yoyote mbaya...” alisema Bwana James.

“Sawa! Ila inawezekana kuna kitu....”

Daktari akamtundikia dripu ya maji na kisha kumpa muda wa kupumzika huku kiyoyozi kikiendelea kupuliza. Baada ya dakika arobaini na tano, vidole vya Catherine vikaanza kutingishika hali iliyoonyesha kwamba alikuwa amerudiwa na fahamu.

“Mwacheni kwanza apumzike,” alisema daktari.

Kama walivyoambiwa ndivyo walivyofanya, wakampa muda zaidi wa kupumzika mpaka baada ya saa mbili ndipo wakaingia chumbani humo ambapo wakamkuta Catherine akiwa amejikunyata huku akilia kitandani mwake.

Wazazi hao wakamsogelea huku mioyo yao ikisikia maumivu makali mno, walipomfikia, nao wakakaa kitandani na kumuuliza tatizo lilikuwa nini mpaka kulia namna ile.

“Nimefeli...” alisema Catherine huku akiendelea kulia.

“Umefeli?” aliuliza baba yake.

“Ndiyo baba.”

Bwana James hakutaka kukubaliana na hilo, kwa kuwa matokeo yalikuwa wazi, akaichukua simu yake na kuanza kuperuzi, alitaka kuona kama kweli binti yake alikuwa amefeli kama alivyosema au kulikuwa na kingine kwani hakuamini kama kuna siku binti yake huyo angeweza kufeli mtihani.

Alipoangalia matokeo, akapigwa na mshtuko, japokuwa binti yake alisema kwamba alifeli lakini matokeo yalionyesha kwamba alikuwa mtu wa pili huku nafasi ya kwanza ikishikiliwa na mwanafunzi aliyeitwa Dylan

Matokeo yale yalionekana kuwa mazuri, baba yake aliyafurahia lakini kitu cha ajabu kabisa Catherine aliyakasirikia na ndiyo hayohayo yalimfanya kuzimia na hata kulia kipindi hicho.

“Nilitaka kuwa wa kwanza baba....” alisema Catherine huku mama yake akimbembeleza.

“Usijali mwanangu, matokeo si mabaya sana....”

“Kwa nini nimekuwa wa pili? Kwa nini nimeshuka? Kwa nini kuna mtu ana akili zaidi yangu? Kwa nini baba?” aliuliza Catherine.

“Huyu aliyeshika namba ya kwanza, hana akili zaidi yako, alikuwa mjanja katika vitu vichache tu binti yangu, amini kwamba wewe una akili zaidi yake,” alisema Bwana James.

“Kweli baba?”

“Ndiyo Catherine, wewe una akili mno...”

Yalikuwa maneno yenye faraja, yaliamsha ari mpya moyoni mwake, japokuwa wakati mwingine alikuwa na huzuni lakini kila alipokumbuka maneno ya baba yake yaliyomwambia kwamba alikuwa na akili mno, yalimpa nguvu mpya.

Matokeo hayo hakutaka kuyaangalia tena, alitaka kuyasahau kabisa, siku zikaendelea kukatika, kitu kilichousumbua moyo wake ni huyo mtu aliyeitwa kwa jina la Dylan ambaye matokeo yalionyesha kwamba alikuwa na akili kuliko yeye.

Alitaka kumuona, alifananaje, alikuwaje, kiu yake kubwa ikawa ni kumuona tu. Alitamani kwenda shuleni kwao, ila ilikuwa uswahilini sana, sehemu ambayo kulikuwa na wahuni wengi, kutoa bunduki lilikuwa jambo la kawaida na hata ukisikia mtu amechomwa visu vingi, hakuna kushangaa kwani mambo kama hayo yalikuwa yakitokea sana tu.

Kwa sababu waliambiwa kwamba watu kumi watakaofanya vizuri wangepata nafasi ya kwenda ikulu na kuonana na rais, alitaka kumuona huyo Dylan kwa kuamini kwamba ile kiu aliyokuwa nayo hakika ingepoa kabisa.

Siku zikaendelea kukatika huku akiendelea kuwa na kiu kubwa ya kumuona huyo Dylan, baada ya mwezi mmoja kukatika ndipo akapokea mualiko maalumu kwamba alikuwa akihitajika katika ikulu ya Marekani kama miongoni mwa wanafunzi waliofanya vizuri.

Siku ya kwenda huko, mama yake, bi Claire ndiye aliyekuwa msindikizaji mkuu, Bwana James hakutaka kwenda kwa sababu alikuwa bize na mambo yake ya biashara kwani siku hiyohiyo ndiyo aliyosafiri mpaka jijini Texas na kusaini mkataba na Wamexico kwa ajili ya kusambaza maji nchini humo.

Walipofika katika geti la ikulu, likafunguliwa na kisha kuingia ndani hasa baada ya shughuli zote za kupekuliwa zilipokamilika. Humo ndani, kulikuwa na sehemu maalumu iliyoandaliwa vizuri, watu walitakiwa kuwa huko.

Kulikuwa na wageni waalikwa, waandishi wa habari na watu wengi, wakatafuta sehemu iliyokuwa na viti viwili na kutulia hapo. Watu walizidi kuongezeka na baada ya dakika kadhaa, hafla ikaanza.

Muda wote Catherine alikuwa na shauku ya kuangalia huku na kule, bado alitaka kumuona huyo Dylan alikuwaje. Wakati rais akiwa amesimama, akaanza kuwaita wanafunzi hao kwa ajili ya kuchukua zawadi, akaanza kwa mtu wa kumi na kushuka chini.

“Naitwa Catherine, ninamshukuru Mungu kwa kufanya vizuri...” alisema Catherine huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.

Alipomaliza akashuka na ndipo jina la Dylan likatajwa. Catherine akajiweka vizuri, mtu aliyekuwa akitaka kumuona ndiye aliyeitwa, alitaka kumuona alifananaje mpaka awe na akili kuliko yeye.

Kijana huyo aliposimama na kwenda mbele, Catherine alimkazia macho, hakumuona kwa mbele, kwa kuwa alikuwa akielekea jukwaani, akabaki akiangalia mgongo tu, kijana huyo alipofika mbele, akapeana mkono na rais na kuwageukia watu waliokuwa mahali hapo.

Kitu cha ajabu kabisa, Catherine na mama yake wakapigwa na mshtuko mkubwa, walipomwangalia kijana huyo, alifanana sana na Bwana James, yaani kama wangesimama pamoja, ilikuwa ni rahisi kusema kwamba watu hao walikuwa mapacha.

“Mmmh!” wote walijikuta wakiguna kwa pamoja.

**

Kwa jina aliitwa Leticia Bullock Christopher, alikuwa miongoni mwa watu masikini waliokuwa wakiishi katika Jiji la Kenner. Watu wengi mahali hapo walimtambua kwa jina la widow yaani mjane.

Miaka michache iliyopita, mume wake ambaye aliyafanya maisha yake kuwa afadhali alifariki katika ajali iliyojaa utata mkubwa hali iliyowafanya watu wengi kuhisi kwamba kulikuwa na mkono wa mtu nyuma ya pazia.

Lilikuwa tukio baya, lililomhuzunisha, taarifa zikatolewa katika kituo cha polisi hapo Kenner kwa ajili ya kufuatilia kwa ukaribu chanzo cha ajali hiyo lakini hakuna kilichofanyika. Hakutaka kukata tamaa, akatoa taarifa mpaka katika Shirika la Upelelezi ndani ya nchi ya Marekani, Fideral Bureau of Investigation (FBI) lakini hakukuwa na kilichoendelea.

Alisikitika sana, pamoja na hayo, moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama yeye ndiye aliyekuwa akipitia maisha hayo, aliwachukia polisi wote, akawachukia wapelelezi wote nchini Marekani na wakati mwingine alihisi kwamba kulikuwa na mtu aliyeyafanya yote hayo, kumsababishia maumivu makubwa moyoni mwake.

Wakati akiwa katika huzuni kubwa juu ya kifo cha mume wake, mtoto wake aliyekuwa akimpenda ambaye alikuwa ndiye mfariji wa maisha yake, Carlos aliyekuwa na miaka minne, naye akafariki kwa ugonjwa wa polio ambao ulimtesa tangu kuzaliwa kwake.

Moyo wake ukaumia, maumivu aliyoyapata hayakuweza kuelezeka, alikuwa mtu wa kulia kila siku, kila kilichotokea katika maisha yake aliona kama alikuwa katika moja ya ndoto ya kusisimua ambapo baada ya muda fulani angeamka na kujikuta akiwa kitandani.

Kilichoendelea hakikuwa ndoto, yalikuwa matukio yaliyoendelea katika maisha yake halisi, maisha yake yaliendelea kuwa na huzuni mpaka pale alipofanikiwa kukabidhiwa mtoto mdogo, aliyekuwa amefunikwa ndani ya friji, huyo ndiye akawa furaha yake kwa mara nyingine.

Alimpenda mtoto huyo aliyempa jina la Dylan, alimlea katika malezi mazuri, hakutaka aishi kama watoto wengine wa mitaani ambao walikuwa na tabia mbaya, kitu cha kwanza kabisa alichokifanya ni kumpeleka sana kanisani kila alipohitajika.

Miaka ikakatika, Dylan akaendelea kukua katika mikono ya mwanamke huyo, hakujua kama aliokotwa, hakujua kama mwanamke huyo aliyemuita mama hakuwa mama yake, kila kitu kilichotokea kipindi cha nyuma kilikuwa siri kubwa sana.

“Mom...” aliita Dylan.

“Yes my son...” (Ndiyo kijana wangu)

“I want to be a pastor when I grow up,” (Nataka kuwa mchungaji nitakapokua) alisema Dylan.

“You will be my son, what you have to do is praying to God, anything can be possible through Him,” (Utakuwa tu kijana wangu, unachotakiwa kufanya ni kuomba, kila kitu kinawezekana kwake) alisema bi Leticia huku akimwangalia Dylan usoni mwake.


Siku zikaendelea kukatika, wakati Dylan anaanza kusoma hapo ndipo bi Leticia alipogundua kwamba mtoto huyo alikuwa na uwezo mkubwa mno. Alipelekwa katika shule ya uswahilini ya Mississippi Nusery School ambapo baada ya kufika hapo, yeye ndiye alikuwa mwanafunzi wa kwanza kujua kusoma na kuandika.

Hilo lilikuwa gumu kuaminika kwa walimu lakini ndivyo hali ilivyokuwa. Aliendelea kukua kila siku, uwezo wake uliendelea kuonekana kwani kwa kipindi kifupi alichokuwa amesoma shuleni hapo, hata kwenye kuandika hakuwa na tatizo lolote lile.

Bi Leticia alipopewa taarifa kwamba mtoto wake alikuwa na uwezo mkubwa darasani, akamshukuru Mungu kwa kumpa mtoto aliyekuwa na akili kama ilivyokuwa kwa Dylan.

Huo ulikuwa mwanzo tu, uwezo wake uliendelea kuonekana kila siku huku akiwaongoza wanafunzi kila walipofanya mtihani. Katika kipindi ambacho alimaliza masomo ya elimu yake ya chini ya msingi, Dylan ndiye aliyekuwa ameongoza kwa kufaulu vizuri zaidi ya wanafunzi wote shuleni hapo.

Hakuwa msomaji, hakuwahi kuchukua daftari na kujisomea, muda wake mwingi ulikuwa ni kwenda uwanjani na mpira wa kucheza kikapu. Hicho ndicho kitu alichokipenda sana lakini lilipokuja suala la kufanya mitihani, Dylan alikuwa moto wa kuotea mbali.

“Nimebadili...”

“Umebadili nini?”

“Sitaki kuwa mchungaji...”

“Kwa nini?”

“Ninataka kuwa na fedha, niwe tajiri, niheshimike na nijulikane dunia nzima...” alisema Dylan.

“Kwa hiyo unataka kuwa nani?”

“Nataka niwe mcheza kikapu...”

“Unasemaje?”

“Ninataka kuwa mcheza kikapu mashuhuri duniani,” alisema Dylan.

Hicho ndicho alichokipata, wazo lake la kuwa mchungaji halikuwepo tena, kitu alichokifikiria kwa kipindi hicho ni kuwa mcheza kikapu hapohapo nchini Marekani. Urefu wake ulimpa moyo kwamba angefanikiwa kuwa miongoni mwa wachezaji mahiri hapo baadaye, alitaka ajulikane ila mbali na hiyo, alitaka kuwa na fedha, atajirike ili mama yake atoke katika maisha ya umasikini aliyokuwa nayo.

“Nitakuwa tajiri mama, nitakutoa hapa ulipo,” alisema Dylan huku akionekana kumaanisha alichokisema.

“Nitashukuru sana, nitafurahi kukuona ukifanikiwa,” alisema bi Leticia.

Siku ziliendelea kwenda mbele, pamoja na kusoma lakini hakuacha kucheza mpira wa kikapu. Mwili wake ulikuwa mwembamba sana hivyo akashauriwa kunyanyua vyuma, hilo wala halikuwa tatizo, akafanya hivyo kwa ajili ya kuongeza mwili.

Kutokana na kuupenda sana mchezo huo, akajikuta akisahau kabisa kusoma jambo lililomtia wasiwasi bi Leticia na walimu wengine lakini kitu cha ajabu kabisa, kwenye mitihani, namba yake ilikuwa ileile, namba moja.

Mpaka muda wa kufanya mtihani wa mwisho wa shule za sekondari ambapo kwa Tanzania ingekuwa kidato cha nne, Dylan aliingia ndani ya chumba cha mtihani kwa ajili ya kufanya mtihani huo na kuendelea na mambo yake.

Hakupenda kusoma, kitu alichokifikiria kilikuwa ni kucheza mchezo wa kikapu tu. Katika kipindi hicho ambacho mtihani ulikuwa ukifanyika ndiyo kipindi ambacho mashindano ya kikapu kitaifa kwa watu walio chini ya miaka kumi na nane yalikuwa yakifanyika.

Alifanya mitihani harakaharaka ili awahi nyumbani kucheza katika timu yake ya mitaani kwani kupitia michezo hiyo, kulikuwa na mawakala mbalimbali waliokuwa wakifika na kutafuta wachezaji kwa ajili ya kuwapeleka ligi kuu.

“Vipi? Nilisikika upo kwenye mtihani!” alisema rafiki yake.

“Ndiyo! Nimefanya harakaharaka ili niwahi...”

“Mmh!”

“Usijali, nitafanya vizuri...” alisema Dylan.

Mashindano hayo yalikuwa na umuhimu mkubwa sana kuliko masomo yake, japokuwa alikuwa na uwezo mkubwa darasani, hakupanga kuwa mwanasheria au daktari, kitu alichokitaka ni kuwa miongoni mwa wachezaji kikapu wenye majina makubwa duniani, atengeneze fedha na kuwa bilionea mkubwa, yote hiyo ilikuwa ni sababu ya umasikini mkubwa aliokuwa nao mama yake.

Mashindano hayo yaliyojulikana kama Underground Bassketball U18 yalipoanza, watu wengi wakavutiwa, wakaanza kuyafuatilia katika kila mechi iliyokuwa ikifanyika. Watu wengi walikuwa wakijaa katika viwanja vilivyokuwa vikitumika kwa ajili ya mashinano hayo na kuangalia mechi hizo.

Hapo ndipo Dylan alipoanza kupata jina, alikuwa shujaa wa timu yake ya mtaani iliyojulikana kwa jina la Cobra, alikuwa na uwezo wa kuruka juu na kufunga pointi mfululizo. Kutokana na umahiri huo.

Dylan akaanza kufagiliwa na wanawake wengi, kila timu yake ilipokuwa ikicheza, wasichana waliongezeka, walichotaka ni kumuona huyo Dylan ambaye tayari alikuwa gumzo tena huku taarifa za chini zikisema kwamba tayari wakala wa timu ya kikapu ya Chicago Bulls iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Kikapu ya NBA nchini humo aliongea na kocha wa timu hiyo ya kina Dylan kwa ajili ya kumsajiri mchezaji huyo.

Maisha ya kimasikini yalimpiga mno, hakutaka kuendelea kuishi huko, aliwaona watu wakiwa na fedha, walitembelea magari ya kifahari na kuyabadilisha kadiri walivyotaka. Aliyapenda maisha hayo lakini hakuwa na jinsi, hakuwa na uwezo na kitu pekee alichokihitaji kwa wakati huo kilikuwa ni pesa tu hata kama umri wake ulikuwa mdogo.

Aliposikia tetesi kwamba kulikuwa na mawakala wa timu mbalimbali za kikapu ambao walifika mahali hapo, akaongeza juhudi, hakutaka kuishia hapo, alicheza kwa nguvu kubwa kwani kwake hiyo ilionekana kuwa kama nafasi ya mwisho ambayo kama angeipoteza basi asingeweza kuipata tena.

Alifunga pointi nyingi, aliruka juu, tena kwa ustadi mkubwa na kwa kumwangalia ilikuwa rahisi kugundua kwamba Dylan angekuwa mchezaji mkubwa, mwenye jina kubwa hapo baadaye.

Mashindano hayo yaliendelea kwa takribani mwezi mzima, yalipomalizika, wachezaji wakaanza kuchukuliwa na timu mbalimbali lakini kwa Dylan, kuchukuliwa ilikuwa ngumu sana.

Alishangaa, hakuelewa ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea. Alicheza vizuri na kuwa mchezaji bora tena huku akiipa ubingwa timu yake, sasa kwa nini hakupata hata nafasi ya kuchukuliwa na timu moja kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine.

“Tatizo?” alimuuliza kocha wake.

“Subiri, usiwe na presha...”

“Lazima niwe nayo! Nimekuwa mchezaji bora, nimeipa timu ubingwa, yaani hata kuuliziwa sijauliziwa kweli! Kuna nini?” aliuliza Dylan huku akionekana kuchanganyikiwa.

Machozi yalimlenga, moyo wake uliumia mno, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea, alijitoa sana katika mashindano hayo lakini mpaka katika kipindi hicho, mambo yalikuwa kimya kabisa.

Hakutaka kubaki hivihivi, muda ulizidi kwenda, alichokifanya ni kuanza kuulizia tatizo lilikuwa nini. Jibu alilolipata ni kwamba tangu mchezo wa kwanza alioucheza, kila mtu alivutiwa naye, timu sita za Ligi Kuu ya NBA zilimwania na walichokifanya viongozi wa timu yake ya mtaani ni kuangalia yupi alikuja na fedha nzuri.

Hicho ndicho kilichokwamisha, wote walitaka kupata fedha nyingi pasipo kujua ni kwa jinsi gani kukataa kwao kusaini mkataba wa kukubali kumuuza ulimuumiza moyoni mwake.

Dylan alipogundua hilo, akashinikiza kuuzwa, kila siku alikuwa ofisini kwa kocha wake, alimwambia wazi kwamba alikuwa kijana masikini ambaye alimuahidi mama yake kwamba ni lazima apambane ili apate fedha na kuyabadilisha maisha yao na hakukuwa na kitu alichokitegemea kuyabadilisha maisha yao zaidi ya kucheza kikapu kwa nguvu zote.

“Hilo nalifahamu Dylan...” alisema kocha wake.

“Tatizo nini sasa?”

“Hii ni biashara, tunaangalia fedha...”

“Kwa hiyo sitouzika?”

“Ndiyo tunawasikilizia waongeze fedha...” alisema kocha huyo.

Moyo wa Dylan ukawaka kwa hasira, hakuona umuhimu wa kuitumikia timu hiyo na wakati ilimzuia hata kumuuza kwa kisingizio cha kuhitaji fedha zaidi. Hakutaka kubaki ofisini humo, alichokifanya ni kuondoka, aliondoka kimasihara sana, wakahisi kwamba kesho yake angerudi lakini huo ndiyo ukawa mwisho wa kurudi katika timu hiyo, akapotea na hata alipofuatwa na uongozi wa timu, aliwaambia wazi aliamua kuachana na masuala ya mchezo wa kikapu.

Yalikuwa ni maamuzi magumu, yalimuumiza lakini hakuwa na jinsi, alitaka kuyabadilisha maisha ya familia yake, aliuchukia mno umasikini, alimchukia mtu yeyote ambaye alisimama mbele yake na kumzuia kupata mafanikio aliyoyataka maishani mwake.

Wiki mbili baada ya kuondoka katika timu hiyo ndipo wakapokea barua kutoka shuleni kwamba Dylan alitakiwa kwenda katika ikulu ya Marekani kwa ajili ya kuzungumza na rais kutokana na kufaulu vizuri katika masomo yake.

Wote walibaki wakimwangalia Dylan, alifana mno na Bwana James kiasi kwamba wakaamini maneno kuwa kweli duniani kulikuwa na watu wawili-wawili. Kwa Catherine, mbali na mfanano aliokuwa nao kijana huyo, akahisi moyo wake ukianza kumpenda, kila alipomwangalia alihisi kabisa kuwa na mapenzi mazito moyoni mwake.

Hakujua kama kweli yalikuwa mapenzi ya kweli au kwa sababu mvulana huyo alikuwa na akili nyingi zaidi yake. Kila alipomwangalia, aliachia tabasamu pana.

“Ninamshukuru Mungu kwa hatua hii niliyofikia, huwa niliamini kwamba mafanikio yangu yapo kwenye mchezo wa kikapu, nikaweka tegemeo langu huko kabla ya viongozi wa timu kukataa kuniuza bila kujali ni umasikini wa aina gani unaitafuna familia yangu. Mbali na mchezo wa kikapu, kumbe kuna sehemu nyingine naweza kufanikiwa, naahidi kupambana, nitakuwa mfanyabiashara mkubwa sana hapa,” alisema Dylan, japokuwa alitoa tabasamu pana, lakini wengi waligundua kwamba tabasamu hilo halikuwa kutoka moyoni.

Akakabidhiwa zawadi yake na kuteremka. Alishindwa kuvumilia, machozi yakaanza kumtoka machoni mwake, aliumia mno, kila alipofikiria maisha aliyokuwa akipitia na mama yake, alihisi kwamba dunia haikuwa na usawa kabisa.

Sherehe iliendelea, watu walikunywa, kila mmoja mahali hapo alionekana kuwa na furaha kubwa isipokuwa watu wawili tu, Dylan na mama yake. Watu hao wawili walionekana kuwa na majonzi, leo hii walikuwa katika jumba kubwa, lililokuwa likiheshimiwa duniani lakini kila walipofikiria kwamba mara watakapotoka ndani ya jumba hilo walitakiwa kwenda kwenye nyumba yao ya kawaida, hakika mioyo yao iliumia mno.

“Habari yako...” Dylan alisikia sauti kutoka nyuma yake, alipogeuka, macho yake yakatua kwa msichana mzuri wa sura, mwenye uso wa tabasamu pana, alikuwa Catherine.

“Safi mrembo, karibu...”

“Asante! Hongera sana, sikufikiria kama kungekuwa na mtu mwenye akili kama zako,” alisema Catherine huku akiliachia tabasamu pana usoni mwake, Dylan akazidi kuchanganyikiwa.

“Kweli?”

“Ndiyo!”

“Asante sana...”

“Inaelekea unasoma sana?”

“Hapana! Sikumbuki mara ya mwisho kujisomea ilikuwa lini, labda nilipokuwa mdogo,” alisema Dylan.

“Mmh! Basi hongera zako!”

Catherine alijitahidi kuzungumza na kijana huyo, alitaka kumzoea kwa ukaribu, alizungumza naye huku muda wote akionekana kuwa mwenye furaha tele. Walipoona wamezoeana vya kutosha, Catherine akamchukua Dylan na kwenda kumtambulisha kwa mama yake kama rafiki yake mpya ambaye mwanamke huyo aliukubali urafiki huo kwa moyo mweupe.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa urafiki wao, mara kwa mara walikuwa wakichati kupitia simu zao, kila mmoja alimpenda mwenzake lakini hakukuwa na mtu aliyekuwa tayari kumwambia mwenzake kwamba alimpenda kwa moyo wa dhati.

Catherine alimuogopa Dylan, hakuamini kama mvulana huyo angekubali kuwa wake, hakujiamini kabisa, kila alipomfikiria, alihisi kabisa moyo wake ukiwa na hofu kubwa hivyo kupotezea ila kwa upande wa Dylan, aliogopa kumwambia msichana huyo ukweli kwa sababu tu kwa muonekano wake alionekana kuwa mtoto wa tajiri ambaye hakustahili kabisa kuwa naye.

Urafiki huo ukaendelea mpaka walipoingia chuoni, kwa miaka miwili, hawakuwa wameonana tena, kazi kubwa waliyokuwa wakiifanya ni kuwasiliana kwenye simu tu. Wakati Dylan akifaulu mtihani wake na kujiunga na Chuo cha Boston University School of Business kilichokuwa Massachusetts kwa ajili ya kuchukua masomo ya kitabibu huku Catherine akijiunga na Chuo Kikuu cha Harvard kilichokuwa hukohuko Massachusetts na kuchukua masomo ya sheria.

Hiyo ilionekana kuwa nafasi yao ya kuonana, wote walikuwa katika jimbo moja japokuwa vyuo vilikuwa mbalimbali mno lakini wakapanga kwamba ilikuwa ni lazima waonane kwani kwa kufanya hivyo ukaribu wao ungekuwa mkubwa na kuzoeana zaidi.

Kwa kuwa mchezo wa kikapu ulikuwa kwenye damu yake, Dylan akapata wakati mgumu sana, kila alipowaona watu wakicheza katika timu ya chuo, akapata hamu ya kutaka kucheza nao.

Hakukuwa na mtu aliyejua uwezo wake, wengi walipomuona, walimdharau na kumtania alikuwa na urefu wa bure na wakati hakuwa na uwezo wowote ule katika kucheza mpira wa kikapu.

Maneno hayo yalimkwaza sana lakini aliendelea kuvumilia mpaka pale alipoona kwamba uvumilivu umemshinda hivyo alitakiwa kuwaonyeshea watu hao yeye alikuwa nani katika mchezo huo.

Alipoomba kujiunga na timu ya chuo kwa upande wa mchezo wa kikapu, wengi walimpuuzia, walimdharau kwa kumuona hajui lakini alipopewa nafasi, kila mtu alishika mdomo kwa mshangao, katika maisha yao, hawakuwahi kumuona mchezaji aliyekuwa na uwezo mkubwa kama aliokuwa nao Dylan.

Siku hiyo alipoonyesha uwezo mkubwa uwanjani, wasichana wakashindwa kuvumilia, wengi wakaanza kujigonga huku wakitamani mvulana huyo atoke nao kimapenzi. Hilo lilikuwa suala lililomnyima furaha sana Dylan, hakutaka kuwa na msichana yeyote, katika maisha yake kipindi hicho, alihitaji kuwa peke yake kwani hakukuwa na kitu alichokipenda kama kutokuwa na msichana yeyote.

Hakuwahi kufanya mapenzi na msichana yeyote na wala hakuwahi kuwa kwenye uhusiano na msichana yeyote yule, kile alichokipenda moyoni mwake ni kuwa peke yake tu, alijitahidi kusoma, kucheza kikapu ili mwisho wa siku kufanikiwa na kuwa bilionea.

“Catherine.....” aliita Dylan kwenye simu.

“Nipo hapa...”

“Kuna kitu nataka kukwambia....”

“Kitu gani tena...”

“Ooh! Au basi...”

“Hapana! Niambie kitu gani!’

“Kuna kitu kinanisumbua tangu utotoni, sina raha nacho kabisa, kinanitesa na kuniua moyoni mwangu,” alisema Dylan kwa sauti ya chini.

“Kitu gani jamani?”

“Nikuulize swali?”

“Niulize...”

“Unanipenda?”

“Ndiyo, tena sana...”


ITAENDELEA

No comments:

Featured Post

 SOMA SIMULIZI ZENYE KUSISIMUA HAPA A. UTAJIRI WENYE UCHUNGU     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-1     UTAJIRI WENYE UCHUNGU-2      UTAJIRI WENYE UCH...